06-Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Sura Ya 4: Mwenye Elimu Ya Ki-Ensaiklopidia

 

 

SURA YA 4: MWENYE ELIMU YA KI-ENSAIKOPIDIA

Elimu Yake Na Kumbukumbu Zake Za Ajabu

Shaykh al-Islaam alikuwa na elimu kubwa kabisa, hii inajumuisha elimu yake katika sayansi ya Qur-aan Tukufu, uwezo wake wa kuelewa manufaa yake yote katika nyanja zote, na nukta zake muhimu, elimu yake ya kuyaelezea matamko ya Wanachuoni, namna yake ya kuyatumia matamko haya kama ni ushahidi, na hali kadhalika uwezo aliopatiwa na Allaah umemuwezesha kuelezea maajabu yake, uzuri wa Shari’ah Zake, hazina zake zilizo adimu na za kushangaza, miujiza yake ya kilugha, na rehema zake zilizo wazi.

 

Iwapo mtu atakuwa ni mwenye kuzisoma baadhi ya Aayah za Qur-aan Tukufu ndani ya mojawapo ya darsa zake, ataendelea kuzielezea, na darsa yake itamalizia kwa hili. Darsa yake itamalizia kwa kipande kizuri cha siku, na wala hakuwa na mtu maalumu aliyetengwa kwa ajili ya kumsomea Aayah zinazotegemewa kwamba atakuja kujitayarisha [kuzisomesha] nazo. Isipokuwa, mtu yeyote ambaye alikuwa anahudhuria darsa zake atasoma kile kilicho chepesi kwake, na Ibn Taymiyyah baadaye atakuja kukielezea kile kilichosomwa. Kawaida yake huwa hasimami isipokuwa kwa wale waliohudhuria wanapoelewa kwamba yareti isingekuwa kwa uhafifu wa muda, angelipiga mbizi kuelezea katika kila pembe zaidi na zaidi. Hata hivyo, husimama kwa ajili ya kuruhusu wasikilizaji kupumzika. Kwa mfano, ametoa tafsiyr ya “Sema: ’Yeye ni Allaah, Mmoja.”[1] Ambayo ufafanuzi alioutoa umechukua kitabu kizima kikubwa. Pia, tafsiyr yake ya Ar-Rahmaan Aliye juu ya ‘Arshi Yake.”[2] iliyojaza taqriban vitabu 35, na imeelezwa kwamba alianza kukusanya tafsiyr ambayo ingelichukua vitabu hamsini kama angeliikamilisha.

 

Ama kwa elimu yake na uoni wake kuhusiana na Sunnah ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), matamko yake, matendo, matukio ya maisha, vita, majeshi, miujiza ambayo Allaah Amemtunukia, elimu yake ya kipi kilicho sahihi kilichopokelewa kutoka kwake dhidi ya kile ambacho sio sahihi, hali kadhalika na matamko, matendo, matokeo, na hukumu za kishari’ah za Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum), bidii yao kwa ajili ya Diyn hii, na sifa zao walizotunukiwa kinyume na watu wengine ndani ya Ummah huu – ndani ya yote haya, alikuwa ni mwenye makini zaidi na alikuwa na uzoefu wa hali ya juu, na alikuwa ni mwenye kutumia muda mchache katika kurudia taarifa yoyote anayohitajia katika hili. Katu hatoitaja Hadiyth au fatwa ambayo ataitumia kama ni ushahidi wa kitu isipokuwa kwamba ataifanyia marejeo kwa chanzo chake sahihi ndani ya maandiko ya Kiislamu, au kuonesha iwapo ni Swahiyh au Hasan, n.k., au kutaja jina la Swahaba aliyeisimulia, na ni kwa nadra sana ataulizwa kuhusiana na simulizi isipokuwa tu ataithibitishia usahihi wake.

 

Imaam al-Bazzaar amesema:

“Na yaliyo maajabu zaidi kuhusiana na hili ni kwamba mnamo siku zake za mwanzo za kushitakiwa mjini Misri, alikamatwa na kufungwa jela, hadi kufikia kwamba alikuwa hawezi kuviingia vitabu vyake. Ndani ya kipindi hichi, aliandika vitabu vingi – vidogo na vikubwa – na akaeleza ndani ya vitabu hivyo ni ipi Ahaadiyth, simulizi, matamko ya Maswahaba, majina ya Wanachuoni wa Hadiyth, waandishi na kazi zao – na akazielezea kila moja ya hizi kwa kurejea vyanzo vyake sahihi, haswa kwa majina.

Pia ametaja majina ya vitabu ndani ya kila simulizi gani imepatikana, hali kadhalika na wapi ndani ya vitabu utavipata. Yote haya yalikuwa safi kabisa moja kwa moja kutoka kwenye kumbukumbu zake, kwani katika wakati huo hakuwa na kitabu hata kimoja pamoja naye kwa ajili ya kutumia kama ni rejeo. Vitabu hivi baadaye vilichapishwa na kuangaliwa tena, na – Shukrani zote ni za Allaah – hakuna hata kosa moja lililoonekana ndani ya kitabu chochote katika hivyo, wala hakukuwa na haja ya kubadili chochote ndani ya vitabu hivyo. Na miongoni mwa vitabu hivi ni ‘as-Swaarim al-Masluul ‘ala Shaatim ar-Rasuul,’[3] na hili ni kutokana na sifa ambazo Allaah – Mtukufu – Amemtunukia mahsusi kwa ajili yake.[4]

 

Na Allaah Amembariki kwa uwezo wa kuelewa tofauti ya mawazo miongoni mwa Wanachuoni, matamko yao, ijtihaad zao ndani ya masuala tofauti, na kipi kimewekewa kumbukumbu (kimerikodiwa) kutokana na maoni yaliyo na nguvu, hafifu, yaliyokubaliwa na yaliyokataliwa kwa kila Mwanachuoni wa kila enzi. Alikuwa na uoni wa ndani kuhusiana na mawazo yao yepi yalikuwa ni sahihi sana karibu na ukweli, na alikuwa pia na uwezo wa kueleza kwa kila Mwanachuoni ni eneo gani alikuja nalo kwa kila wazo. Hali hii ilifikia hadi kwamba iwapo ataulizwa kuhusiana na lolote katika hili, ilikuwa ni kana kwamba kila tamko la Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba wake, na Wanachuoni – kutoka wa mwanzo hadi wa mwisho wao – kulikuwa na sura iliyoganda ndani ya ubongo wake, pamoja naye akichagua anachotaka na kuacha anachotaka. Hili ni jambo ambalo kwa kila aliyekuwa anamuona au akipita kwenye elimu yake na wasiochukuliwa na ujinga au utashi wanakubaliana nalo.

 

Ama kwa vitabu vyake na maandiko yake, ni zaidi ya ninazoweza kutaja au kufikiria mada zake. Ukweli ni kwamba, nina wasiwasi kwamba mtu yeyote anaweza kuzitaja zote, kwani zipo katika nambari, vyenye ukubwa tofauti, na vimetandawaa duniani kote. Ukweli kwamba, hakuna nchi niliyotembelea isipokuwa nimeona moja ya vitabu vyake nchini humo.

 

Baadhi yake vilifikia vitabu kumi na mbili kwa ukubwa, kama vile ‘Talkhiys at-Talbiys ‘ala Asas at-Taqdiys,’ n.k. Baadhi yake vilikuwa na ukubwa wa vitabu saba, kama vile ‘al-Jam’ Bayn al-‘Aql wan-Naql.’[5]  Baadhi yake vina urefu wa vitabu vitano, kama vile ‘Minhaaj al-Istiqaamah wal-I’tidaal.’ Baadhi yake ni vitabu vitatu, kama vile ‘ar-Radd ‘ala an-Naswaara.’ Baadhi yake ni vitabu viwili, kama vile ‘Nikaah al -Muhallal’ na ‘Ibtwaal al-Hayl’ and ‘Sharh al-‘Aqiydah al-Asbahaaniyyah.’ Baadhi yake ni kitabu kimoja tu au chini ya hapo, na hivi ni vingi mno kuweza kuviorodhesha.”[6]

 

 

Al-’Aqiydah Al-Waasitwiyyah

Tokeo jengine ambalo linaonesha uwezo wake mkubwa na mpana wa elimu aliyokuwa nayo, yeye mwenyewe, Ibn Taymiyyah amesema:

 “Jaji mmoja wa Kishafi’i kutoka Waasit (nchini Iraaq) kwa jina la Radhiyud-Diyn al-Waasitwiy, alinitembelea akiwa njiani kuelekea Hajj. Shaykh huyu alikuwa ni mtu mzuri na mwenye imani. Alinielezea hali za watu nchini huko (yaani Iraaq), chini ya Tartar (Wamongoli) waliokuwa na utawala wa kijinga, usio na haki, na upotefu wa imani na elimu.

Aliniomba nimwandikie ‘Aqiydah (Elimu ya Imani) kama ni rejeo kwake yeye na familia yake. Lakini nikakataa na kusema:  masuala mengi kuhusiana na ‘Aqiydah yameandikwa. Rejea kwa Wanachuoni wa Sunnah. Hata hivyo, alisisitiza katika ombi lake, akisema: Sitaki ‘Aqiydah yoyote isipokuwa ile utakayoandika. Hivyo nikaandika hii moja kwa ajili yake nikiwa nimeketi mchana mmoja.[7]

Kwa mchana mmoja tu aliweza kuandika kitabu kizima cha ‘Aqiydah kutoka kichwani mwake kwa dalili tele ndani yake. Haya ni maajabu ya Mwanachuoni huyu adhimu.

 

Mchango Wake Kwenye Fiqh Na Uswuul Yake

Ibn Taymiyyah tokea enzi za utotoni mwake, alikuwa ni mwanafunzi chipukizi na, kama wanaomsifia wakisema, hakuchukua hamu yoyote kwenye michezo na mazoezi [isiyokuwa na maana]. Baadaye, pia, alipokuwa mkubwa, hakurudi nyuma, sio dhihaka wala tamasha iliyochukua akili zake. Hata hivyo, kazi zake zinashuhudia ukweli kwamba alikuwa na elimu kisawasawa kwa aina tofauti za jamii yake ndani ya kipindi chake, tabia zao na mila, ustaarabu wao na hulka na hata starehe zao na ubunifu. Inaonesha kwamba sio tu kwamba alitumia muda wake kama ni Mwanachuoni aliyezikwa na vitabu, lakini pia alizisoma kwa mapana alama za matatizo na jamii ya kisasa [ya wakati huo].

Ibn Taymiyyah alikusanya [kwa shida] elimu ya kisekula na sayansi ya Dini ndani ya kipindi chake. Aliweka mkazo mahsusi kwenye lugha ya Kiarabu na akapata uweledi wa sarufi na maneno (lexicology). Sio tu alikielewa vyema kitabu cha Al-Kitaab cha Sibawayh, mamluki mkuu wa sarufi na elimu ya lugha (syntax), lakini aliweza kubainisha makosa yaliyomo ndani ya kitabu hicho pia; aliweza kumkosoa bingwa wa lugha ya Kiarabu maarufu.[8] Uwezo wake kwenye nyanja hii ulithibitisha kwa mapana kuwa na faida kwake baadaye katika kutengeneza kazi zake mwenyewe.

Alama safi ya kielimu ilimzunguka Ibn Taymiyyah ambaye, ukiachilia mbali uwezo wa kuhakiki elimu iliyokuwepo wakati wa enzi zake, aliiwasilisha upya ikiwa na dhamana zote na ufasaha inayomfaa mfikiriaji mbunifu. Akiwa na elimu yake ya ndani kwenye Qur-aan na uoni wake wa chini kwenye malengo na azma za ndani katika Shari’ah na kanuni za maarifa ya Shari’ah, Ibn Taymiyyah aliweza kuwasilisha somo lolote analotaka kulielezea, kwa kutumia vyanzo vya kishari’ah na uwezo wake wa kufahamu mambo mengi.

Hakuna hata kazi yake moja aliyoitengeneza ambayo mpangilio wake haupo mpana kwamba haiwezi kuridhiwa kama ni rejeo kuu (encyclopaedia) kwenye somo hilo. Majmu’ al-Fataawa inatuonesha sisi kwamba elimu kubwa mno ya uelewa wake katika Shari’ah kwa ujumla wake, na Fiqh kwa mahsusi. Kazi zake zinaunganisha ufahamu wa vitu vingi pamoja na ustadi wa kufikiri kama pia ni chakula cha kuwafikirisha kwa wasomaji.

Fasili za kishari’ah na ubunifu wa mawazo ya kishari’ah zilikuwa ni bidii nyengine ambazo nguvu zake Ibn Taymiyyah katika elimu ziliikamata vyema. Akiwa na uelewa makini mzuri katika hili pia, maandiko yake kwenye somo hili unahusisha mijadala kwenye masuala tata ya kishari’ah. Utengenezaji wa maarifa ya kishari’ah wa Ibn Taymiyyah unahusisha Iqtidha’ as-Swiraat al-Mustaqiym kikiwa na mjumuiko wa vitabu vingi vya mawazo ya kishari’ah na idadi kadhaa ya makala ndogo ndogo kama vile Al-Qiyaas na Minhaaj al-Wusuul ilaa ‘Ilm al-Usuul.

Kazi zinazohusiana na ukusanyaji wa misingi ya kishari’ah ya madhehebu tofauti ya kishari’ah yalikaribia kukamilika wakati wa Ibn Taymiyyah. Hata hivyo, alipitia hoja tofauti akiwa na fikra kamili na ustadi wa hali ya juu na ambayo yalikuwa na athari ya kutoa nguvu mpya kabisa kwenye mfumo wa kishari’ah. Katika kuelezea mawazo yake ya kishari’ah, bidii yenye kuendelea ya Ibn Taymiyyah ilikuwa ni kutoa muongozo wa mahitajio ya mabadiliko kwa kuegemea Sunnah. Mawazo ya kishari’ah na hali kadhalika kanuni zinazozitawala zilizoelezewa na Ibn Taymiyyah zimehifadhiwa kwenye vitabu chini ya jina la Fataawa Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah (Majmu’ al-Fataawa li Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah).[9]

 

 

 [1] Al-Ikhlaas: 1

[2] Taahaa: 5

[3] Inatafsirika kama ni ‘Upanga Usio na Ukali katika Kumtusi Mtume’

[4] Kitabu ambacho kina zaidi ya Ahaadiyth 250, Athar 100, utajo wa zaidi ya wasifu wa watu maarufu 600 kutoka historia ya Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah, na mkusanyo wa taarifa kutoka kwenye rejeo zaidi ya arobaini – zote kutoka kwenye kumbukumbu zake, na kitabu chote kimeandikwa katika kujibu tukio moja tu la ambalo Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah (Allaah Amrehemu) alimsikia Mkiristo akimtukana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)!

[5] Maarufu kinajulikana kama ni Dar’ Ta’arudh al-‘Aql wan-Naql’ na ‘Muwafaqat Swahiyh al-Manquul li Swariyh al-Ma’quul,’ na kinajadili uhusiano baina ya hoja na Wahyi.

[6] The Lofty Virtues of Ibn Taymiyyah, ukurasa, 9.

[7] Majmu’ Fatawa Ibn Taymiyyah, Kitabu cha 8, ukurasa 164

[8] Al-Kawaakib ad-Duriyyah, uk.2

[9] Vitabu hivi ambavyo vinafikia 37, kwa hakika ni rejeo kuu (encyclopaedia) katika Maarifa ya Shari’ah za Kiislamu.

 

Share