Kundi La Jama’at At-Tabliygh (Masufi)

 Kundi La Jama’at At-Tabliygh (Masufi)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Asili Yake

 

Limeanzishwa kundi hili na Muhammad Ilyaas Kandhalvi mwenye asili ya India katika mji wa Kandhla, aliyenasibishwa na Madrasah kubwa katika mji huo, ijulikanayo kama Deobandi[1] , iliyoanzishwa tarehe 18 mwezi wa Muharam mwaka 1288H katika kijiji cha Deobandi nchini India. Nayo ni Madrasah kubwa inayofuata madhehebu ya Hanafiy, na aliyeanzisha Madrasah hii -kwa madai ya wafuasi wake- ni Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mbele ya Muhammad Qaasim Nanotvi; na kwa maelezo ya wafuasi hao, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akija na Swahaba na Khalifa zake katika hii Madrasah kwa ajili ya kudhibiti hesabu zake. [Al-Arwaah Ath-Thalaathah, uk. 434].

 

 

Muda alipoona Muhammad Ilyaas watu wengi wa kabila la Mewati kutoka katika jimbo la Mewat wanaoishi karibu na mji wa Delhi, India wako mbali na Uislamu na ni wenye kuchanganyika na waabudu mizimu na wamajusi, na ni wenye kujiita majina yao na kujipamba na mavazi yao, na wameoana nao, na haukubakia Uislam kwa watu hawa isipokuwa majina tu ya Kiislam; na ile dhana ya kuwa wao ni kizazi cha Kiislam tu basi, ni watu waliogubikwa na ujinga mkubwa.

 

 

Ghera ya dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ikamchukua na akakusudia kuwaendea mashekh zake na mashekh wa Twariyqah yake, mfano shekh Raashid Ahmad Gangohi, na shekh Ashraf ‘Aliy Thanwi, na akawashauri juu ya jambo hili (kuanzisha kundi la Tabliygh), baada ya kuifahamu fikra hii toka alipokuwa Hijaaz. Hivyo akaanzisha harakati ya kidini ya Tabliygh kwa amri ya shekh wake na kuelekezwa mikakati. [Dwaratu ‘Aaabirat I’tibaariyah uk. 7-8 cha shekh Sayfur-Rahmaan bin Ahmad Dahlawiy].

 

 

Anasema Muhammad Ilyaas: “Nimeamrishwa kufanya jambo hili nilipokuwa Madiytnatul-Munawwarah, na niliambiwa: Tutakutuma na kukukalifisha jambo.” [Mawlaana Ilyaas aur ankaa diiniy da’wat uk. 19].

 

 

Na anasema Al-Haaj ‘Abdur-Rahmaan: “Hakika shekh Muhammad Ilyaas hakuwa shujaa kufanya jambo isipokuwa pale alipoamrishwa na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndipo akafanya jambo hili.” [Irshaadaat wa Maktuubaat ash-Shaykh Muhammad Ilyaas uk. 35].

 

 

Anasema Muhammad Ilyaas: “Imenipambaukia Twariyqah hii ya Tabliygh na kupewa wahyi (ndoto) usingizini tafsiri ya Aayah:

 

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ ۗ  

Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah. [Aal-‘Imraan: 110]

 

 

Akaambiwa kuwa wewe umetolewa kwa ajili ya watu kama walivyotolewa Manabii; na kwa maana ya Aayah hii, kazi inahitaji misafara kuelekea miji mbalimbali, na kazi yako ni kuamrisha mema na kukataza  maovu; na akafahamishwa maana ya kipande cha Aayah (وَتُؤْمِنُونَ) kuwa iymaan yako itazidi na kama si hivyo basi itabakia kama ilivyo kwa maana ya kipande hiki (كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ)  na wala usikusudie kuongoka kwa watu wengine bali niyyah yako iwe kuinufaisha nafsi yako kisha akafahamishwa maana ya kipande hiki (أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ) kuwa umetolewa kwa wasiokuwa Waarabu. [Malfuudhwaat Muhammad Ilyaas, uk. 44].                                              

 

 

Na anasema tena Muhammad Ilyaas: “Mimi sikuweka misingi na kanuni za kundi hili kwa matakwa yangu, bali nimepewa na kuamrishwa kuzitekeleza na kuzifanyia kazi.” [Tabliyghiy tahriyk ibtidaai aur uskii banayaady uswuul, uk. 57].                                                       

 

 

Na katika ukurasa 56 kabla ya huu kitabu hicho hicho amesema mtunzi: Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) alimjuza shekh Ilyaas hii misingi ya kundi hili la Tabliygh.

 

 

Na anasema Miyaanjiy Muhammad ‘Iysaa: “Hii misingi ndiyo Allaah Aliyompa shekh Muhammad Ilyaas kwa ilhaam, na alikuwa shekh Muhammad Yuusuf akiichunga misingi hii, na alikuwa hafuati rai yake mbele ya shekh Muhammad Ilyaas. Basi ni juu ya kila amiri katika ma-Amiri wa Jama’at At-Tabliygh kuweka jambo hili (la kufuata misingi ya kundi hili iliyowekwa na shekh Muhammad Ilyaas) mbele ya macho yao. [Tabliygh ka maqaamiy kaam ‘Al-‘Amal Al-Baliygh Al-Mahaliy’) uk. 7-12].

 

 

Na anasema shekh Sayfur-Rahmaan bin Ahmad Dahlawiy: “Hakika kunasibishwa kwa kundi hili kuna mahusiano makubwa na Muhammad Said An-Nursiy Al-Kurdiy anayefahamika kwa jina la Badiiuz-Zamaan An-Nursiy aliyezaliwa mwaka 1293H na amekufa mwaka 1379H. Naye ndiye aliweka misingi hii sita ambayo wameichagua Jama’at At-Tabliygh wal Khuruuj... Lakini kadari zilipita na kufa harakati hii na kupotea fikra hizi  huko Uturuki kabla ya kuanza kwa uwazi na ujumla, na jambo lililo wazi ni kuwa shekh Muhammad Ilyaas, Mhindi, alipokwenda Hijaaz kuhiji na kufanya ziara na mwenye kuhama, alisikia fikra hii na akaichukua kuipeleka India.” [Nadhwrat ‘Aabirah I’itibaariyah hawla Al-Jama’at At-Tabliygh, uk. 11].

 

 

Uhakika Wa Da’wah Ya Jamaat At-Tabliygh

 

Ni da’wah ya Kisufi na hakuna shaka katika hilo. Dalili ni kuwa mashekh wa wa kundi hili na walezi wake ni Masufi wakubwa (kindakindaki) na wanasisitiza Usufi na kuutangaza. Hata shekh wao, Muhammad Ilyaas alitoa kiapo cha utiifu mwaka 1315 kwa shekh Raashid Ahmad Gangohi na akala tena kiapo kwa shekh Khalil Ahmad Saharanpuri baada ya kufa shekh Gangohi na kufika daraja ya Ukhalifa.

 

 

Amesema Muhammad Aslam: “Shekh Muhammad Zakariya Kandhalvi amehariri shahada ya Ijaazah na Khilaafah ambayo amempa shekh Ilyaas. Mtoto wake, shekh Muhammad Yuusuf alisema katika shahada hiyo, ‘Mimi ninawatunukia hawa bay’ah,’ na akaongeza shekh Muhammad Ilyaas akandika, ‘Mimi natunukia kiapo hicho kwa niaba ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)’.” [Siyrat Muhammad Yuusuf, uk. 196]

 

 

Amesema Ahmad Nuur: “Kabla ya miaka kadhaa ya kuumwa kwa Twaahir Shaah na kupelekwa hospitali, na pale hali yake ilipokuwa mbaya, zilimtembelea roho ya mama yake na roho ya baba yake, akaambiwa kuwa wakati wake wa kuelekea kwenye nyumba nyingine umekurubia na wanamsubiri. Wakati huo Malaika wawili wakafika na kuondoka na Twaahir Shaah kwenda kukutana na Rabb wake (Allaah), wakaenda Malaika hawa na roho ya Twahir Shaah mpaka mbinguni. Huko alikutana na Maulana Yuusuf (Amiri wa Jama’at At-Tabliygh, mtoto wa Maulana Muhammad Ilyaas, muasisi wa kundi hilo) na pia alikutana na Ahmad Aliy; wakashangaa mashekh hawa wawili kwa kuhitajiwa Twahir Shaah na Allaah kuja mbinguni na hali ya kuwa hakubaki ardhini yeyote mwenye kuisimamia kazi hii ya Tabliygh. Hivyo hawa mashekh wakamshitakia shekh Ilyaas jambo hilo na shekh Ilyaas naye akenda kumshtakia Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Shekh Ilyaas akamtaka Twaahir Shaah arudi duniani na wakati huo Twaahir Shaah alikuwa amefariki kule hospitali na kiwiliwil chake kimebebwa kinapelekwa nyumbani kwake. Wakati huo basi alifufuka Twaahir Shaah, akasimama mwenyewe kuelekea nyumbani kwake. Kisa hiki amenisimulia Twaahir  Shaah mwenyewe nami nakisimulia kwenu kama alivyo nieleza. [Qabr kiy zindagi aur mawt ke jundi ‘Manaadhwir Waaqi’aat wa Mushaahadaat’ – Maktabat Khaliyl Yuusuf, Market Urdu Bazaar, Lahore, Pakistan].

 

 

Na amesema Muhammad Zakariyah: “Mimi namuona shekh Thanwi na shekh Madani kama vile jua na mwezi. Yeyote kati ya hao wawili mtakayemfuata mtaongoka, na shikamaneni na dini waliyokuwa nayo mashekh zetu, mfano shekh Gangohi na shekh Nanotvi na kamateni dini hiyo kwa meno yenu ya magego kwani ni jambo gumu kuzaliwa mfano wao. Basi ni juu yenu kufuata mienendo yao.” [Tays Majaalis, Thalaathuuna Majlisa, uk. 132-176].

 

 

Na amesema tena: “Na kwa hali yoyote sisi kama kundi tunaona ulazima wa kufuata Twariyqah hii ya Tabliygh, na kama tunavyoona Usufi wa kisheria ndio njia ya karibu ya kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na yeyote atakayetukhalifu katika mambo mawili haya (Taqliyd na Usufi), huyo yuko mbali na kundi letu hili, na kila jambo katika hayo mawili ni muhimu sana katika madhehebu ya Deobandi. [Fitnat Mawduudiyat, Muhammad Zakariyah, uk. 126; Tays Majaalis, Thalaathuuna Majlisa, uk. 135].

 

 

Na amesema tena: “Bora ya Twariyqah kwa ajili ya kuzidisha furaha za shekh Ar-Ruuhaaniyyah, ni kushikamana na mafunzo yake na kuwa madhubuti na mafunzo hayo na kufanya juhudi katika kuyaeneza mafunzo hayo.” [Tabliyghiy Jama’at Bar’umuumiy iitiraadhaat aur ankaa jawaabaat, uk. 128].

      

           
Na amesema tena: “Inampasa kila muridu kufuata shekh wake katika kila kauli zake na vitendo vyake, na kunazingatiwa kumfuata shekh ni faradhi wala asipingane naye kabisa, na wala asipambane naye katika hali yoyote. [Swaqaalatul Quluub, uk. 172].

 

 

Na anasema: “Kila desturi zote za mashekh wetu zina haki ya kukamatwa (kufuatwa) kisawasawa. Na mimi toka niliposikia kwamba shekh Gangohi alikuwa akisoma katika Swalah ya Taaraawiyh usiku wa thelathini wa Ramadhaan, Suwrah Alam Tara, nami ni mwenye kufanya hivyo, na kama si kuona mwezi muandamo basi ningemuamrisha shekh ‘Abdur-Rahiym atuswalishe Taaraawiyh kwa kusoma Suwrah Alam Tara (Suratul Fiyl). [Tays Majaalis, Thalaathuuna Majlisa, uk. 176].

 

 

Na amesema Sufi Muhammad Iqbaal naye ni katika wafuasi wakubwa wa shekh Muhammad Zakariyah Kandhalvi: “Amesema shekh Gangohi zaidi ya mara moja, ‘Sikizeni vizuri, hakika haki ni ile inayotoka katika kinywa cha Raashid Ahmad (anajikusudia yeye mwenyewe) na naapa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mimi si kitu chochote isipokuwa kuokoka na muongozo ni kwa wale  wafuasi wangu tu.” [Swaqaalatul Quluub, uk. 190].

 

 

Na amesema shekh Gangohi: “Sikiliza, Nikuwa nikitaka idhini kutoka kwa Hadhrat Al-Haaj (ImdaadiLLaah) kabla ya miaka kumi, baada ya hapo nikaanza kutaka idhni kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) moja kwa moja. [Tays Majaalis, Thalaathuuna Majlisa, uk. 311].

 

 

Na amesema Sufi Muhammad Iqbaal: “Amesema shekh Gangohi, ‘Nilipokuwa katika daraja fulani ‘la Shekh’ nilikuwa sifanyi jambo mpaka nipate ufafanuzi kutoka kwa shekh Al-Haaj ImdaadiLLaah, kisha nikafikia fulani ‘ya Rasuli wa Allaah nilikuwa sifanyi jambo lolote katika muda wa miaka mitatu ila kwa idhini ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akanyamaza, akulizwa akasema na baada ya hapo ni daraja ya Ihsaan. [Mahbuubul ‘Aarifiyn, uk. 57].

 

 

 

 


[1] Deobandi wanafuata madhehebu ya Hanafiy ki-Fiqh, na ki-‘Aqiydah wanafuata ‘Aqiydah ya Ashaa’irah na Maaturudiyyah, na kwa upande wa Usufi wanafuata Twariyqah za Chisti, Naqshabandiyyah, Qaadiriyyah na Suhrawardiyyah.

 

 

 

 

 

Share