Hukumu Ya Kufunga Siku Ya Jumamosi Pekee
SWALI
Shukran kwa kazi zenu munazofanya kuelimisha umma.
Tumeelezewa kwamba haifai mtu kufunga saum ya sita katika siku ya jumamosi, je hii ni sawa. Je ikiwa nafunga saum ya 13, 14 & 15 ikiangukia jumamosi nifunge au vipi? Shukran
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Ahsante
Utata huu umesababishwa na kufahamika Hadiyth hii kuwa ni ya makatazo katu, nayo inasema:
Kutoka kwa 'Abdullaah bin Busr kutoka kwa kaka yake kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Msifunge siku ya Jumamosi isipokuwa ikiwa mmefaridhiwa na Allah kwenu. Ikiwa mtu hakupata chochote cha kula isipokuwa ganda la zabibu au gome la mti, basi alitafune)) [at-Tirmidhy, Abu Dawud, an-Nasaaiy, Ibn Maajah, Ahmad na al-Haakim). Al-Haakim anasema kuwa hii ni Hadiyth Sahihi kulingana na sharti za Muslim na at-Tirmidhy akasema ni Hasan]
Wanaokataa kufunga kwa siku hiyo wanategemea Hadiyth hiyo.
Wale wanaosema kuwa inawezekana kufunga siku hiyo wanategemea Hadiyth zifuatazo. Miongoni mwazo ni: Abu Dharr (Radhiya Allahu 'anhu) amesema:
"Mtume wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru kufunga siku tatu katika kila mwezi – yaani masiku meupe, ambapo mwezi unakuwa umekamilika (tarehe 13, 14, na 15 katika miezi ya Kiislamu). Na akasema kufanya hivyo ni sawa na kufunga milele” (An-Nasaaiy na Ibn Hibbaan, ambaye amesema ni Sahihi).
Wanachuoni wanasema kuwa hii ni kauli ya kijumla katika kufunga siku hiyo na huenda Jumamosi ikaangukia moja ya terehe hizo. Na pia ipo Hadiyth ambayo inatupigia mfano wa funga ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika suala
Amesema ‘Abdullaah bin ‘Amr bin al-‘Aas (Radhiya Allahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:
“Funga inayopendeza zaidi kwa Allah ni funga ya Nabii Dawud … alikuwa anafunga siku moja na anakula siku moja” (Al-Bukhariy, Muslim na an-Nasaaiy).
Hii ni Hadiyth ndefu ambayo inapatikana katika Riyaadhus Swaalihiyn cha Imam an-Nawawiy, Hadiyth Namba 150. Jambo ambalo linaweza kupatikana katika kufuata Sunnah hii ya funga ambayo ni bora kabisa ni lazima baada ya kila wiki mbili utakuwa ni mwenye kufunga siku ya Jumamosi. Na ikiwa aina hii ya funga imeitwa ndiyo funga bora na Mtume wa Allah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tutaweza kuitekeleza namna gani?
Juawyriyah bint al-Haarith, Mama wa Waumini anatuhadithia:
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinitembelea Ijumaa siku ambayo ilikuwa nimefunga, akaniuliza: “Je, ulifunga jana”. Nikasema: “Hapana”. Akauliza tena: “Je, una nia ya kufunga kesho?” Nikasema: “Hapana”. Akasema: “Basi fungua”. Katika riwaya nyingine: “Alimuamuru afungue, naye akafungua” (Al-Bukhaariy).
Na katika Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Usifunge siku ya Ijumaa mpaka uwe umefunga siku kabla yake au siku inayofuata” (Al-Bukhaariy na Muslim).
Kwa hiyo hapa inaonesha kuwa siku inayofuata baada ya Ijumaa ni Jumamosi.
Imepokewa kwa Abu Qataadah (Radhiya Allahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kufunga siku ya ‘Arafah kunafuta madhambi ya miaka miwili; iliyopita na ijayo. Na kufunga siku ya ‘Aashuraa kunafuta madhambi ya mwaka uliopita” (Jama‘ah isipokuwa na Al-Bukhaariy na at-Tirmidhiy).
Wale wenye rai ya kuwa unaweza kufunga Jumamosi wanasema kuwa hii ni kauli ya kijumla kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kufunga siku ya ‘Arafah na ‘Aashuraa siku yoyote itakayokuwa ikiwa ni Jumamosi, Jumapili au siku nyingine yoyote. Na ikiwa hutafunga basi utakuwa umekosa fadhila kubwa
Kuhitimisha ni kuwa tunanukuu kauli ya Imam At-Tirmidhiy ambaye amesema inachukiza kwa mtu kuihusisha siku ya Jumamosi kwa kufunga kwani ni siku ambayo inatukuzwa na Mayahudi. Na hii ndiyo kauli ya wanachuoni wa awali na pia wa sasa.
Madhehebu ya Ki-Hanafi, Ki-Shafi‘iy na Hanbali wanasema kuwa inachukiza kufunga siku ya Jumamosi peke yake kulingana na dalili zilizotolewa. Imam Maalik ametofautiana nao kwa kusema unaweza kufunga Jumamosi yoyote unayotaka lakini Ahaadiyth tulizoona ni dalili dhidi ya rai yake hiyo.
Na Allaah Anajua zaidi
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


