Wanakufurisha Ahlus Sunnah Na Waislamu Wote Wasiokubali Maimaam Wao

 

Wanakufurisha Ahlus Sunnah Na Waislamu Wote Wasiokubali Maimaam Wao

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’aiy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) Aliridhika

 

Shia wa mwanzo hawakuwa wakiwalaani wala kuwakufurisha Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ninaamini kuwa wakati wa ‘Umar na wakati wa Abu Bakr na wakati wa ‘Uthmaan hapakuwa na aliyeukanusha ukhalifa wa yeyote kati yao, lakini baada ya kufariki ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) walikuwepo waliokuwa wakiona kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alistahiki zaidi Ukhalifa kuliko ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhum), na haya yalionekana katika uchaguzi uliosimamiwa na ‘Abdur-Raahman bin ‘Awf (Radhwiya Allaahu ‘anhu) baada ya kufariki Khalifa wa pili ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), wakati nusu ya umma walipomchagua ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na nusu nyingine walimchagua ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum), lakini ‘Aliy aliridhika wakati ‘Abdur-Rahmaan alipomchagua ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhum) awe Khalifa wa tatu wa Waislamu.

 

Na dadili ni kauli ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika kitabu maarufu cha Shia, Nahju Al-Balaaghah aliposema:

 

"Kwa Muawiyah:

 

 

Bisimillaahir Rahmaanir Rahiym,

 

Amma baad, kwa vile watu wote wamefungamana nami katika mji wa Madiynah, basi nawe pia uliyeko huko Shaam (Syria) unalazimika kufungamana nami. Na hii ni kwa sababu watu waliofungamana nami ni wale wale waliofungamana na Abu Bakr na ‘Umar na Uthmaan. Kwa hivyo aliyehudhuria hana haki ya kulikataa na asiyehudhuria hana haki ya kulipinga. Kwa hakika ushauri ni wa Muhaajiriyn na Answaar (Watu wa Makkah na wa Madiynah). Wanapokubaliana wote juu ya mtu na kumchagua kuwa Imam wao, na Allaah Anaridhika na uchaguzi wao.

 

Nimemtuma kwako Jariyr, naye ni katika watu wa Imani na watu waliohajir, kwa hivyo fungamana nami - Walaa quwwata illa billaah!".

Nahjul-Balaaghah- uk. 427 mlango wa 6

 

Inashangaza kuona kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe aliridhika na uchaguzi Alioridhika nao Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) (kama alivyosema), wakati wapo wanaowakufurisha Waislamu kwa sababu na wao pia wameridhika na alichoridhika nacho (‘Aliy Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Hitilafu ilikuwepo juu ya nani aliyestahiki kutawala baina ya ‘Uthmaan na ‘Aliy, na baada ya kuchaguliwa ‘Uthmaan, wote waliridhika na uchaguzi huo akiwemo ‘Aliy mwenyewe (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Lakini hitilafu haikufikia daraja ya kukufurishana na kulaaniana, na kugeuza uchaguzi wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni wahyi ulioteremeka kutoka mbinguni, na kwamba kila asiyeamini kuwa ‘Aliy ni Imaam wa mwanzo keshakuwa kafiri aliyelaaniwa. Jambo hili linatushangaza sana na kutustaajabisha.

 

 

Kila Asiyekuwa Shia Ni Kafiri

 

Hebu tuisome kauli ya Muhammad bin ‘Aliy Al-Hussayn bin Baabawayh Al-Qummy maarufu kwa jina la As-Saduuq katika maudhui haya, na huyu ni katika maulamaa wakubwa wa Kishia aliposema:

 

‘Itikadi yetu ni kuwa mtu yeyote asiyeamini uimamu wa Amiri wa Waislamu ‘Aliy bin Abi Twaalib na imamu waliofuata baada yake (‘Alayhim-salaam) mfano wao ni mfano wa wenye kuukanusha utume wa manabii wote. Na itikadi yetu juu ya mwenye kumuamini Amiri wa Waislamu kisha akamkanusha yeyote kati ya imamu wengine waliokuja baada yake anakuwa katika daraja ya mwenye kuwakanusha manabiy wote kisha akaukanusha utume wa Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).’

 

Risaalat al-I’itiqaadaat Uk. 103

 

Kisha hapo hapo akanukuu hadithi iliyonasibishwa na Imam As-Swaadiq kuwa eti amesema: ‘Mwenye kumkanusha wa mwisho wetu ni sawa na mwenye kumkanusha wa mwanzo wetu.’

 

Risaalat al-I’itiqaadaat ukurasa 103

 

Yusuf Al-Bahrani katika encyclopedia yake ijulikanayo kwa jina la Al-Hadaaiq an-Naadhirah fiy ahkaam al-‘Itwrah at-Twaahirah uk. 153, juz. 18 amesema:

 

‘Pana tofauti gani baina ya mwenye kumkufuru Allaah na mwenye kuwakataa imamu (‘Alayhim-salaam) baada ya kuthibiti kuwa Uimamu ni asili ya dini.’

 

Na mwanachuoni maarufu na mfasiri wa Qur-aan wa Shia Al-Faidh al-Kashaaniy naye amesema:

 

‘Mwenye kumkataa Imamu yeyote anakuwa mfano wa mwenye kuwakataa Manabiy wote.’

Minhaaj an-Najaat uk.48

 

Anasema pia Al-Mullah Muhammad Baaqir al-Majlisiy:

 

‘Jua ya kwamba anaitwa mshirikina na kafiri kila asiyeamini uimamu wa Amirul Muuminiyn na imamu wa vizazi vyake (‘Alayhis-salaam) na akawafadhilisha wengine, ni dalili kuwa hao ni watu wa Motoni watabaki humo milele.’

Bihaar Al-Anwaar 390/23

 

Ndugu zangu Waislamu, kauli hizi zinamaanisha kuwa yeyote asiyekuwa Shia Ithnaashari basi huyo ni kafiri aliwakanusha Rusuli na kuikanusha asili ya dini, na ataingia motoni na kubaki humo milele, naye ni sawa na aliyemkufuru Allaah!!

 

 

Naaswib Kwa Mashia Maana Yake Ni Sunni

 

Anasema Al-Qummiy (As-Swaduuq) katika kitabu cha Ilal ash-Sharaai’a kutoka kwa Daud bin Farqad kuwa amesema:

 

’Nilimuuliza Abu ‘Abdillaah ‘Alayhis-salaam (Ja’afar As-Swaadiq, Imamu wa Sita wa Mashia): ‘Unasemaje juu ya Naaswib? (Sunni). Akasema: ‘Damu yake ni halali lakini uwe na tahadhari. Kama utaweza kumuangushia ukuta au kumzamisha katika maji itakuwa bora ili asiweze kushuhudia dhidi yako, basi fanya hivyo, nikamuuliza: ‘Na vipi juu ya mali yake.’  akasema; ‘Chukua kiasi unavyoweza kuchukua.’

 

Anasema Al-Kulayni katika kitabu maaarufu sana cha Mashia, Al-Kaafi kutoka kwa Muhammad bin Muslim kuwa eti alisema:

 

‘Nilipoingia nyumbani kwa Abu ‘Abdillaah (Ja’afar As-Swaadiq) nilimkuta Abu Haniyfah akiwa pamoja naye, nikamuambia (Ja’afar): ‘Nafsi yangu ni mhanga kwa ajili yako, niliota ndoto ya ajabu.’ Akasema: ‘Ee mwana wa Muslim, tuhadithie kwani mjuzi wa jambo hilo (huyu) amekaa. ’Akamuashiria kwa mkono wake Abu Haniyfah. Akasema: ‘Nikasema, nimeota kama kwamba nimeingia nyumbani nikamuona mke wangu amenitokea huku akivunjavunja lozi nyingi kisha anazipukutisha juu ya mwili wangu, nikashangazwa na ndoto hii.’ Akasema Abu Haniyfah: ‘(maana ya ndoto yako ni kuwa) Wewe utashindana na kujadiliana na wabaya katika warithi wa ‘aila yako, na baada ya tabu kubwa utapata haki yako katika urithi In Shaa Allaah.’ Akasema Abu ‘Abdillaah (Jaafar As-Swaadiq): ‘Umesibu sawa sawa Wa-Allaahi ee Abu Haniyfah.’ Kisha Abu Haniyfah akatoka na kwenda zake, nikamuambia (Ja’afar As-Swaadiq): ' Nafsi yangu ni mhanga kwa ajili yako, mimi sijapendezewa na majibu ya Naaswib huyu (Sunni huyu).’ Akasema: ‘Ee mwana wa Muslim, Allaah Asikuletee maudhi, kwani ibara zao hazifanani na ibara zetu, wala ibara zetu hazifanani na ibara zao, na si kweli alivyosema.” Nikamuambia: ‘Lakini ulimwambia kuwa amesibu na ukaapa kwa jambo hilo wakati yeye amekosea? ‘Akasema: ‘Ndiyo niliapa kwa jambo lile nikikusudia kuwa amesibu katika kukosea.” Nikamuambia: ‘Nini taawiyl yako juu ya ndoto hiyo?’ akasema: ‘Ee mwana wa Muslim, hakika wewe utafunga ndoa ya mut’ah na mwanamke, na mke wako atakuja kujua atakuchania nguo zako.’

Al-Kaafi juz.8 uk.212

 

Abu Haniyfah ambaye ni mmoja katika maimaam wanne walio maarufu zaidi wa Ahlus Sunnah, anajulikana kuwa alikuwa mtu aliyekuwa akiwapenda sana watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa mara kwa mara akiwazuru na kuzungumza nao. Lakini watu wasioutakia kheri umoja wa Waislamu wamezuwa hadiyth hii na kumuita kuwa yeye ni Naaswib, na hawajasita hapo, bali walimsingizia uongo hata Imaam Ja’afar (Allaah Awe radhi nao wote) na Awaepushe mbali kabisa na uongo.

 

Kinachoshangaza zaidi si hadiyth hizi nilizozinukuu kutoka katika vitabu vya wakubwa wa ‘ulamaa wa Shia wanaotegemewa katika historia ya Shia na vinatangazwa sana na vimejaa kwenye tovuti zao nyingi na hata tovuti za maulamaa wao wakubwa wanaotegemewa zama hizi.

 

 

Tovuti ya Ayatollah As-Sistani (Ambaye Ni Marejeo Makubwa Ya Mashia Wengi Ulimwenguni Kwa Wakati huu)

 

Kinachoshangaza hasa ni kuwa baadhi ya vitabu hivi vimewekwa katika tovuti (website) ya Ayatollah As-Sistani.

 

Dr. Muhammad Al-Hashimi mwendeshaji wa channel ya TV ya Al-Mustaqillah aliwahi mara nyingi kumuandikia Ayatollah As-Sistani akimuomba aviondoe vitabu hivyo katka website yake, lakini hakupata majibu yoyote kutoka kwake, na niliwahi kumsikia akihojiana na Ayatollah Al-Qazwiyniy akimuomba amfikishie salamu zake kwa As-Sistani, lakini Qazwiyniy badala ya kumkubalia alianza kutoa shutuma mbali mbali kuwashutumu Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Share