Wengi Si Hoja: Idadi Kubwa Ya Wafuasi Haimanishi Kuwa Jambo Walifanyalo Ni La Haki

 

WENGI SI HOJA*

Idadi Kubwa Ya Wafuasi Haimanishi Kuwa Jambo Walifanyalo Ni La Haki 

 

Imeandikwa Na Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhahu Allaah)

www.alhidaaya.com

 

 

BismiLlaah Al-Hamdulillaah was Swalaatu was Salaamu 'alaa RasuuliLlaah
 

Amma ba'd.

 

 

Wengi Si Hoja

 

Kutokamana na tabia za watu wa zama za Jaahiliyyah (zama za ujinga kabla ya Uislamu) ni kwamba walikuwa wakiangalia kundi lenye wafuasi wengi kuwa ni ushahidi wa jambo walifanyalo kuwa ni la sawa na kundi lenye wafuasi kidogo wakisema hawa wako kwenye batili. Ilikuwa kiakili zao ni kwamba jambo lifanywalo na wafuasi wengi ni la Haki na jambo lifanywalo na wafuasi wachache ni la batili machoni mwao hivi ndivo walivyokuwa wakipima ukweli na uongo.

 

 

Kama hivi ndio kipimo cha kubainishia ukweli na makosa, basi ni makosa kwani Allaah amesema:

 

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾

 

“Na ukiwatii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Allaah. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kusema uongo tu.” (Al-An’aam: 116)

 

Allaah amesema tena:

 

قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٨٧﴾

 

“Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu. Lakini aghlabu ya watu hawajui.”  [Al-A’araaf: 187]

 

Na Allaah Akasema tena:

وَمَا وَجَدْنَا لِأَكْثَرِهِم مِّنْ عَهْدٍ ۖ وَإِن وَجَدْنَا أَكْثَرَهُمْ لَفَاسِقِينَ ﴿١٠٢﴾

 

“Wala hatukuwaona wengi wao kuwa wanatimiza ahadi; bali kwa hakika tuliwakuta wengi wao ni mafaasiq.” [Al-A’araaf: 102]

 

Kwa hivyo, kipimo si idadi ya watu wengi au kidogo kuwa jambo la kishari’ah ya Dini linakuwa ni sawa au makosa. Bali kishari’ah ya Dini tunaangalia ukweli na Haki iko wapi hata kama yuko mmoja pekee yake ndiye atakuwa kwenye Haki na atapaswa kuungwa mkono na watu wote. Na ikiwa idadi kubwa ya watu wako upande wa makosa na batili, ni waajib kuwapinga na watu wasilazimishwe kukubali makosa na upotofu wa watu kama hao. Mazingatio yanapaswa yawekwe kwenye ukweli wenyewe kimakinifu. Na kwa ajili hio ndio Ma’ulamaa wamesema: “Haki haitambuliki kwa njia za watu bali watu wanatambulikana kwaHaki yenyewe’’.

Hivyo, yule aliyesimama katika haki, anapaswa kufuatwa na kuungwa mkono.

 

Kwenye visa Alivyotueleza Allaah kuhusu mataifa yaliyotutangulia, Anatueleza yakuwa kila mara ukweli una wafuasi kidogo kama Alivyosema:

 

وَمَا آمَنَ مَعَهُ إِلَّا قَلِيلٌ ﴿٤٠﴾

 

“Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu.” [Huud: 40].

 

Na kwenye Hadiyth ambayo inayohusiana na mambo ya mataifa yaliopita aliyofikishiwa Mtume, Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema aliona Mtume aliyekuwa na wafusasi kidogo pamoja naye, na Mtume mwengine alokuwa na wafuasi wawili au mmoja wakifuatana naye. Na Mtume mwengine ambaye alikuwa hana mfuasi hata mmoja. [Al-Bukhaariy]

 

Kwa hivyo ki-Dini hatuamui jambo kulingana na wingi wa wafuasi au udogo wao, bali tunatakikana tupime ukweli uko wapi na makosa yako wapi. Kwa hivyo, hata kama ukweli una wafuasi wachache inatakikana watu wote waufuate kwani huko ndio kujiokoa na upotevu.

Makosa ama upotevu hautetewi na kuungwa mkono kwa ajili tu una wafuasi wengi. Hivi ndivyo inatupasa Waislamu kutumia kipimo hiki katika kuhukumu mambo.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

“Uislamu ulianza ugeni na utarudi kuwa mgeni kama ulivyokuja.” [Muslim].

 

Haya yatatokea wakati uovu, fitna, na upotevu utakapozidi. Hakutabakia mtu kwenye ukweli ila wale watakaokubali kuonekana kama wageni kwa watu wao na makabila yao (kwa ajili ya Dini yao). Wataonekana kama watu wa maajabu na wageni kwa watu wao.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa utume wakati ulimwengu umefunikwa na kutomwamini Allaah na upotevu. Na alipolingania watu, ni watu wachache sana walimwamini Mtume na wakawa naye. Ni hadi baadaye kabisa ndio wakazidi kuwa wafuasi wengi. Kabila la ki-Quraysh bila kutaja bara arabu zima lilikuwa kwenye upotevu. Na Mtume alikuwa peke katika kulingania watu. Kwa hiyo walomfuata walikuwa wachache sana katika kulinganisha na idadi ya ulimwengu mzima.

 

Hivyo, hatuangalii kundi lipi lenye wafuasi wengi. Tunaangalia ni kundi lipi lenye kufuata Haki.

Na kuufanikisha ukweli. Naam, ikiwa idadi kubwa ya watu wameshikamana na Haki, basi hayo ni mambo mazuri kabisa. Lakini, mfumo wa Allaah unaonyesha kuwa watu wengi wanashikamana na batili na upotofu.

 

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾

 

“Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi vipi.” [Yuusuf: 103]

 

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾

 

“Na ukiwatii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Allaah. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kusema uongo tu.” (Al-An’aam: 116)

 

*[Kwenye (sharh) kusherehesha maneno ya Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema: “kutokamana na kanuni zao kubwa, walikuwa wakivutika na wengi wanaofanya mambo hayo, wakiona kuwa wengi ndio wako sawa na hivyo jambo maadam lafanywa na wengi, basi ndio sahihi. Kadhalika walikuwa wakihukumu jambo kuwa ni batili au ni jambo la ajabu, kwa sababu tu lafuatwa na wachache.

Hivyo basi, Allaah Akawashushia muongozo kinyume na hivyo walivyokuwa wakiamini na kuhukumu mambo. Na haya yamebainishwa sehemu nyingi ndani ya Qur-aan.”]

 

 

Marejeo:

Sharh Masaail al-Jaahiliyyah (uk. 60-62) cha Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab.

 

 

Share