04-Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Sura Ya 2: Maisha Ya Awali

  

SURA YA 2: MAISHA YA AWALI

Kuzaliwa Kwake Na Utotoni Mwake

Shaykh al-Islaam, Taqiyud-Diyn Abu al-‘Abbaas Ahmad bin Shihaab ad-Diyn Abu al-Mahaasin ‘Abdul-Haliym bin Majdud-Diyn Abi al-Barakaat ‘Abdus-Salaam bin ‘Abdillaah bin Abi al-Qaasim Muhammad bin al-Khidhwr bin Muhammad bin al-Khidhwr bin ‘Aliyy bin ‘Abdillaah bin Taymiyyah, alizaliwa mnamo siku ya Jumatatu ya mwezi 10 ya Rabiy’ al-Awwal mwaka 661 Hijriyyah sawa na tarehe 22/Januari/1263 Miylaadiyyah sehemu za Harraan[1] kwenye familia maarufu ya watu wa Diyn.

Babu yake, aitwaye Abu al-Barakaat Majdud-Diyn Ibn Taymiyyah (amefariki mwaka 653 H/1255 M) alikuwa ni mwalimu maarufu wa madhehebu ya Kihanbali na mwenendo wake wa Muntaqaa al-Akhbaar (yaani uchaguzi wa misemo ya Kitume) ambao unazipa sifa Ahaadiyth ambazo zimeegemezwa na Shari’ah za Kiislamu, hadi hii leo unatambulika kwamba ni kazi muhimu mno. Vivyo hiyo, mafanikio ya kiuanachuoni ya baba wa Ibn Taymiyyah, Shihaabud-Diyn ‘Abdul-Haliym Ibn Taymiyyah (amefariki mwaka 682 H/1284 M) yalienea kwa mapana.

 

Huu ulikuwa ni wakati ambapo magenge ya Wa-Tartar chini ya Hulagu Khaan walikuwa wakisumbua ulimwengu wa Uislamu kwa mateso yao maovu yanayoendelea katika uuaji. Ibn Taymiyyah alikuwa na umri wa miaka saba pale Wa-Tartar walipoanzisha uvamizi wao Harraan. Hapo hapo, wakazi waliiacha Harraan kwa kutafuta makazi sehemu nyengine. Familia ya Ibn Taymiyyah ilielekea Damascus mnamo mwaka 667 H/1268 M; ambayo kipindi hicho ilitawaliwa na Mamluki wa Misri. Ilikuwa ni hapa ambapo baba yake alikhutubia kutoka mimbari ya Msikiti wa Umayyah na alialikwa kusomesha Hadiyth ndani ya Msikiti (huo) na pia kwenye Daarul-Hadiyth ‘As-Sukuriyyah huko Damascus. Mihadhara hii ilihudhuriwa na wanafunzi walio na idadi kubwa na halikadhalika kwa Wanachuoni. Ibn Taymiyyah alifuata nyayo za baba yake ambaye alikuwa ni Mwanachuoni wa masomo ya Kiislamu kwa kujifunza kutoka kwa Wanachuoni wakubwa wa wakati huo, ambao miongoni mwao alikuwa ni mwanamke aliyeitwa kwa jina la Zaynab bint Makkiy akimfundisha (somo la) Hadiyth.

 

Malezi yake

Shaykh al-Islaam, Ibn Taymiyyah alilelewa, kuthaminiwa na kusimamiwa na baba yake. Alipata elimu kutoka kwake na Mashaykh wengine wa enzi zake. Hakujifunga tu mwenyewe na elimu ya wale waliomzunguka, lakini alitilia mkazo kwenye kazi za Wanachuoni waliokuwepo kabla ya wakati wake kwa njia ya kuchunguza na kuhifadhi. Alikuwa na kipaji cha akili na hodari wa kukamata elimu.[2] Umakini wake wa muda kutoka umri wake wa awali,[3] ambao ulimsaidia kumuongoza maisha yake yote yaliyobakia kujazwa na matendo ya Jihaad, ualimu, uamrishaji mema, ukatazaji maovu, uandishi wa vitabu na barua na kuwajibu wapinzani. Upana na nguvu za athari zake na hoja zake (zilimuathiri) Myahudi kuukubali Uislamu mikononi mwake hali ya kuwa akiwa ni kijana mdogo.

 

Alianza kutoa fatwa akiwa na umri wa miaka kumi na tisa[4] na kuanza kusomesha ndani ya Daar al-Hadiyth as-Sukuriyyah akiwa na umri wa miaka takriban 22 ya umri wake.[5] Vyanzo vikuu vya elimu vilizunguka kwenye masuala ya sayansi kama vile: Tafsiyr; Sayansi ya Qur-aan; Sunnah; Vitabu sita; Musnad Imaam Ahmad; Sunan ad-Daarimiy; Mu’jam at-Twabaraaniy; Sayansi ya Hadiyth na wasimuliaji; Fiqh na Uswuwl yake; Uswuwl ad-Diyn na vigawanyo vyake; lugha; maandiko; hesabati; historia na mada nyengine kama vile elimu ya nyota, utabibu na ufundi. Ushahidi wa haya unapatikana kwa kuzisoma kazi zake ambazo baadae aliziandika; mada yoyote aliyoichunguza na kuiandika inamuacha msomaji kufikiria kwamba Ibn Taymiyyah alikuwa ni mweledi ndani ya nyanja hiyo.

 

 

Ibn Taymiyyah: Mtoto Mwenye Kipaji cha Akili

Siku moja, baba yake na familia yake walimwambia ajiunge nao kwenda mapumzikoni lakini ghafla akatokomea asionekane alipokwendea, hivyo ilibidi waende bila yeye. Waliporejea mwishoni mwa siku hiyo, walimlaumu kwa kutokwenda pamoja nao. Akasema, akiashiria kitabu kwenye mkono wake: “Hamjafaidika chochote kutokana na safari yenu, isipokuwa mimi nimehifadhi kitabu chote hichi kipindi mlipoondoka.”

Alitambulikana kwa sura yake, kipaji chake cha kuhifadhi mambo na uhodari wake ambao uliwashangaza watu wa Damascus na kuwafanya kumstaajabia zaidi na zaidi. Ingawa alikuwa ni mdogo kiumri, umaarufu wake ulifikia maeneo ya jirani. Mara moja, mmoja wa Wanachuoni wa Halab alimtembelea Damascus. Wanachuoni na watu maarufu wa mji huo walikwenda kumlaki. Aliwaambia: “Nimesikia katika baadhi ya vitongoji kwamba kuna mtoto ambaye ni mwepesi wa kuhifadhi kila kitu. Nimekuja hapa ili kumuona.”

Wakamuongoza huyo mtu kwenda chuo kimoja kidogo ambacho mtoto huyo akienda kuhifadhi Qur-aan. Mwanachuoni wa ki-Halabi akakaa kwa muda hadi huyo mtoto akapita na bao lake kubwa mkononi. Mwanachuoni huyo akamwita, hivyo akaenda kwake.

Mwanachuoni akalichukua bao kutoka kwake na kumwambia: “Kaa hapa ewe kijana, na nitakuhadithia baadhi ya simulizi za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili uandike.” Akamsimulia baadhi yake, kisha akamwambia azisome.

Kijana akaanza kuzisoma kutoka baoni. Kisha Shaykh akamwambia: “Acha nikusikilize kutoka kwako.” Akaanza kuzirudia simulizi hizo kutoka kichwani mwake namna sawa sawa kama vile anasoma kutoka kwenye bao. Mwanachuoni akamwambia: “Futa hii, ewe kijana.” Akanukuu simulizi zaidi za Mtume na kumwambia azirudie. Kijana akafanya vile vile kama mwanzo; akazisoma kutoka baoni na kutoka kichwani mwake. Mwanachuoni akasimama na kusema: “Iwapo kijana huyu ataishi zaidi, atakuwa na hadhi kubwa [kuwa ni Mwanachuoni mkubwa]. Hatujapatapo kuona mtu kama huyu hapo kabla.” 

 

 

Kipaji cha Kumbukumbu cha Hali ya Juu

Imaam Al-Bazzaar[6] alisema: “Rafiki mmoja aliyekuwa muaminifu akimjua aliniambia kwamba pale Shaykh (Rahimahu Allaah) akiwa yungali katikati ya umri wake wa ujana na akitembea kwenda maktaba, huwa anasimamishwa njiani mwake na Yahudi mmoja aliyekuwa akiishi pembezoni mwa barabara ikielekea maktaba. Yahudi huyo huwa anamuuliza masuala ya mambo tofauti, na huwa na uhakika wa masuala yake (kujibiwa vyema) kutokana na uhodari na ushupavu wa akili ya Ibn Taymiyyah. Ibn Taymiyyah humjibu harakaharaka hadi kwamba Yahudi huwa na shauku naye. Mwishowe, pindipo Ibn Taymiyyah akimpita yeye, basi humpatia vipande vya taarifa ambazo zinahakikisha uongo ambao upo dhidi yake (huyo Yahudi). Hili liliendelea hadi akaukubali Uislamu na akawa ni Muislamu mwenye kuufuata Uislamu kwa ukamilifu, na hili ni kutokana na baraka aliyopewa Shaykh tangu katika umri wa ujana.

 

Na tokea kuingia kwenye ujana, aliutumikia muda wake wote akishughulika na jitihada na utendaji, na akiihifadhi Qur-aan yote akiwa mdogo, na kuendelea kwa kusoma na kuhifadhi Hadiyth, Fiqh, na lugha ya Kiarabu hadi akawa mweledi wa masomo yote hayo. Hili lilikuwa linaenda sambamba na umakini wake wa hali ya juu katika kuhudhuria darsa za duara za elimu na kusikiliza simulizi za Hadiyth na Athar. Amesikia vitabu vingi kutoka kwa Wanachuoni tofauti wenye vipaji vya juu.[7] Ama kwa vitabu vikuu vya Uislamu kama vile ‘Musnad’ cha Ahmad, Swahiyh za al-Bukhaariy na Muslim, ‘Jaami’ cha at-Tirmidhiy, ‘Sunan' cha Abu Daawuwd as-Sijistaaniy, an-Nasaaiy, Ibn Maajah, na ad-Daaraqutniy (Rahimahumu Allaah); kila kimoja katika hivi vimesimuliwa kwake kwa ukamilifu wake mara kadhaa. Kitabu cha mwanzo alichokihifadhi kwa ghayb katika Hadiyth kilikuwa ni cha al-Humaydi ‘al-Jam’ Bayn asw-Swahiyhayn.’

 

Ni nadra kuwepo kitabu katika nyanja za sayansi ya Uislamu [akawa hajakisoma] isipokuwa kwamba yeye ameshakutana nacho, na Allaah Akambariki kwa uwezo wa kukihifadhi upesi, na kukisahau ni nadra kwake. Mara chache [kuona kwamba] atakutana au kusikia kitu isipokuwa kwamba kimebakia kwenye akili yake, aidha kwa maneno au maana. Ilikuwa kana kwamba vile taaluma kwake imeganda ndani ya nyama yake, damu yake na mwili wake wote. Hakuchukua tu kibubusa vipande vya taaluma kutoka hapa na pale. Isipokuwa, alikuwa na uelewa na maarifa kamili, na alikuwa ni miongoni mwa watu wa juu wenye hadhi ya juu na ubora. Allaah Alimpatia kazi ambayo kikawaida huwa ndio sababu ya kumuharibu mtu mwengine yeyote, [lakini Allaah Akamjaalia] kumuongoza katika utukufu na furaha katika nyanja zote za maisha yake, na kutia athari ya uongozi wake kwa alama zilizo wazi kwa watu wote, hadi kufikia kwamba kila mtu mwenye uelewa mdogo tu kukubali kwamba yeye ni wale ambao kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakusudia pale aliposema: “Kwa hakika, Allaah humleta katika kila mwanzo wa karne [mtu ambaye] atahuisha masuala ya Diyn kwa Ummah huu.” [8] Kwa vile Allaah Ameihuisha kupitia kwake Shari'ah za Diyn hii ambazo hapo zama za kale zilisahaulika kabisa, na kumfanya kuwa ni ithibati juu ya watu wote wa enzi hizi, na shukrani zote ni za Allaah, Bwana wa ulimwengu wote. [9]

 

 

 

 

 

 

 

[1] Imepakana na mpaka wa baina ya Syria ya leo, Uturuki na Iraaq (ambayo sasa ni sehemu ya Uturuki ya kusini-mashariki).

[2] Al-'Uquwd ad-Duriyyah, uk. 4, na al-Kawaakib ad-Durriyyah Fiy Manaaqib al-Mujtahid Ibn Taymiyyah cha al-Karmiy al-Hanbaliy, uk.80.

[3] Ar-Radd al-Waafir 'alaa man za'ama bi anna man sammaa Ibn Taymiyyah Shaykhul- Islaam Kaafir cha Ibn Naasir ad-Diyn ad-Dimashqiy, uk. 218, na A'yaan al-'Asr 'an Shaykhul-lslaam Ibn Taymiyyah, Siyratuh wa Akhbaaruh 'inda al-Mu'arrikhiyn cha Muhammad bin Swaalih, uk. 49.

[4] Sharafud-Diyn al-Maqdasiy (amefariki mwaka 694 H) amempa ruhusa ya kutoa hukumu za kishari'ah. Baadaye akatumia nafasi hii kujisifia, akisema “Nimempatia mimi ruhusa ya kutoa hukumu za kishari'a.” Al-Bidaayah wan-Nihaayah cha Ibn Kathiyr, 13/341, na al-'Uquud ad-Durriyyah, uk. 4.

[5] Al-'Uquud ad-Durriyyah, uk. 5; al-Bidaayah wan-Nihaayah, 13/303; ar-Radd al-Waafir, uk. 146 na adh-Dhayl 'alaa Twabaqaat al-Hanaabilah cha Ibn Rajab, 2/388.

[6] Abu Hafsw ‘Umar bin ‘Aliy al-Bazzaar ambaye alikuwa ni rafiki yake binafsi na swahiba wake, ameandika maisha yake marefu na ya mwanzo kuhusu Ibn Taymiyyah katika kitabu kiitwacho ‘al-A’laam al-’Aliyyah fi Manaaqib Ibn Taymiyyah,’

[7] Amesoma kwa zaidi ya Wanachuoni 200. Angalia al-Kawaakib ad-Durriyyah’ (uk. 52)

[8] ‘Swahiyh al-Jaami’(1874) na as-Silsilah asw-Swahiyhah’ (599)

[9] Manaaqib Ibn Taymiyyah, ukurasa wa 7.

 

Share