Nifanye Nini Ili Niweze Kuipata Simu Yangu Iliyoibiwa Na Pia Iwe Fundisho Kwa Wezi Bila Ya Mimi Kuingia Katika Shirki?

SWALI

Asalaam alaykum warahmatulahi wabarakatuh mimi ni muislam nasoma chuo cha ualimu mhonda kiko morogoro, nimeibiwa simu ya mkononi ambayo niliipenda sana na niliinunua kwa gharama ya shilingi laki mbili na elfu ishirini, sasa simu hii imeibwa na mwanachuo mwenzangu hapa chuoni japo simjui hasa ni nani.

wako watu walionishauri niende kwa waganga wa kienyeji nikaona ni moja ya madhambi makubwa ambayo allah ameyakemea sasa nauliza nisome dua gani au nifanyeje ili simu yangu irudi na pia iwe fundisho kwani kuna  wimbi la wizi sana. Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya, na ninajivunia alhidaya.

ALHIDAYA INAWAKUTANISHA WAISLAMU


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu ufanye nini ili uipate tena simu yako uipendayo.

Hakika ni kuwa hakuna kisomo chochote ambacho Muislamu anaweza kusoma ili kukirudisha kitu chake kilichoibiwa.

Kitu cha pekee ambacho unaweza kufanya ni kumuomba Allaah Aliyetukuka kwa uwezo wake ulio mkubwa Akusahilishie kuipata kutoka kwa aliyeiba kwa njia Anayoitaka Yeye Mtukufu. Na jingine ni kumuombea aliyeiiba kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Du’aa ya aliyedhulumiwa hairudi”.

Mbali na hayo, unatakiwa kama Muislamu uchukue tahadhari za ziada katika kuchunga mali zako. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akufanye ni mwenye kuipata simu yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share