SWALI:
Assalamu alaykum,
Kuna Wanaojiita waalimu wanumuambia mgonjwa una majini wahitaji kutolewa, baada ya kukusomea anamwambia mgonjwa kama amevaa pete azitowe azitie kwenye kijitunga na nguo mbili hivi anazozipenda
Vipi mambo haya??
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani kwa swali lako kuhusu hao wanaojiita waalimu kuwalisha yamini wagonjwa kwa wanavyovitoa.
Hakika ni kuwa waalimu hawafai kupatiwa vitu
Ni nasaha kwetu kwa Waislamu wanapokuwa wagonjwa na ikashukiwa kuwa amekumbwa na jini basi aende kwa Mwalimu au Shaykh Muislamu mwaminifu na mcha Mngu ambaye atamsaidia na wala sio yule mwenye kumuingiza katika shirki ya aina moja au nyengine.
Hao ‘Maalim’ na ‘Maustaadh’ au ‘Mashekhe’ wa aina hiyo uliowataja, ni wale watu wadanganyifu na wasio na Iymaan ambao labda wanajua Aayah chache na kuzitumia kudanganyia watu ili kupata chakula chao na kushibisha njaa zao. Yote inasababishwa na watu kutotaka kujituma na kufanya kazi na kubuni hila na njia za mkato za kuwapatia chumo rahisi la haraka.
Wapo wengine pia wenye kuwatengenezea Waislamu makombe na kuwafungia baadhi ya Aayah na maneno ya Kiarabu yasiyojulikana ili ziwakinge. Na kuna wengine waliojenga majumba na kutajirika kwa kazi kama hizo za kuwadanganya Waislamu dhaifu wajinga wasiojua Dini
Ni muhimu Waislamu wajihadhari na mashekhe na maalim na maustaadh waongo
Na Allaah Anajua zaidi.