Matumizi Ya Ijitihaad Kwa Maswahaba Wa Mtume (Radhiya Allaahu ‘Anhum) Na Sababu Za Kutofautiana Kwao

Naaswir Haamid

 

 

Utangulizi

 

Taariykh ya Shari'ah ilianza kuchukua hatamu tokea siku ya mwanzo ambapo Mtume Muhammad alipewa Utume kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kutambulika kuwa ni Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wala hakuna shaka yoyote kwamba Mtume Muhammad amefunga milango ya kuja Mtume mwengine.

 

Shari'ah iliendelea kwa watawala wa mataifa ya Kiislamu baada ya kifo cha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Matokeo yake kulikuwa na vyanzo tofauti vya Shari'ah kwa kulinganisha na kipindi cha Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Vyanzo vikuu vya Shari'ah wakati wa maisha ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) havikuwa tofauti na tunavyotumia sasa; navyo ni Qur-aan tukufu na Sunnah (mwenendo wa Mtume). Hivyo, Shari'ah wakati wa kipindi hichi ilitokana moja kwa moja na hoja za wazi na sio dhana. Pindipo tatizo linapoibuka, kulikuwa na suluhisho mahsusi kutoka Qur-aan ama Sunnah, ambazo hazikuleta mabishano ya mjadala. Kwani daima Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakitoa hoja moja kwa moja. Ingawa kwa upande mwengine Ijtihaad ilitumika, lakini bado vyanzo vikuu vilibaki kuwa ni Qur-aan na Sunnah.

 

 

Matumizi Ya Ijtihaad Miongoni Mwa Maswahaba

 

Ijtihaad ilianza kutumika tokea zama za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini kilikuwa ni chanzo kidogo tofauti na ilivyopewa kipaumbele baada ya kifo cha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa mujibu wa taariykh, Mtume pia alikuwa akifuata Ijtihaad yake lakini pindipo tu anapokosea, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) alikuwa akimrekebisha mara moja. Mfano wa amri ya kuwaachia huru wapiganaji wa Taabuuk iliyotolewa na Allaah kwani hawakutaka kupigana. Na Allaah Aliwatambua kuwa ni wanafiki wa Uislamu.

 

Kwa vile Mtume alitoa baadhi ya amri kwa kutumia Ijtihaad, ndio sababu ya kuwaruhusu Maswahaba wengine kuifanyia kazi. Kwa mfano, Mtume alipompeleka Mu'aadh nchini Yemen[i], mazungumzo yao yalikuwa kama ifuatavyo:

 

MTUME: Kwa kutumia nini utasuluhisha mgogoro?

MU'AADH: Qur-aan.

MTUME: Kama hutopata (kanuni kutoka Kitabu cha Allaah)?

MU'AADH: Kwa kutumia Sunnah ya Mtume wa Allaah.

MTUME: Kama hutopata (kanuni kutoka Sunnah)?

MU'AADH: Nitatumia maoni yangu.

MTUME: Shukurani ni kwa Allaah, aliyempatia mafanikio mjumbe wa Mtume wa Allaah kwa kufanikisha lile Analolipenda Allaah.[ii]

 

 

Sasa Ni Nini Hiyo Ijtihaad?

 

Kwa mujibu wa sifa zake, Ijtihaad inaweza kufasiriwa kama ni matumizi ya mawazo binafsi, ambayo chanzo chake na hoja yake yanatokana moja kwa moja aidha kutoka Qur-aan au Sunnah au vyote. Shari'ah inayofanywa hapa ni lazima iwe inatoka kwa mtu aliyebobea kielimu na ucha Mungu kama vile Mujtahid au Swahabah. Wengine wanaifasiri kama ifuatavyo:

 

Matumizi ya hoja binafsi ya mwanazuoni ili kupata amri mpya ya kisheria.[iii] Pia Ijtihaad inamaanisha kufanya bidii kubwa ya kutoa amri ya kisheria kwa kuegemeza kwenye ithibati yake au kuichambua kutoka vyanzo vyake ambapo ithibati zake au vyanzo vyake havijatolea maelezo ya wazi.[iv]

 

Umuhimu wa Ijtihaad ni kupanua kanuni za jumla kutoka Qur-aan na Sunnah kwani idadi ya aya za Qur-aan zinazojadili kuhusu mambo ya kisheria yamekadiriwa. Hali hiyo pia ni kwa Sunnah ambayo haiendi zaidi ya masuala ya kisheria alfu moja au mbili. Tofauti na masuala ya kisheria ambayo wanakumbana nayo Waislamu, ambayo hayana idadi maalum.

 

Kutokana na kubadilika wakati na Uislamu kuenea zaidi, kulikuwa na haja ya kufasiri adhabu kwa wanaotiwa hatiani. Kulikuwa na sababu ya kutofautisha baina ya wajibu wa kijamii na wa kisheria, wajibu wa yale yanayopendekezwa, yanayozuiwa na yanayoruhusiwa.[v]

 

Ijtihaad ilitumiwa kwa mapana na Maswahaba wa Mtume Muhammad (Radhiya Allaahu ‘Anhum). Sababu kuu ya Khulafaau Raashiduun kuifanyia kazi Ijtihaad ni kupanuka kwa Taifa la Kiislamu hadi sehemu za Persia, Iraaq, Syria na Misri. Ambapo huko walikuwa na mila, tamaduni, miiko, lugha, siasa na uchumi; yote yakiwa tofauti na mazingira aliyoyaacha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kanuni ya Ijtihaad haitolewi tu kama ni mawazo huru kabisa. Ni lazima yapite kutoka Qur-aan kupitia Sunnah, kama hakujaonekana kitu, basi hilo suala ni geni na itabidi lifananishwe na Qur-aan au Sunnah, hapo kati ndipo panapopatikana Ijtihaad.

 

Maswahaba walikuwa na kawaida ya kuifanyia kazi Ijtihaad kupitia Qur-aan au Sunnah. Ijtihaad ilifanyiwa kazi kwenye kuifasiri Qur-aan na Sunnah pamoja na fafanuzi zake. Kama tatizo halijaonekana ama halipo, wanalifananisha na mfano uliomo ndani ya Qur-aan au Sunnah.

 

Kwa mfano, Sayyidna 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alifananisha baina ya kizuka ambaye mumewe hakumpatia kiwango maalum cha mahari kabla ya kufariki na kesi ya mjane aliyeachwa kabla ya kuingiliwa na hakuwekewa wala hakupatiwa mahari yake.

 

Ni kupitia kwa aya ifuatayo ambapo Sayyidna 'Aliy aliilinganisha:

 

{{Si dhambi kwenu kama mkiwapa wanawake talaka ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari (yao). Lakini wapeni cha kuliwaza (kitoka nyumba); mwenye wasaa kadiri awezavyo, na mwenye dhiki kadiri awezavyo. Matumizi hayo (wanayopewa) yawe kama inavyosema Shari'ah. Ndio wajibu kwa wafanyao wema.}} [2:236]

 

Hoja ya kulinganisha aliyoruhusu kuifanya Sayyidna 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) ilikuwa kwamba talaka na kifo ni sababu za kubatilisha mahusiano baina ya mume na mke.

 

Ukusanyaji wa Qur-aan kukusanywa pamoja ni mfano mwengine wa namna Ijtihaad ilivyofanyiwa kazi. Sayyidna Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alikubaliana na Ijtihaad zilizofanywa na Maswahaba wengine za kuikusanya pamoja Qur-aan wakikhofia kuipoteza Qur-aan kutokana na sababu za uhamiaji na kufariki kwa mahaafidh wa Qur-aan. Sayyidna 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alitoa wazo (Ijtihaad) kuikusanya Qur-aan kwa kuiwekea irabu ili kwamba kusitokee khitilafu ya kisomo baina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu.

 

 

Sababu Za Kutofautiana Kwa Ijtihaad

 

Kwa mujibu wa Dr. Hussain Alamid Hassan, yeye ameeleza sababu za kutokea kwa hitilafu baina ya Maswahaba, ambazo tunazifupisha kama ifuatavyo:

 

1) Ufahamu wa maana za maneno ya Qur-aan.

 

2) Matini mbili zenye maana tofauti. Kwa mfano katika suala la eda kwa mwanamke aliyeaachika akiwa mja mzito. Hili linajadiliwa ndani ya matini mbili sawasawa.

 

Ya kwanza ambapo inabainisha kuwa kipindi cha eda kinamalizika baada ya kushusha mzigo (kujifungua) ni:

 

{{Na wale waliokoma kutoka hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayo shaka (katika muda wao wa eda), basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, na (pia ndiyo eda kwa wale) ambao hawajapata hedhi bado. Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa. Na anayemwogopa Mwenyezi Mungu, (Mwenyezi Mungu) humfanyia mambo yake kuwa mepesi.}} [65:4]

 

Na ya pili ni ile inayoeleza kipindi cha miezi minne na siku 10, hata kama hakuzaa:

 

{{Na wale wanaofishwa (wanaokufa) miongoni mwenu na kuacha wake; hawa (wake) wangoje (wasiolewe) miezi minne na siku kumi. Na wanapofikia muda wao (wa kumaliza eda yao hiyo), basi si dhambi juu yenu kwa yale wanayoyafanyia nafsi zao (hao wanawake) kwa yanayowafiki (kufuata) Shari'ah. Na Mwenyezi Mungu Anazo habari za yote mnayoyatenda.}} [2: 234]

 

3) Kiwango cha ufahamu wa Sunnah.

 

4) Kutofautiana katika hoja za ufahamu wa Sunnah. Mujtahiduun waliokuwa wakifanya Ijtihaad walikuwa na mawazo yanayokaribiana. Baadhi ya Mujtahid walihitaji kwamba Mujtahid mwengine ama msimulizi lazima akubaliane na Ijtihaad yake na ale kiapo.

 

5) Tofauti ya mawazo ya kisheria (fatwa) ambapo Swahaba atalinganisha kesi na nyengine kwa kukisia, vivyo hivyo akimtumia Swahaba mwengine na hapo hitilafu hutokezea na kutofautiana na kiwango ama hadhi ya maamuzi.

 

Hizo ni sababu alizozieleza Dr. Hussain. Hata hivyo, wanazuoni wengine wengi wanakubaliana kwamba sababu zilizo hapa chini ndizo zilizosababisha kutofautiana kwao.

 

 

1 - Kupanuka Kwa Taifa la Kiislamu

 

Kutokana na kupanuka kwa taifa la Kiislamu na mabadiliko yaliyotokea kutokana na tofauti ya tamaduni, 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alikataa kukubaliana na mawazo ya Maswahaba wengine. Simulizi ya Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kusafiri pamoja na Maswahaba kwenda Iraaq ni vyema kuitaja. 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliwaambia kwamba watu wa Iraaq sio Waarabu wanaoweza kuisoma Qur-aan vizuri. Wana sauti kama za mingurumo ya nyuki. Alieleza zaidi:

 

"Hivyo, msiwaweke mbali na Qur-aan kwa kufananisha tamaduni kibubusa. Kufanya hivyo kutawavunja (moyo). Isome Qur-aan vizuri na wasimulieni Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah kila mara, na mimi ni mfuasi wenu.[vi]

 

 

2 - Eneo La Mgongano Wa Mawazo

 

Sehemu ambapo masuala yanatokea ni sababu nyengine ya kutokea tofauti ya mawazo baina ya Maswahaba. Mila na tamaduni za Makkah ni tofauti na watu wa Iraaq. Hiyo ndio sababu 'Umar alifanya Ijtihaad na kupingana na Maswahaba wengine wa Makkah au Madiynah kwa sababu ya eneo.

 

Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliifanyia kazi Ijtihaad kwa kusimulia Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah na ili kuaminiwa alikula kiapo. Katika jambo hilo, tunalotambua hapa ni kwamba hakukuwa na lengo la kuwaweka mbali Wairaqi na Qur-aan kwa kuwa tu haifanani moja kwa moja na tamaduni zao na kisomo chao. Hivyo, Maswahaba walihitajika kuwa wakali katika kutoa Ijtihaad kwa kuegemeza ushahidi madhubuti.

 

 

3 - Wakati

 

Wakati unaweza kuwa sababu nyengine ya kutokea Ijtihaad tofauti. Kwa mfano, wakati wa kipindi cha vita, Qur-aan ilikusanywa pamoja kama ni kitabu kimoja chini ya uongozi wa Sayyidna Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) ambapo 'Uthmaan aliweza kubuni irabu za Qur-aan ili kuzuia usomaji wa makosa huku Taifa la Kiislamu likipanuka zaidi.

 

Ndani ya mifano hiyo ya Ijtihaad iliyokuwa ikifanyiwa kazi, tumeona kwamba waliifanyia kazi Ijtihaad kwa kufasiri au kufananisha matini ya Qur-aan na Sunnah. Lakini kutokana na wakati na eneo ambapo hiyo kesi imeibuka, matumizi ya Ijtihaad yalitofautiana.

 

 

4 - Ufahamu Wa Vyanzo Vikuu

 

Sababu nyengine ni uweledi wa Qur-aan na Sunnah pamoja na fafanuzi tofauti. Mfano ni suala la ugawaji wa mali ya hazina (baytul maal). Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alisema kwamba usawa katika ugawaji ni bora. Lakini Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alipingana na Ijtihaad hiyo akiwa na maoni kwamba ruzuku hiyo itolewe kwa mujibu wa haja ya mtu; kwa mfano jihaad, masikini na wale Waislamu wepya walioingia kwenye Uislamu. Hivyo, Maswahaba hawa wawili walitofautiana na namna ya kugawa mali ya hazina.

 

'Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliifanyia kazi Ijtihaad pale alipoteka sehemu nyengine za ardhi kama vile Syria na Iraaq. Alitoa Ijtihaad yake kwamba ardhi hiyo isigaiwe lakini iwekwe Waqf kwa Waislamu.

 

Pia tunaona namna walivyotofautiana Sayyidna 'Uthmaan na 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhum). Hitilafu yao ilitokana na Ijtihaad ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba ngamia wasichukuliwe na mtu mwengine hadi afike bwana wake. 'Umar alitoa hoja kwamba ngamia hao wasichukuliwe na wala hawatapotea. 'Umar aliitumia hoja yake kwa kuwepo athari yake inayoonekana. Kwa upande wa Sayyidna 'Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) hakukubalina na Ijtihaad iliyowahi kutolewa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa sababu athari ya kutowachukua na matumizi yake hayaonekani tena. Hoja yake Sayyidna 'Uthmaan kwamba, iwapo ngamia hao wataachwa bila ya kuchukuliwa, wataibiwa. Matumizi ya matini pamoja na kutotimiza sababu ya matumizi yake hakutoi maslahi kwa jamii, ingawa matini hiyo inadhaminiwa ndani ya Ijithaad ya Mtume Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).[vii]

 

Maswahaba hawakuwa tu wakitumia Ijtihaad bila ya sababu za msingi. Walikuwa wakiifanyia kazi Ijtihaad kwenye kufasiri matini iwapo imeonekana na inahitaji fafanuzi na matumizi yake kwa tatizo lililowakabili.[viii]

 

 

5 - Maana tofauti Ya Matini

 

Pia tunaweza kupata sababu nyengine ya kutofautiana kwa Ijtihaad. Hii sasa inapatikana kutokana na maana tofauti ya matini. Kwa mfano neno "qur’u" ndani ya Qur-aan. Sayyidna 'Umar na Ibn Mas'uud wao wamesema kwamba ina maana ya twahara wakati Zayd ametofautiana kwa maana ya hedhi.

 

Hivyo, tafsiri ya neno "qur’u" linatambulika kuwa lina maana nyingi, wakati tafsiri kwa maana ya hedhi na twahara inaitwa kuwa ni Ijtihaad ya 'Umar, Ibn Mas'uud na Zayd (Radhiya Allaahu ‘Anhum).

 

Kutokana na hitilafu hiyo, Maswahaba walitofautiana na hukumu ya kipindi cha eda cha hedhi ya mwanamke aliyeachwa. 'Umar na Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu ‘Anhum) waliitumia Ijtihaad katika somo hilo wakifananisha "qur’u" na twahara kuwa kipindi cha eda kinamalizika baada ya kuhitimisha vipindi vitatu vya twahara.[ix] Zayd kwa upande wake anaifasiri kumaliza kipindi cha eda kwa kuanza kipindi chake cha tatu.

 

Maswahaba hawa watatu, wote walitoa hoja zao katika kufikia hukumu ya kisheria, ambapo ilizuka hitilafu katika maamuzi yao kutokana na ufahamu tofauti wa neno "qur’u".

 

Kama ambavyo tumeifasiri Ijtihaad kwa maana ya Mujtahid kuelewa hukumu ya Shari'ah na kuvitumia vipengele hivi kutokana na vyanzo vikuu ambavyo vitatoa hukumu mpya. Tunaweza kuelewa kwamba, Mujtahid yeyote alikuwa huru kutoa na kuitumia Ijtihaad. Na kwa vile ni toleo la kibinaadamu, watu waliruhusiwa kuitolea hoja. Hili liliwafanya Maswahaba kutojipa hadhi ya kuifanya hoja yake kuwa yenye nguvu kuliko ya mwengine. Hivyo, hawakufungika na Ijtihaad. Kila mtu alikuwa huru kutoa Ijtihaad isipokuwa tu iwe inaenda sambamba na Qur-aan na Sunnah. Kwa mujibu wa Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu), mawazo (Ijtihaad) ni maarufu baina ya Mujtahid wote. Ni ushahidi kwamba wanazuoni ama Maswahaba daima walitangaza na kutambulika kwamba Ijtihaad zao zilikuwa sahihi au sio sahihi.[x]

 

 

 

Hitimisho

 

Maswahaba kama tulivyoeleza hapo juu ni kwamba walihitalifiana kutokana na wakati na eneo. Kwa mfano Sayyidna Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu), katika kipindi chake cha Ukhalifa hakushuhudia upanuzi mkubwa wa Taifa la Kiislamu hali ya kuwa Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alilishuhudia hilo. Sambamba na Sayyidna 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu), ambapo kipindi chake cha utawala kilikuja na mizozano kadhaa baina ya Waislamu wenyewe.

Pia tofauti ya kiwango cha ufahamu wa Sunnah, ambapo baadhi ya Maswahaba wa Mtume (Radhiya Allaahu ‘Anhum) walikuwa karibu naye kuliko wengine ambao walijishughulisha zaidi kuhifadhi Qur-aan ndani ya vifua vyao.

 

Sunnah ilikusanywa na kuwekewa kumbukumbu kwa kuandikwa. Sunnah haikuwa na maelezo ya hadhi ya maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na kila Swahaba alitofautiana na mwenziwe kutokana na ufahamu wake. Hili lilisababisha kuwepo na kiapo wakati wa utawala wa Sayyidna 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Kwani Hadiyth zilikuwa ni nyingi mno na nyengine alisingiziwa tu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kwa maelezo hayo, kuanzia taariykh ya Ijtihaad hadi sababu za hitilafu ya maamuzi ya Ijtihaad baina ya Maswahaba. Tunaweza kutambua kwamba Ijtihaad ilikuwa muhimu wakati huu, kwani ilitoa nafasi ya fafanuzi zaidi na iliyo pana ndani ya maeneo ambayo Uislamu haukuota mizizi sana kama ilivyo kwa Makkah na Madiynah. Hivyo, kwa kutumia Ijtihaad Waislamu waliweza kuzielewa amri kwa uwazi.

 

Kwa vile Ijtihaad ni mawazo binafsi, haikutambulika kuwa ni miongoni mwa chanzo kikuu mwa vyanzo vya Shari'ah. Ilipewa hadhi yake ya juu iwapo Maswahaba tofauti watakubaliana na Ijtihaad mpya.

 

Ijtihaad ilisuluhisha migogoro na kutoa mawazo bora kabisa ambayo yalirithishwa hadi kwa Waislamu wa leo.

 

Kwa kuwa Ijtihaad ilifanyiwa kazi, ililazimika kupitia mianya ya hitilafu lakini iliyo finyu kabisa wakati wa Khulafaau Raashiduun. Hivyo, walikhitalifiana katika maamuzi.

 

Kutokana na maelezo hayo juu, tunaweza kukhitimisha kwa ufupi tu kwamba sababu kuu ya kutokea hitilafu za Ijtihaad baina ya Maswahaba ni elimu na wakati. Nyengine ni mawazo binafsi ya kisheria, mtindo wa kuchambua na kutoa hoja. Hizo zilikuwa ni sababu ndogo ndogo.

Kwa kweli matumizi ya Ijtihaad yalienea kwa kasi bila ya kujali mipaka baada ya kifo cha kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kuwa maeneo mepya yaliongezwa na kutekwa na kufanya Taifa la Kiislamu kukuwa zaidi.[xi]

 

[i] Japokuwa tukio hili ambalo ni maarufu sana linatumika sana kama hoja kuu ya Ijtihaad, wanachuoni wa Hadiyth wameona kuna udhaifu wa riwaya hiyo.

 

[ii] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 2.

[iii] Dr. R. K. Sinha, The Muslim Law, Toleo La 4, Uk. 30.

[iv] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 22.

[v] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 39.

[vi] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 40.

[vii] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 45.

[viii] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 46.

[ix] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 46.

[x] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 42

[xi] M. Al-Haj Ahmed, The Urgency Of Ijtihaad, Uk. 32.

Share