Makusudio Sahihi Ya Aliyekunja Uso (Surat 'Abasa) Kujibu Tafsiri Ya Wapotoshaji

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy

 

Imepokelewa kuwa siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa na wakubwa wa Ma-Quraysh akiwalingania Diyn kwa hima kubwa akitaraji kuwa wakisilimu wakubwa hao, na wanyonge wao watafuata kwa sababu wengi kati ya wanyonge walitaka kusilimu lakini walijizuia kwa kuwaogopa wakubwa wao hao.

 

Wakati huo akatokea kipofu mmoja aliyesilimu tokea zamani aitwaye Ibn Ummi Maktuum (Radhiya Allaahu ‘Anhu), na bila kujua kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameshughulika akawa anampigia kelele kumwambia: “Ewe Mtume wa Allaah, nifunze na mimi katika aliyokufunza Allaah.”

 

Akawa anayarudia maneno hayo, na kwa vile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika kutaka kuwasilimisha viongozi wale wakubwa, akamfinyia uso yule kipofu wala asimsikilize, ndipo Allaah Alipomteremshia aayah za mwanzo za Suuratu-‘Abasa. Allaah Anasema:

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

عَبَسَ وَتَوَلَّىٰ ﴿١﴾

1. Alikunja kipaji na akageuka.

أَن جَاءَهُ الْأَعْمَىٰ ﴿٢﴾

2. Alipomjia kipofu.

وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّهُ يَزَّكَّىٰ ﴿٣﴾

3. Na nini kitakachokujulisha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) huenda akatakasika?

أَوْ يَذَّكَّرُ فَتَنفَعَهُ الذِّكْرَىٰ ﴿٤﴾

4. Au atawaidhika na yamfae mawaidha?

أَمَّا مَنِ اسْتَغْنَىٰ ﴿٥﴾

5. Ama yule ajionaye amejitosheleza.

فَأَنتَ لَهُ تَصَدَّىٰ ﴿٦﴾

6. Nawe unamgeukia kumshughulikia.

وَمَا عَلَيْكَ أَلَّا يَزَّكَّىٰ ﴿٧﴾

7. Na si juu yako asipotakasika.

وَأَمَّا مَن جَاءَكَ يَسْعَىٰ ﴿٨﴾

8. Ama yule aliyekujia kwa kukimbilia.

وَهُوَ يَخْشَىٰ ﴿٩﴾

9. Naye anakhofu.

فَأَنتَ عَنْهُ تَلَهَّىٰ ﴿١٠﴾

10. Basi wewe unampuuza.

كَلَّا إِنَّهَا تَذْكِرَةٌ ﴿١١﴾

11. Laa hasha! Hakika hizi (Aayah) ni mawaidha.

فَمَن شَاءَ ذَكَرَهُ ﴿١٢﴾

12. Basi atakaye ahifadhi na awaidhike.

 

Shia wanasema kuwa makatazo ndani ya aayah hizi si kwa ajili ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu si yeye (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) aliyekunja uso na kugeuka na kwamba yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawezi kukunja uso wala kukosolewa, bali aliyekosea na kukosolewa ndani ya aayah hizo ni ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu).

 

Tatizo ni kuwa baadhi yao hawana uoga hata kidogo, na wako tayari kubadilisha maneno ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala), kwa ajili ya kutaka kuiuza bidhaa yao mbovu.

 

Sisi Tunasema: Lau kama aliyeteremshiwa aayah hizi ni ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu), basi hii ni sifa kubwa kwake, kwa sababu mtiririko wa aayah unatujuulisha kuwa aliyekatazwa ni mtu aliyekuwa akiwalingania watu katika Diyn, na hii ni sifa nzuri hata kama atakatazwa au kukaripiwa kidogo na Mola wake (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Allaah Anasema:

{{Alikunja uso na akageuka. Kwa sababu alimjia kipofu. Na nini kilichokujuulisha (ya kuwa huyo Swahaabah kipofu hahitaji mawaidhah mapya), huenda yeye atatakasika (kwa kusikia mawaidha yako).}} [‘Abasa: 1-3]

 

Kutokana na aayah hizi, (kwa rai ya Shia) inaleta maana kuwa kipofu (‘Abdullaah mwana wa Ummi Maktuum), hakumuendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wala hakumuendea ‘Aliy bin Abi Twaalib wala Maswahaabah (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliokuwepo mahali hapo, bali alimuendea ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kwa ajili ya kutaka kupata mawaidhah na uongofu kutoka kwake. Kwa sababu aliyekunja uso ni ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na si Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Huu ni ubabaishaji wa maneno, kwa sababu aayah zinatufahamisha kuwa aliyejiwa ndiye aliyekunja uso, na haiwezekani kwa mwana wa Ummi Maktuum kumuacha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuendea ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu).

Kama wangelitafakari kidogo tu kabla ya kuandika maandishi yao haya yenye sumu, wangeligundua kuwa maneno yao ni utovu wa adabu dhidi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hadiyth sahihi zinasema kuwa kipofu yule alimuendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku akimuambia: “Nifundishe katika yale Aliyokufundisha Allaah.” Akawa anaendelea kuyakariri maneno hayo, na kwa vile yeye ni kipofu, hakuelewa kuwa wakati ule Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika kutaka kuwasilimisha wakubwa wa Ma-Quraysh waliokuwa naye akiwa na tumaini kuwa huenda mmoja wao atasilimu. Ndipo alipokunja uso na hakumjibu, na hapo ndipo zilipoteremshwa aayah za kumkosoa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na hili ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote anayekatwa maneno wakati akizungumza, na hili ni funzo kwetu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwa tusiwakate watu maneno wanapozungumza kwa sababu hili ni jambo linalokera.

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumdharau kipofu yule wala hakumkaripia kwa kumuambia kwa mfano: “Nyamaza!” au “Ondoka hapa!” bali alikunja uso wake tu bila kumjibu. Lakini Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) alimkaripia Mtume wake na kipenzi chake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kuwa kipofu yule hawezi kuuona uso wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala kujua kuwa amekasirikiwa.

Ikiwa aayah hizi ameshushiwa ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu), kwa nini basi asikaripiwe kwa unafiki na ukafiri wake kama Mashia wanavyoamini kuwa yeye ni mnafiki. Wakati kitendo cha unafiki ni kikubwa zaidi na kinachostahiki zaidi kukaripiwa kuliko kukunja uso.

 

Wengine wakasema kuwa eti mwana wa Ummi Maktum hakuwa akiuliza mambo ya Diyn, bali ni mambo ya kidunia tu ndiyo maana akamuendea ‘Uthmaan!

 

Enyi Shia! Hebu zingatieni vizuri mtiririko wa hizi aayah:

Allaah Anasema:

Lakini anayekukimbilia. (Ewe ‘Uthmaan?) Naye anaogopa (Anaogopa nini?). Wewe unapuuza (Usifanya hivyo, sivyo! Hakika hii (Qur-aan) ni nasaha huenda yeye atatakasika (Akatakasika na nini?).”

 

Kama aayah hizi ametereshiwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu), basi ni sifa kubwa kwake kwa kukimbiliwa na kutakiwa amsikilizishe kipofu yule mawaidhah apate kuongoka.

Kwa kila mwenye kupenda haki, musikubali kudanganywa na tafsiri kama hizi zenye kubadilisha maneno ya Allaah na kupotosha.

 

Hii si mara ya mwanzo kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukosolewa ndani ya Qur-aan tukufu. Na sisi tunaamini kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakosolewi kwa kuwa amefanya kitendo cha dhambi, bali hukosolewa kutokana na kujitahidi kwake sana au kwa ajili ya huruma nyingi aliyonayo au kwa ajili ya kuwataka watu waingie haraka ndani ya Diyn ili waepukane na Moto kama ilivyoelezwa katika Suuratul-Kahf.

Allaah Anasema:

فَلَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ عَلَىٰ آثَارِهِمْ إِن لَّمْ يُؤْمِنُوا بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَسَفًا

{{Labda unajiangamiza nafsi yako kwa kusikitikia hali yao kuwa hawaziamini Hadiyth hizi. Usijihuzunishe hivyo, kama hawataki kuamini basi.}} [Al-Kahf: 6]

 

Ifuatayo ni mifano mingine michache:

Allaah Anasema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكَ ۖ تَبْتَغِي مَرْضَاتَ أَزْوَاجِكَ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

{{Ewe Nabii! Kwa nini unaharimisha Alichokuhalilishia Allaah? Unatafuta kuwaridhi wake zako. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.}} [At-Tahriym: 1]

 

Na Akasema:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُم أَصْحَابُ الْجَحِيمِ ْ

{{Haimpasii Nabii na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina, ijapo kuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa hao ni watu wa Motoni.”

At-Tawbah -113

 

Na Akasema:

مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَى حَتَّى يُثْخِنَ فِي الأَرْضِ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللّهُ يُرِيدُ الآخِرَةَ وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ. لَّوْلاَ كِتَابٌ مِّنَ اللّهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

“Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda baraabara katika nchi. Munataka vitu vya dunia, na Allaah anataka Akhera. Na Allaah ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.}} [Al-Anfaal: 67]

 

Sisi tunaamini kuwa hizi ni sifa njema na fahari kubwa kwa kiumbe kusemeshwa na kufundishwa na Mola wake (Subhaanahu wa Ta’ala), na kukosolewa kwa ajili ya huruma zake na wala si sifa mbaya. Lakini wanayoyatambua haya ni wenye akili peke yao.

 

Allaah Anasema:

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٢٨﴾ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُلْ حَسْبِيَ اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ ۖ وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ

{{Amekufikieni Mtume aliye jinsi moja na nyinyi; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana, kwa Walioamini ni mpole na mwenye huruma. Basi wakidumu kukengeuka (hao makafiri), sema: ‘Allaah Ananitosheleza. Hapana wa kuabudiwa ila Yeye tu. Namtegemea Yeye, na Yeye ndiye Mola wa (hiyo) Arshi iliyo kubwa kabisa.’}} [At-Tawbah: 128-129]

 

 

Ndani Ya Vitabu Vya KiShia

Tafsiri sahihi kuwa aliyekusudiwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimo hata ndani ya vitabu vyao na tafsiri za Ma’ulamaa wao wakubwa na maarufu, na zinakubaliwa na wanavyuoni mbali mbali wa Shia kuwa aliyekusudiwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Anasema At-Tubrusiy ambaye ni mmoja katika Ma’ulamaa wakubwa wa Shia Ithna-‘Ashariyah: “Kule kuambiwa Mtume ‘alayhis salaam kuwa aliukunja uso wake siyo tuhuma, kwake.” [Tafsiyr Majma’al Bayaan, ukurasa 266 Juzuu ya 10]

Tembelea tafsiri ya At-Tubrusiy katika anuani hii: http://www.holyquran.net/cgi-bin/majma.pl

 

Anaendelea kusema At-Tubrusiy:

Aayah hii imeteremshwa kwa ajili ya ‘Abdullaah mwana wa Ummi Maktuum na jina lake ni Shurayh bin Maalik bin Rabiy’ah Al-Fahary, anayetokana na kabila la Bani ‘Aamir bin Luay. Aliyemjia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakati huo alikuwa akiwalingania ‘Utbah bin Rabiy’ah na Abu Jahal bin Hishaam na Al-‘Abbaas bin ‘Abdil Muttwalib na Umayah bin Khalaf akiwalingania wamuamini Allaah, akitarajia kusilimu kwao. Akasema (Mwana wa Ummi Maktuum): “Ewe Mtume wa Allaah, nifunze na mimi katika Aliyokufunza Allaah.” Akawa anamuita huku akiyakariri maneno yale bila kujua kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika na watu wengine. Mpaka kuchukizwa na kukabainika usoni mwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na kukatwa maneno yake kila anapotaka kusema. Ikampitikia nafisini mwake kuwa wakubwa wa makafiri hawa watasema kuwa wafuasi wake ni vipofu na watumwa, akageuka asimjibu na kuwaelekea wale aliokuwa akiwalingania, ndipo zilipoteremka aayah.

 

Akawa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya siku ile akimkirimu na kila anapomuona, husema: “Karibu ewe ambaye kwa ajili yake Amenikosoa Mola wangu.” Kisha humuuliza: “Una haja yoyote?:” Na alimpa ugavana wa mji wa Madiynah mara mbili.

 

Anaendelea kusema At-Tubrusiy ambaye ni mmoja wa Ma’ulamaa wakubwa wa Shia akijibu hoja za wenye madai hayo:

“Kutajwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amekunja uso siyo tuhuma kwake. Kama mtu atasema: ‘Ikiwa kweli amekosolewa, hii ina maana kuwa kumkunjia mtu uso ni dhambi?

 

Jawabu: ‘Kukunja uso au kutabasamu mbele ya uso wa kipofu si kitendo cha dhambi kwa sababu kitendo hicho hakimdhuru, na kwa ajili hiyo si kitendo cha dhambi.’

 

Huenda ikawa Allaah Amemkosoa Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili awe na tabia bora kupita zote na kumtanabahisha juu ya utukufu wa Muislamu anayetafuta uongofu na kumjuulisha kuwa kumuongoza Muislamu apate kuthibiti katika imani yake ni bora kuliko kutegemea kusilimu kwa mshirikina.”

(Mwisho wa kunukuu maneno ya At-Tubrusiy)

 

Mwanachuoni mwengine wa KiShia aitwae Al-Jibaiy anasema: “Ndani yake mna fundisho kuwa hapo mwanzo kitendo cha kukunja uso hakikuwa cha dhambi, mpaka amri ya kukataza ilipoteremka.”

 

Anaendelea kusema:

“Imepokelewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa kila anapomuona ‘Abdullaah mwana wa Ummi Maktuum humuambia: “Karibu karibu, hapana Wallah! Allaah Hatonikataza tena juu yako.” Na alikuwa mpole sana kwake.”

Maneno kama haya pia yamenukuliwa kutoka mmoja katika Ma’ulamaa wakubwa wa Shia Muhammad Haadi Al-Yuusufiy kutoka kwa At-Tubrusiy katika kitabu chake ‘Encyclopedia ya Taariykh’ Juzuu ya 1, ukurasa 494.

 

Na maneno hayo pia yameandikwa na mwanachuoni wa KiShia Al-Majlisiy katika Bihaar al Anwaar, juzuu ya 17, ukurasa wa 78.

 

Yamenukuliwa maneno kama haya pia kutoka kwa mwanachuoni mkubwa wa KiShia katika wakati wetu huu Muhammad Husayn Fadhlullah katika tafsiri yake ‘Wahyul Qur-aan’.

 

Atakaye anaweza kuutembelea ukurasa huo katika mtandao wake unaopatikana penye anuani ifuatayo: http://arabic.bayynat.org.lb/books/quran/abas1.htm

 

Hebu tumsikilize Ayatullah Muhammad Husayn Fadhlullah akiwajibu Mashia wenzake wanaosema kuwa waliokusudiwa katika aayah zile ni ‘Uthmaan au mtu katika watu wa kabila la Bani Umayyah. Anasema mwanachuoni huyu wa KiShia:

“Riwaya inayonasibishwa na Imaam Asw-Swadiq (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa aayah imeteremshwa kwa ajli ya mtu wa kabila la Bani Umayyah haikubaliani na mtiririko wa aayah. Kwa sababu ni wazi kuwa kusudi la aayah hizo ni kuwa aliyekusudiwa ni mtu mwenye kumiliki sehemu muhimu katika kuifikisha risala na kwamba mtu huyo anabeba jukumu la kuwatakasa na kuwafundisha wale waliokwisha hidika na kuikubali risala hiyo kwanza, ili wawe na msingi mzuri na uwezo wa kuifikisha Dini kwa watu, kinyume na wale wasiohidika ambao hawastahiki kupewa juhudi kubwa.”

(Mwisho wa maneno ya Muhammad Husayn Fadhlullah)

 

Kutokana na haya, tunaona kuwa waliosema kuwa aliyekusudiwa katika aayah zile ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) si Masunni peke yao. Bali pia yamesemwa na Ma’ulamaa wakubwa wa KiShia ambao ni At-Tubrusiy, Al-Majilisy, Al-Yuusufiy na Muhammad Husayn Fadhlullah kama tulivyoona.

 

Na hii chini ni anuani ya mtandao unaoitwa Az-Zahraa wa mwanachuoni wao aliyesema uongo juu ya aayah hizi, na ndani ya mtandao huu zimo hotuba mbili za Muhammad Fadhlullah akitamka kuwa aayah hizo ziliteremshwa kwa ajili ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

http://www.mezan.net/sounds_files/sounds1/7/r007.html 

Share