05-Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Sura Ya 3: Maisha Yake Ya Ucha Mungu

 

SURA YA 3: MAISHA YAKE YA UCHAJI ALLAAH

 

‘Ibaadah Zake

 

Ibn Taymiyyah alikuwa na ukaribu mno kwa Mola wake ambao ulidhihiri ndani ya ‘ibaadah zake na utegemezi wake wa hali ya juu Kwake, hivi ndivyo tunavyomsadiki kuwa na hatuziweki sifa za yeyote mbele ya Allaah. Wale ambao wameandika wasifu wake wamejadili umaarufu wake katika ‘ibaadah, utawa, haya, mwenye kujitolea, unyenyekevu na ukarimu.[1]

 

Ibn al-Qayyim anasema kuhusu dhikri za Ibn Taymiyyah kwa Mola wake: “Nilimsikia Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah, Mola Amrehemu roho yake, akisema ‘Dhikri kwa moyo ni kama vile maji kwa samaki. Itakuwaje hali ya samaki iwapo itatengana kutokana na maji? …Mara moja nilihudhuria Swalah ya Alfajr pamoja na Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah, kisha akaketi na kumkumbuka Allaah hadi kukaribia mchana. Kisha akageuka na kuniambia, ‘Hichi ndicho chakula changu cha asubuhi ya mapema, iwapo sitopata kifungua kinywa hichi, nguvu zangu zitaanguka.’”[2]

 

Kinachodhihiri zaidi katika ‘ibaadah zake ilikuwa ni utegemezi wake halisi juu ya Mola wake na imani zake ndani ya amri za Allaah. Mara nyingi pale anapokumbana na aina ngumu za mitihani, alikuwa na uegemezi mkuu mbele ya Mola wake. Pale habari za kufukuzwa kwake kwenda Alexandria zilipomfikia na alipoambiwa: “Wanapanga kukuua, kukufukuza au kukufunga.” Alijibu: “Iwapo wataniua itakuwa ni shahaadah kwangu. Iwapo watanifukuza, itakuwa ni hijrah kwangu; iwapo watanifukuza kwenda Cyprus, nitawalingania watu wake kwa Allaah ili wanisikilize. Iwapo watanifunga, hiyo itakuwa ni sehemu yangu ya kufanya ‘ibaadah zangu.”[3]

 

Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah) pia anasema: “Alikuwa akisema mara kwa mara kwa unyenyekevu pale anapofungwa, ‘Ee Allaah, nisaidie ili nikukumbuke wewe, niwe mwenye kukushukuru wewe na kukuabudu wewe kisawasawa.’ Na alisema mara moja kuniambia mimi, ‘Yule ambaye amefungwa (kikweli kweli) ni yule ambaye moyo wake umefungwa kwa ajili ya Allaah na aliyependezeshwa mno ni yule ambaye matamanio yake yamemtia utumwani.’ "[4]

 

Al-Imaam al-Bazzaar (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wakati wa usiku, alikuwa akijitenga kutokana na kila mtu, akijifunga pamoja na Mola wake, akiwa na uendelevu thabiti wa kuisoma Qur-aan tukufu, na kuzirudia ‘ibaadah tofauti za kila siku na za usiku.

 

Pale usiku unapokwisha, atakusanyika na watu kwenye Swalah ya Alfajr, akiswali Swalah ya Sunnah kabla ya kukutana nao. Pale anapoanza Swalah, moyo wako utataka kuruka kutoka sehemu yake kwa namna tu anavyoileta Takbiyraatul-Ihraam. Pale anaposoma, atakirefusha kisomo chake, kama ilivyopokewa kwa usahihi namna ya usomaji wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Rukuu yake na utulivu wake, na halikadhalika namna yake ya kuja juu, ni namna kamilifu za namna ilivyopokelewa kwa taratibu za Swalah ya fardhi. Na hujiachia nafasi vizuri katika kikao chake cha mwanzo cha tashahhud, na huitamka tasliym ya mwanzo kwa sauti ya juu, hadi kufikia kwamba kila mtu aliyehudhuria kuisikia...

...Nikaja kutambua kwamba ni tabia yake kwamba hakuna yeyote atakayezungumza naye baada ya Swalah ya Alfajr isipokuwa pale kunapokuwepo haja maalumu. Atabakia katika mtindo wa dhikri za Allaah, akijisikiza mwenyewe. Ataendelea kubakia hivyo hivyo hadi jua linapochomoza, na ambapo muda wa kuharamishwa kuswali umekwisha kuondoka.

 

Wakati wa kukaa kwangu pamoja naye Damascus, huwa natumia baadhi ya siku yangu na muda mwingi wa usiku wangu pamoja naye. Ataniita kuwa pamoja naye, nikikaa pembezoni mwake. Nikisikia yale anayosoma na kuyarudia, na huona akiirudia ‘al-Faatihah’ mara kwa mara nyingine tena, na hutumia muda wake wote baina ya Fajr na jua kuchomoza akifanya hivi. Hivyo, hukaa nikijifikiria, nikiwaza: ni kwanini akisoma Suwrah makhsusi ya Qur-aan akiziacha nyingine? Ghafla, ikaja wazi kwangu – na Allaah ndiye Ajuaye zaidi – kwamba lengo lake katika kufanya hivyo ilikuwa ni kuunganisha pamoja kwa yale anayosoma baina ya yale yaliyopokelewa ndani ya Ahaadiyth na yale ambayo yaliyojadiliwa na Wanachuoni, kwa namna ambayo adhkaar iliyopokelewa ichukue hatamu dhidi ya Qur-aan, ama kinyume chake. Hivyo, aliona kwamba kuirudia ‘al-Faatihah’, huweza kuunganisha baina ya maoni yote, na kuvuna faida za matendo yote, na hili ni kutokana na hoja zake muhimu na uoni wake wa ndani.

 

Baada ya hili, huswali Dhwuhaa, na iwapo anataka kusikiliza Hadiyth kwenye sehemu nyingine, atakimbilia sehemu ile pamoja na yeyote aliyekuwa naye kipindi kile.

 

Ilikuwa ni nadra kwamba kwa mtu yeyote mwenye akili zake timamu anapomuona yeye kutokwenda na kuibusu mikono yake. Hata wafanyabiashara waliokuwa na shughuli nyingi walikuwa na kawaida ya kuacha yale wanayofanya ili kwenda kumsalimia.[5]

 

Iwapo ataona jambo ovu lolote mtaani, atafanya bidii ya kuliondoa, na iwapo atasikia kuna maziko yanafanyika sehemu fulani, atakimbilia kuswalia au kuomba msamaha kwa kuyakosa. Baadhi ya nyakati, huenda baada ya kumaliza kusikiliza Hadiyth kwenye kaburi la aliyefariki na kuliswalia.

 

Mara moja, yeye na swahiba zake walitoka kwenda kuharibu baadhi ya vilabu vya pombe. Wakavunja vyombo vyao, kumwaga ulevi wao, na kuvunja idadi kadhaa ya vinjwaji hivyo. Vilevile, kuna wakati alivunja nguzo kwenye Msikiti hapo Damascus ambayo watu walikuwa wakiiomba baraka kutokana nayo.[6]

 

Baadae, hurejea Msikitini mwake, ambapo hubaki aidha akitoa fataawa kwa watu au akitimiza mahitaji yao hadi inapofika wakati wa kuswali Adhuhr kwa Jamaa’ah. Hutumia baki ya siku yake kwa namna kama hiyo.

 

Darasa zale zilikuwa wazi kwa jamii: kwa wazee, vijana, matajiri, masikini, walio huru, wafungwa, wanaume na wanawake. Alikuwa na mvuto kwa kila mtu anayempita, na kila mtu alikuwa akijisikia kwamba yeye Ibn Taymiyyah anamtumikia zaidi kuliko anavyowatumikia watu wengine waliohudhuria.

 

Kisha huswali Swalah ya Maghrib na kufuatiliza kwa Swalah za Sunnah kama ambavyo Allaah Anavyomuwezesha. Baadaye, mimi au mtu mwengine yeyote humsomea maandiko yake, na hutufaidisha sisi kwa nukta na maelezo mbali mbali. Hufanya hivi hadi tunaposwali ‘Ishaa, baada ya hapo huendelea kama tulivyokuwa kabla, tukichunguza kwenye nyanja tofauti za elimu. Huwa tunafanya hivi hadi muda mwingi wa usiku unapopita. Wakati wote huu – usiku na mchana – Ibn Taymiyyah mara kwa mara humdhukuru Allaah, akitaja Upweke Wake, na kuomba msamaha Wake.

 

Na kila mara huinua macho yake mbinguni na hatoacha kufanya hivi, kama vile kuna kitu amekiona huko juu kinachoyafanya macho yake yagande huko. Hufanya hivi kwa muda wote ninapokaa pamoja naye.

 

Hivyo, Subhaana-Allaah! Ni kwa namna gani siku hizi zilikuwa ni fupi! Yareti zingelikuwa ni refu! Naapa kwa Allaah, hadi hii leo, hakuna wakati uliotokea ukawa ni wenye kupendezesha zaidi kwangu kuliko muda ninaokaa pamoja naye, na hakuna kipindi nilichoonekana kwenye nafasi bora kama kipindi hicho, na hili halikuwa kwa sababu nyingine isipokuwa ni kheri alizotunikiwa Shaykh (Rahimahu Allaah).

 

Kila wiki, alikuwa akitembelea wagonjwa, haswa wale waliopo hospitalini, na nimearifiwa na zaidi ya mtu mmoja ambaye ukweli wake siutilii shaka kwamba maisha yake yote ya Shaykh yalitumika kwenye mtindo ambao nimeushuhudia na niliouleza hapo juu. Hivyo, ni ‘ibaadah gani, na jihaad gani, iliyo bora kuliko hii?[7]

 

Hivyo, angalia ni kwa namna gani Allaah Amemuongoza Imaam huyu kuepukana na yote isipokuwa yale anayohitajia ndani ya maisha yake. Alizidiwa na mapenzi yake kwa Allaah, na matokeo yake alitunikiwa sifa zote na ubora kinyume na Wanachuoni wa kidunia ambao wanauchagua, kuutafuta, na kuukimbilia. Wanapochagua mazuri yake, wanajifungia mbali kutokana na njia yake ya uongofu, na matokeo yake wanaangukia kinyume chake. Wanaenda kwenye mtindo wa kuchanganyikiwa, kama ambavyo mtu anayetembea kwenye giza, asijue kipi wanachokula wala wanachovaa. Wala hawaelewi lipi wanategemea kufanikiwa kutokana na malengo yao maovu na ya udhalilifu. Wanashindana kwayo, wakifanyia uadui kwa sababu zake, wakiijaza miili yao pamoja nazo, na wakisukuma kila kitu nje ya mioyo yao. Wanategemea zaidi muonekano wao wa nje hali yakuwa mioyo yao imepiga weusi na iliyojaa ufisadi. Wala hawatosheki hadi pale wanapokuwa maadui kwa wale wanaokana na wanaochukizwa na aina hiyo ya maisha.

 

Pale walipomuona Imaam huyu kama ni Mwanachuoni wa Aakhirah – akiachana na tabia zao za kukusanya mazuri ya dunia hii, akijiepusha na yenye kutia shaka, na kukana yale mambo ambayo hayana umuhimu kuruhusiwa – wakaja kuona kwamba mwenendo wake unawaweka wazi na kuwatia aibu. Hivyo, wakazidi choyo kwamba yeye ameonesha sifa za kiroho hali ya kuwa wao walikuwa hawana kitu zaidi ya yale maovu, na wakakusanyika kumvuruga kwa namna itakayokuwa, wakisahau kwamba wao walikuwa ni mbwa mwitu wakati yeye ni simba. Hivyo, Allaah Amemlinda yeye kutokana nao ndani ya matokeo zaidi ya moja, kama ambavyo Anafanya kwa waja Wake wapenzi. Amemlinda yeye kwa kipindi chote cha maisha yake, na kusambaza elimu yake baada ya kifo chake hadi hatamu za Ardhi.

 

 

Zuhd Yake

 

 

Imaam al-Bazzaar amesema kuhusiana na zuhd ya Shaykh al-Islaam:

 

“Ama kwa zuhd yake kutokana na dunia na marembo yake, Allaah Amefanya hili kuwa ni somo endelevu ndani ya maisha yake tokea wakati wa ujana wake. Rafiki mmoja muaminifu alinisimulia kwamba mwalimu wake aliyemsomesha Qur-aan Ibn Taymiyyah akisema:

 

 “Baba yake ameniambia wakati bado akiwa ni mtoto mdogo: “Nitapendelea kwako wewe kumuhakikishia kwamba iwapo hatoacha kusoma na kuifanyia kazi Qur-aan, nitampatia dirham arobaini kila mwezi.” Hivyo, akanipatia zile dirham arobaini, na kuniambia: “Mpatie yeye. Bado ni kijana, na huwnda akafurahikia na kuongeza hamu yake katika kuhifadhi na kuisoma Qur-aan, na mwambie kwamba atakuwa na kiwango kama hicho cha fedha kila mwezi.” [Hata] Hivyo, Ibn Taymiyyah akakataa kuzikubali, akisema:

 

 “Ewe mwalimu wangu, nimemuahidi Allaah kwamba sitokubali aina yoyote ya malipo kwa ajili ya Qur-aan,” na wala hakuzikubali daima. Nikajisemeza kwamba hili haliwezi kutokea isipokuwa kwa kijana ambaye ametengwa na Allaah.

 

Mwalimu huyu amezungumza ukweli, kwani hifadhi na ulinzi wa Allaah ndio uliomkuza yeye kwenye mazuri yote ndani ya maisha yake kutoka mwanzo hadi mwisho. Kila mtu aliyekutana naye – haswa wale waliosuhubiana naye kwa vipindi virefu vya wakati – wanakubali kwamba hawakupata kuona mtu sawa na yeye kwenye zuhd yake ya dunia, hadi kufikia kiwango kwamba alikuwa ni maarufu kwa hili, na hili lilikuja kuwa wazi ndani ya kila moyo wa mtu asikiaye sifa zake, wa mbali na wa karibu. Ukweli kwamba, iwapo utakuwa ni mwenye kumuuliza mtu ambaye akiishi hapa kila siku ambaye hakuwa karibu mno na Shaykh: ‘Ni nani ambaye ameonesha zuhd ya juu ndani ya enzi zetu, na alikuwa ni mwenye ukakamavu wa kukana mambo yasiyo na muhimu ya dunia, na mwenye hamu kubwa ya kuitafuta Aakhirah?’ basi atasema: ‘Sijasikiapo mtu yeyote kama Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)!’[8]

 

Hakuwa maarufu kwa hili isipokuwa kwa sababu ya kujitolea kwake katika kufanya hivyo. Ni Wanachuoni wangapi tunawashuhudia ambao wameridhika na kiwango kidogo cha dunia walichonacho kuliko alivyokuwa yeye? Hakupatapo kusikilikana akiulizia kuhusu mke mzuri, ama mtumwa wa kike aliye mchangamfu, ama nyumba iliyojengwa vyema, au watumwa watiifu, au bustani za kifakhari, au mnyama mwenye nguvu kwa ajili ya kutembelea, au nguo laini na za kisasa, au nafasi ya uongozi, wala hakupatapo kuzuia dinaar au dirham, wala hakupatapo kuonekana kukimbilia kupata kitu chenye kuruhusika na kisicho na umuhimu. Hili lilikuwa, ingawa kwamba, ukweli upo kuwa wafalme, watawala na wafanya biashara maarufu walikuwa chini ya amri yake, wenye kuyakubali maneno yake, wakiwa tayari kuja karibu naye kadiri wanavyoweza, wakimsifu wazi wazi, na kila mmoja akiwa tayari kushughulikia mahitaji yake ya kifedha.

 

Hivyo, je alikuwa ni sawa na wale ambao wanajihimilishia wenyewe elimu hali ya kuwa hawakuwa ni wenye kutokana na watu wake – wale ambao wanababaishwa na Shaytwaan kwenye kumtumikia yeye katika neno na kitendo? Je huoni kwamba wanaziangalia sifa zao na zake, tabia zao na zake, uchoyo wao katika kushindana dunia na kuachana kabisa kwake na mapambo yake, makimbilio yao katika kukusanya [dunia] kwa kadiri wawezavyo na kimbilio lake yeye kuiepuka, utumilikivu wao kwa watawala na kuendelea kubakia milangoni mwao kinyume na kujitumilikisha watawala kwake yeye, ukosefu wake wa vitisho kutoka kwenye mamlaka na nguvu zao, uwepesi wake wa kuzungumza kwake ukweli mbele yao, na nguvu ambayo atawahutubia wao? Kwa hakika, naapa kwa Allaah! Hata hivyo, wamejinyoa wenyewe – kwa dini yao, sio nywele zao, na mapenzi yao ya dunia yamechukua ndoto zao, na wameibiwa kwa nguvu – kwa elimu zao, sio kwa miliki zao, hadi kufikia kwamba watakimbilia mbali kutokana na wale ambao wamekuja kukiuliza kutokana nao, na hufanya urafiki kwa wale tu ambao watawasaidia kupata zaidi.

 

 

 

 

[1] Al-A'laam al-'Aliyyah, uk. 36-41, 42, 48 & 63 na al-Kawaakib ad-Durriyyah, uk. 83-88.

[2] Al-Waabil as-Sayyib cha Ibn al-Qayyim, uk. 60.

[3] Naahiyah min Hayaat Shaykhul-Islaam, uk. 30.

[4] Al-Waabil as-Sayyib, uk. 61.

[5] Hii ni kwa namna ya kwamba walikuwa wakikimbilia kupata barka za kuwa naye karibu na elimu yake, sio kwa sababu alikuwa ni mrithi wa chanzo cha barka.

[6] Al-Bidaayah wan-Nihaayah (13/34 na 14/122-123).

[7] The Lofty Virtues of Ibn Taymiyyah, ukurasas 15.

[8] The Lofty Virtues of Ibn Taymiyyah, ukurasa, 18.

Share