Vipi Atajua Kama Kapatwa Na Jicho Au Uchawi?

 

SWALI:

 

Assalam aleikum warahmatullah! Nimesoma hadith isemao alikua mtume alayhiswalat wassalam akiamrisha tujizungue na jicho! Hii hadith yatupa faida kiwango gani? Nifaidisheni! Na mtu anaposomewa aya ama hadith zenye dua za ruqya kitu gani kinajulisha kama hii ni ain ama sihr?? Kwa sababu nimepata hadith yasema jicho laingiza  watu kaburini ama ngamia sufuriani! Natatizika nitatulieni shukran


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupatwa na jicho au uchawi.

Hapa hapana utata kabisa kwa kuwa kila kitu kipo wazi. Mtu aliyepatwa na husuda ya jicho au uchawi anajulikana kwa njia rahisi. Mwanzo aliyerogwa tabia yake inabadilika kabisa kwa kiasi anaweza kuhisi amefanya kitu na kumbe hajafanya. Kwa kusomewa Aayah za Ruqyah, jini aliyetumiwa huwa anajitokeza na kuanza kuzungumza. Katika kufanya hivyo, mwenye kuzingua zunguo hilo la shari’ah anazungumza naye ili apate ufumbuzi wa sihri hasa aliyofanyiwa. Baada ya kusema kilichofanywa kama vile ilivyoripotiwa katika Al-Bukhaariy na Muslim, alipokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefanyiwa sihri. Vile vitu vilivyotiwa kisimani na Labiyd bin A’swam, Myahudi, vilikwenda kutolewa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapona na kuwa mzima kabisa.

 

Ama kijicho basi huwa mtu anabadilika kama vile kutosikia vizuri au kutoweza kula na mengine. Kwa kusomewa, mtu kama huyo huwa hatingishiki wala jini kuzungumza kwa niaba yake. Kwa hiyo, hiyo Ruqyah litamsaidia kujinasua na kijicho hicho.

 

Kwa hali zote, inatakiwa sisi tujilinde na kujikinga na kupatwa na Shaytwaan au kijicho kwa kusoma asubuhi, jioni na wakati wa kulala kinga mbili, yaani Suratul Falaq na an-Naas mara tatu tatu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share