Kaachishwa Mume Wa Kwanza Mahakamani Na Wazee Wake Na Sasa Kaolewa Na Mume Mwengine Na Yule Mume Wa Kwanza Anasema Bado Ni Mkewe

SWALI:

 

Namshukuru ALLAH (S.W) kwa kunipa FURSA Hii adhimu  ya kuuliza swali langu hili. ISHAALLAH ALLAH (S.W), Akulipeni kheri zake, kwa jitihada zenu ISHAALLAH.

Swali langu ni hili; Nina ndugu yangu aliolewa na mume wa kwanza bila ya mafahamiano mazuri na wazee wake. Baadae yule mume alipata matatizo akafungwa jela. Ingawa alikuwa akishughulikiwa na mume wake, Wazee wake waliamua kumuachiza mahakamani, na kumuoza mume mwengine. Yule mume wa kwanza kahamaki na kusema yeye hayuko radhi na anajua kuwa bado ni mkewe, Sasa ndugu yetu yuko njia panda, AFANYE NINI?   Tunaomba msaada wenu ISHAALLAH.


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu mke kuachishwa na wazee.  

Swali lako linazua maswali kadhaa kutokana na kutokuwa wazi. Je, wazee walipotaka kumuachisha walikwenda mahakama gani? Je, walikwenda mahakama za Qaadhi au mahakama za serikali? Ikiwa walikwenda mahakama za kiserikali kutakuwa hakuna talaka hapo.

Ikiwa walikwenda mahakama za Qaadhi inaweza kuwa talaka imepita ikiwa Qaadhi alitumia njia nzuri ya kutatua tatizo hilo kwa kumuita mume ili aweze kusikiliza pande zote mbili. Tufahamu kuwa katika Uislamu talaka inatoka kwa mume na sio kwa mke wala wazazi wala mahakama. Mahakama za Qaadhi zinaingilia kati ikiwa mke mwenyewe atataka kujitoa katika ndoa au mume ana shida na mke anaona hawezi kuketi na mume katika hali hiyo.

Ikiwa njia za sawa hazikutumiwa na inaonyesha hivyo ndivyo ilivyokuwa kulingana na swali lako.

Hivyo, dada yako huyo atakuwa ni mke wa mume wa kwanza ikiwa Nikaah halali ilifungwa. Kwa minajili hiyo, dada yako atakuwa anazini na huyu mume wa pili kwa kuwa bado ni mke wa mtu.

Ikiwa ndoa ya kwanza haikuwa sawa kishari’ah kwa kukosekana idhini ya walii ambaye ni baba. Wanandoa hao walikuwa wakizini na hii ndoa ya pili itakuwa ndiyo ya sawa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share