Kusema ‘Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym’ Baada Ya Kumaliza Kusoma Qur-aan Au Kutaja Aayah; Inafaa?

 

Kusema ‘Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym’ Baada Ya Kumaliza Kusoma Qur-aan

Au Kutaja Aayah; Inafaa?

 

 

SWALI:

 

Tumesikia kwamba mtu anapomaliza kusoma Qur-an kusema ‘Sadakallaahu l adhim’  ni bid’a,  Je ni kweli? Tunaomba jibu la ufafanuzi kwa dalili.

 

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Hakika Muislamu anapaswa kutambua kwamba vitendo vyote vya ibada lazima kupatikane dalili. Pindi isipothibiti dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah, basi kitendo hicho hakifai kama alivyotuonya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

 

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

 

Swali hilo limeshaulizwa kwa Maulamaa wetu wakubwa na wakalijibu vizuri kabisa kwa maelezo bayana. Tunaweka hapa majibu yao kama ifuatavyo:

 

 

Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz (Rahimahu-Allaah):

 

“Sifa zote Njema ni za Allaah.

Sijui (sijapata) dalili yoyote ya ada ya watu kusema: “Swadaqa-Allaahul-‘Adhiwym” wanapomaliza kusoma Qur-aan. Kwa hiyo isifanywe kuwa ni ada. Hakika anayeamini kuwa ni Sunnah kufanya hivyo, basi katika Shari’ah ya Kiislamu ni bid’ah. Kwa hiyo haipasi kutamkwa wala kufanywa ni mazoea au ada.  

 

Ama kuhusu maana ya Aayah: (Akatoa hoja kama hiyo ya Shaykh Ibn ‘Uthaymin Rahimahu-Allaah akaendelea):

((قُلْ صَدَقَ اللّهُ))

((Sema: Swadaqa-Allaah [Amesadikisha Allaah])) [Aal-‘Imraan 3:95]

 

Hii Aayah haizungumzii masuala haya. Bali Allaah Alimuamrisha Mtume Wake kuwafafanulia watu kwamba Allaah Amesema kweli kwa kile Alichosema ndani ya Vitabu Vyake, Tawraat n.k., na kuwa Amesema kweli kwa yote yale Aliyoyasema kwa waja Wake ndani ya Tawraat, Injiyl na Vitabu vingine vilivyoteremshwa.

 

Na Allaah Amesadikisha yote Aliyoyasema katika Qur-aan kwa waja Wake. Lakini hivyo si dalili kwamba inapendekezeka kusema “Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym” baada ya kusoma Quraan au baada ya kusoma Aayah au Surah, kwani haikuripotiwa au kujulikana kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomsomea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Suratun Nisaa mpaka alipofikia:

 

  ((فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَى هَؤُلاء شَهِيدًا))  

 

((Basi itakuwaje pindi Tukiwaletea kutoka kila Ummah shahidi, na Tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa? [yaani dhidi ya Ummah wake)) [An-Nisaa 4: 41]

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Hasbuka [Inatosheleza])) Ibn Mas’uud akasema: “Nikamtazama na kuona macho yake yamejaa machozi” yaani alikuwa akilia kwa sababu ya kutajwa jinsi hali ngumu itakavyokuwa Siku hiyo ya kufufuliwa [kama ilivyo Aayah hiyo].

 

La muhimu ni kwamba hakuna dalili katika Shari’ah kuongezea maneno ya “Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym” anapomaliza mtu kusoma Qur-aan, kwani haikuamrishwa hivyo kuwa ni kufuata mfano wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum). Lakini mtu akitamka hivyo mara moja moja bila ya kukusudia, haina neno kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasadikisha ukweli katika mambo yote. Lakini kufanya kuwa ni ada, desturi, au mazoea kila anapomaliza mtu kusoma Qur-aan kama wanavyofanya aghlabu ya watu siku hizi, ni kwamba hakuna dalili kama ilivyotajwa juu”

 

Kitaab Majmuu’ Fataawa wa Maqaalaat Mutanawwi’ah li Samaahat al-Shaykh al-‘Allaamah ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz (Rahimahu Allaah), mj. 9, uk. 342.

 

 

Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah):

 

“Sifa Njema zote ni za Allaah. Aghlabu ya watu wana tabia ya kumalizia kusoma Qur-aan kwa kutamka: ‘Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym’ (Amesadikisha Allaah Mtukufu). Lakini hiyo hakuna dalili katika Uislamu kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya wala haikuwa ni ada (desturi) ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum), na pia haikutambulikana miongoni mwa Taabi’iyn (Waliowafuata Maswahaba).  Ada hii imeanzia nyakati zilizofuatia kwa sababu  baadhi ya wasomaji Qur-aan waliipenda Aayah inayosema:

 

((قُلْ صَدَقَ اللّهُ))

 

((Sema: Swadaqa-Allaah [Amesadikisha Allaah])) [Aal-‘Imraan 3:95]

 

Lakini kuipenda huko kunapasa kukanushwa  kwa sababu ingelikuwa ni jambo zuri, basi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wake na Taabi’iyn ambao ni wa karne za mwanzo zilizo bora kabisa za Ummah wasingelipuuza kufanya hivyo. Aayah hiyo ((Sema Allaah Amesadikisha)) haimaanishi kwamba maneno hayo yatamkwe baada ya kumaliza kusoma Qur-aan. Ingelikuwa inapasa hivyo, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Angelisema: “Unapomaliza kusoma, sema: Allaah Amesadikisha” kama vile Alivyosema: ((Na Unapotaka kusoma Qur-aan, tafuta (omba) kinga kutokana na Shaytwaan aliyetezwa [aliyelaaniwa])) [An-Nahl 16: 98]

 

Aayah wanayoitumia Ahlul-bid’ah (wazushi) kuipa nguvu kauli yao ya ‘Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym’ baada ya kusoma Qur-aan imeteremshwa hasa kwa muktadha ya kuthibitisha yaliyotajwa kwamba chakula chote kilikuwa ni halali kwa Bani Israaiyl (Wana wa Israayiyl), isipokuwa kile alichokifanya haramu mwenyewe (Israaiyl; yaani Nabii Ya’quub [‘Alayhis-Salaam])

 

((كُلُّ الطَّعَامِ كَانَ حِلاًّ لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ إِلاَّ مَا حَرَّمَ إِسْرَائِيلُ عَلَى نَفْسِهِ مِن قَبْلِ أَن تُنَزَّلَ التَّوْرَاةُ))

 

((Kila chakula kilikuwa halali kwa Wana wa Israaiyl isipokuwa alichojizuilia Israaiyl mwenyewe kabla haijateremshwa Tawraat)) [Aal-‘Imraan 3:93]

 

 

ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akasema:

 

 

  ((قُلْ فَأْتُواْ بِالتَّوْرَاةِ فَاتْلُوهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ))  ((فَمَنِ افْتَرَىَ عَلَى اللّهِ الْكَذِبَ مِن بَعْدِ ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ)) ((قُلْ صَدَقَ اللّهُ فَاتَّبِعُواْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ))

 

 

((Sema [ee Muhammad]: Leteni Tawraat muisome ikiwa nyinyi ni wasema kweli)) ((Na wanaomzulia uongo Allaah baada ya hayo, basi hao ndio madhaalimu)) ((Sema [Ee Muhammad, [Swadaqa-Allaah] Allaah amesema kweli. Basi fuateni mila ya Ibraahiym mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina)) [Aal-‘Imraan 3:93-95

 

 

Ingelikuwa Aayah hiyo imemaanisha kwamba maneno hayo yatamkwe baada ya kusoma Qur-aan, basi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angelikuwa wa kwanza kutambua na kutekeleza hivyo. Lakini kwa vile hali haikuwa hivyo, nasi tunajua kwamba hivyo sivyo ilivyokusudiwa.

 

Kwa kuhitimisha, tunasema kwamba kusema: “Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym” baada ya kusoma Qur-aan ni bid’ah (uzushi) na hivyo Muislamu hapaswi kutamka hayo.

 

Lakini itambulike kwamba kuamini kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesadikisha (Amesema kweli) ni wajibu. Na yeyote asiyeamini au akatilia shaka ukweli Aliosema Allaah basi yeye ni kafiri anayetoka nje ya Uislamu. Tunajikinga na Allaah kutokana na hilo.

 

Ikiwa mtu atasema katika hali ya kawaida: “Swadaqa-Allaah” (Allaah Amesema kweli), mfano imezungumzwa jambo na ikathibitishwa kauli Aliyoisema Allaah, hapo inaruhusiwa, kwa sababu hivyo ni kama ilivyothibiti katika Sunnah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihutubia na Al-Hasan na Al-Husayn wakaja, naye akataremka kutoka katika minbar akawabeba na kuwaweka mbele yake kisha akasema: ((Hakika Allaah Amesadikisha))

 

na baada ya hapo akataja kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ))

((Hakika mali zenu na watoto wenu ni fitnah [mitihani[)) [At-Taghaabun 64: 15] 

 

Mwisho wa kauli ya ibn ‘Uthaymin (Rahimahu-Allaah) iliyorekodiwa kutoka: ‘Izaalat as-sitaar ‘an al-jawaab al-mukhtaar   Ibn ‘Uthaymiyn, 79-80).

 

 

Hivyo, hapo kwenye fatwa ya Shaykh juu tunaona hata ilivyothibiti kwenye Hadiyth ni kuwa Mtume alisema kabla ya kutaja Aayah na si baada ya kutaja Aayah au kumaliza kusoma Qur-aan kama ilivyozoeleka kwa wasomaji Qur-aan wengi na wahadhiri wenye kutoa mawaidha. Kwa hiyo, hawezi mtu kutumia Hadiyth hiyo kama ni dalili au hoja ya kufanya hivyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share