Kuna Tofauti Ya Muda Wa Kunyonyesha Baina Ya Mtoto Wa Kiume Na wa Kike?

  

Swali:

Kuna ubaya gani mtoto wa kiume kunyonyeshwa ziwa la mama zaidi ya miaka miwili na  kwa nini sio mtoto wa kike? au si kweli?

 


 

Jibu:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Hakuna tofuati baina ya mtoto wa kike na kiume katika kunyonyeshwa. Hukumu yote ni moja ya kunyonyeshwa miaka miwili. Hii kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa mlichoahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni Allaah, na jueni kwamba Allaah Anayaona yote mnayoyatenda)) [Al-Baqarah: 233]

Ama kuzidisha kunyonyesha zaidi ya miaka miwili si jambo la kupasa kufanywa ingawa hakuna makatazo kutokana na dalili inayopatikana katika jibu lifuatalo:

Kunyonyesha Kupindukia Mipaka ya Miaka Miwili Inafaa?

Lakini itambulike kwamba Allaah (Subhaanah wa Ta’ala) Anapoweka hukmu Zake basi huwa zina Hikma ndani yake. Na hivyo kipindi hicho cha miwaka miwili kinamtosheleza mtoto kupata maziwa ya mama akanufaika kwa kila upande. Na itambulike kuwa uhusiano wa kunyonyesha unapatikana ndani ya hiyo miaka miwili tu. Ama nje yake hakuna tena uhusiano. Na faida zake za ki afya na siha kwa mtoto na mama pia zinapatikana ndani ya  hiyo miaka miwili tu  kama zilivyothibiti katika sayansi. Na yote hayo hakuna tofauti kati ya mtoto mwanamume na mwanamke.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share