Zingatio: Rabb Awatakabalie Hijjah Zao Pamoja Na Sisi Kughufuriwa Madhambi Yetu

Rabb Awatakabalie Hijjah Zao Pamoja Na Sisi Kughufuriwa Madhambi Yetu

Naaswir Haamid

 

Hakika Uislamu wetu umetimia na wala hakuna Diyn inayotoa usawa wa binaadamu zaidi ya Uislamu. Wamejumuika weusi kwa weupe katika ‘ibaadah ya Hijjah kwa lengo la kutafuta radhi za Muumba. Ni ‘ibaadah iliyoasisiwa na Nabii ‘Ibraahiym ('Alayhis Salaam).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Na (taja) Tulipomwonyesha Ibraahiym mahali pa Nyumba; Al-Ka’bah, (Tukamwambia): “Usinishirikishe na chochote; na twaharisha Nyumba Yangu kwa wafanyao Twawaaf, na wanaosimama kuswali na wanaorukuu na kusujudu.}} [Suwratul-Hajj: 26]

 

Nabii ‘Ibraahiym ('Alayhis Salaam) akaamrishwa yeye pamoja na Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuisimamisha nguzo ya Hijjah:

{{Na tangaza kwa watu Hajj; watakufikia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, watakuja kutoka katika kila njia pana za milima zilioko mbali kabisa.}} [Suwratul-Hajj: 27]}

 

Muumba wetu hatutakii mabaya kwa kutuwekea ‘ibaadah hii, bali lengo ni kushukuru neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pamoja na kughufuriwa madhambi yetu:

{{Ili washuhudie manufaa yao; na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kwa yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. Basi kuleni humo, na lisheni mwenye shida fakiri.}} [Suwratul-Hajj: 28-29]}

 

Kwa wasiopata nafasi ya kwenda kuhijji, basi wamewekewa Swawm ya ‘Arafah ili kupata nafasi ya kujumuika na Mahujjaaji pamoja ‘ibaadah ya Hijjah kwa ujumla wake. Hivyo, ni muhimu kwa Waislamu kushikamana na funga hii ‘adhiymu. Bila ya kusahau kwamba ‘ibaadah hii ya Hijjah inaambatana na sikukuu ya ‘Iydul-Adhw-haa. Hivyo tunawahimiza Waislamu wote kushikamana na mwenendo sahihi wa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye sherehe hizi za ‘Iydul-Adhw-haa.

 

Bila ya shaka hii ni nafasi ya kuonesha umoja wa Waislamu ulimwenguni bila ya kizuizi chochote. Mahujjaaji wote wamevaa sawa sawia wakiitikia wito wa “Labbayk” kuomba maghfira na radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Ni kipindi kigumu kwa Mahujjaaji kwani sio wote wanaokamilisha vilivyo a’amali za Hijjah. Tunawaombea Mahujjaaji wote Hijjah zenye kukubaliwa – Aamiyn.

 

'IYD MUBAARAK

Tunawaombea Mahujjaji wote,
Hajj yenye kutaqabaliwa na
wawe ni wenye kufutiwa madhambi yao.

 

Pia tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Atughufirie madhambi yetu
na wale wasiopata nafasi ya kutekeleza ‘ibaadah hii
Awajaalie ni wenye kuitimiza kabla ya kufariki kwao.

تقبل الله منا ومنكم

 

 

Share