Utumiaji Wa Mpira (Condom)

 

SWALI:

 

jee ! uko udhuru  wa kuruhusiwa  mwanamume  kuweza kuvaa "condom" wakati anapotaka  kumwingilia mke wake? Tafadhali kama uko udhuru huo naomba unifahamishe nipate "kustafidi".
wabillah Taufiki.

 


 

JIBU:

Kuhifadhi aina ya kiumbe mwanaadamu ndio lengo la msingi la ndoa, na hili litapatikana kwa kuzaana. Hivyo, Uislamu unahimiza kupata watoto na hii ni baraka kwa aina yoyote ambayo Allaah Atakupatia, wasichana au wavulana. Hata hivyo Muislamu anaruhusiwa kupanga familia yake kwa sababu zinazokubalika kishari'ah na kidharura.

Mtume صلي الله عليه وآله وسلم amesema:

“Oeni wenye mapenzi wenye kuzaa, kwani mimi nitajifakharisha kwa wingi wenu juu ya Umma wengine Siku ya Qiyaamah.” [Abu Daawuwd, An-Nasaaiy, na Shaykh Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Adaabuz-Zafaaf].

Katika khitilafu ambazo zipo baina ya Waislamu wakati huu wetu wa leo ni mas-alah ya kuzuia kizazi. Wengi hawakubali au wana shaka kuhusu jambo hili kuwa lafaa au halifai.

Kuzuia kizazi ni aina mbili:

1. Kuzuia kabisa kabisa (permanently).

2. Kuzuia kwa muda (temporarily).

 

Namna hii ya kwanza ni jambo ambalo lisilokubalika katika shari'ah yetu isipokuwa kwa dharura kwa misingi ya kishari'ah.

Kuna kanuni za kiuswuwl isemayo, adh-dhwaruuraat tubiyhul mahdhwuraat (Dharura hulalalisha kilicho haramu) na akhaffu dhwararayn (kitu chenye madhara madogo zaidi katika vitu viwili ambazo zina madhara). Ama hii sampuli ya pili inakubaliwa na shari'ah ya Kiislamu. Na hata katika zama za Mtume صلي الله عليه وآله وسلم baadhi ya Maswahaba walikuwa wanafanya jambo hilo. Njia ya kawaida iliyokuwa ikitumika wakati wa Mtume صلي الله عليه وآله وسلم ni ‘azl (coitus interruptus – azili, chomoa kumwaga nje), hiyo kuzuilia kuingia ndani kwa mbegu za kiume. Maswahaba walikuwa wanafanya hivyo na Qur-aan ilikuwa inaendelea kuteremshwa.

"Imepokewa kwa Jaabir رضي الله عنه ambaye amesema: “Tulikuwa tunafanya ‘azl wakati wa Mtume صلي الله عليه وآله وسلم na Qur-aan ilikuwa inateremshwa.” [Al-Bukhariy na Muslim].

Katika riwaya ya Muslim: “Tulikuwa tukifanya ‘azl wakati wa Mtume صلي الله عليه وآله وسلم. Alikuja kujua lakini hakukataza.”

"Kuna mtu aliyekuja kwa Mtume صلي الله عليه وآله وسلم akimwambia: “Nina kijakazi. Nami napenda kile kinachopendwa na kila mwanamume, lakini sitaki ashike mimba, hivyo ninafanya azl. Mayahudi wanasema hii ni njia ndogo ya kuwazika watoto wakiwa hai”. Mtume صلي الله عليه وآله وسلم alisema: “Mayahudi wamekosea. Allaah akitaka kumuumba mtoto, huwezi kuzuilia.” [Abu Dawud, an-Nasaai, at-Tirmidhy na Ibn Maajah].

Hii inamaanisha kuwa japokuwa mtu atafanya ‘azl lakini huenda tone la manii likabakia kwenye sehemu za siri za mwanamke bila kutanabahi, hivyo kupelekea mwanamke kutunga mimba.

Katika kikao cha Maswahaba ambacho ‘Umar رضي الله عنه alikuwepo pamoja na wengineo kama kina Az-Zubayr na Sa‘ad رضي الله عنه. kuna mtu ambaye alisema: “Baadhi ya watu wanasema kuwa ‘azl ni aina ndogo ya kumzika mtoto akiwa hai”. ‘Ali رضي الله عنه alisema: “Hivyo sivyo kabla ya kumalizika vipindi saba: kuwa ni matokeo ya mchanga, tone la manii, pande la damu, pande la nyama, kisha mifupa, baadae mifupa ikavikwa nyama na kisha akafanywa kuwa kiumbe chengine kabisa (‘Aliy   رضي الله عنه alikuwa anafupisha Qur’an 23:12–14)”. ‘Umar رضي الله عنه alisema: “Umesibu, Allah akupe umri mrefu” (Abu Ya‘la). Bali wanachuoni wakubwa kama Imaam Ar-Ramliy mwenye sharh ya Minhaaj wamekubali hilo (tazama uk. 279 wa Bughyatul Mustarshidiyn).

Hivyo, mbali na ‘azl, Allah ameweka kipindi cha miaka miwili kwa mama kumnyonyesha mtoto wake. Na hii ni njia ya kupanga watoto kwa sababu mara nyingi mama wanaonyonyesha huwa hawapati ada yao ya kawaida ya mwezi hivyo kuondoa uwezekano wa kutunga mimba miaka miwili inayofuata baada ya kuzaa. Huo ni mpango wa kimaumbile ambao umewekwa na Muumbaji ili kuwapatia watoto fursa ya kunyonya na hivyo kuinukia katika siha nzuri kabisa.

 

Zipo sababu ambazo zinakubalika kishari'ah katika kuzuilia mimba isiingie. Sababu zenyewe ni kama zifuatazo:

1. Ikiwa ipo hofu kwamba kushika mimba na kuzaa huenda ikahatarisha maisha au siha ya mama. Hii ni kutokana na ujuzi wake wa awali juu ya hilo au rai ya daktari baada uchunguzi wa kina. Daktari anatakiwa awe mwenye kutegemewa, mwaminifu na akiwa atakuwa ni Muislamu itakuwa aula zaidi.

Allaah Anasema:

وَلاَ تُلْقُواْ بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ وَأَحْسِنُوَاْ إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ

 

“Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema.(2:195).

Na Amesema tena Aliyetukuka:

وَلاَ تَقْتُلُواْ أَنفُسَكُمْ إِنَّ اللّهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا  

“Wala msijiue (wala msiue wenzenu). Hakika Allaah ni Mwenye kukuhurumieni.” (4:29).

 

2. Kuhofia siha ya watoto

"Imepokewa kwa Usaamah bin   Zayd رضي الله عنه kwamba alikuja mtu kwa Mtume صلي الله عليه وآله وسلم na kumwambia: “Mimi nafanya azl na mke wangu.” Mtume صلي الله عليه وآله وسلم akamuuliza: “Kwa nini?” Alisema: “Ninahofia watoto wake,” au inawezekana alisema: “kwa watoto wake.” Mtume صلي الله عليه وآله وسلم alisema: “Lau mimba ya mama mwenye kunyonyesha ingekuwa na madhara, ingewadhuru Wafursi na Wayunani.” [Muslim].

 

3. Kujikinga na magonjwa angamizi ya kuambukiza kama Ukimwi.

Anasema Allaah Aliyetukuka:

وَلاَ تَقْتُلُواْ أَنفُسَكُمْ إِنَّ اللّهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا  

“Wala msijiue (wala msiue wenzenu). Hakika Allaah ni Mwenye kukuhurumieni.” (4:29).

 

4. Hofu ya kuwa mimba mpya au mtoto mwengine atamdhuru  mtoto mwenye kunyonya. Mtume صلي الله عليه وآله وسلم aliipatia jina la ghiylah lile tendo la ndoa na mama mwenye kunyonyesha, akifikiria kuwa mimba itaharibu maziwa au itamdhoofisha mtoto anayenyonya. Mtume صلي الله عليه وآله وسلم alikuwa anajali sana maslahi ya ummah wake na kuwakataza watu katika yale yenye adhara. Alisema:

“Muiwaue watoto wenu kisirisiri kwani ghiylah inamshinda mpandaji na kumtupa chini ya farasi”. [Abu Daawuwd].

 

Inasemekana ya kwamba mtoto kama huyo anapata madhara baadae kama vile mtu aliyeangushwa na farasi. Lakini Mtume صلي الله عليه وآله وسلم hakukataza kwa wanandoa kujamiiana kwani hii ingekuwa ni nzito sana kwa wanaume.

 

Kwa zama zetu hizi zipo njia nyingi za kuzuia kizazi ambazo wakati wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  zinatekeleza lile lililokusudiwa.  Miongoni mwa hizo ni vidonge, mpira (kondom) na nyinginezo.  Inatakiwa ieleweke vizuri kuwa Uislamu unamlinda mtumiaji asije akadhurika.  Hivyo ikiwa unataka kutumia vidonge ni lazima uonane na daktari mzoefu na mwaminifu na akipatikana Muislamu itakuwa bora zaidi.  Maana dawa nyingi zina madhara makubwa kwa hiyo tuwe na tahadhari sana

 

Katika utumiaji wa njia hizi za kuzuia kizazi inatakiwa ifanywe kwa ridhaa ya mke isiwe mume anajali maslahi yake tu kwani kuna maslahi ya mke ambayo ni lazima yachungwe vilivyo. Kwani yeye pia ana haki ya kupata starehe ya kimwili na pia kuamua kama anataka mtoto mwengine au hataki. ‘Umar رضي الله عنه alikataza ‘azl bila ruhusa ya mke. Na hii ilikuwa ni kumpatia haki mke wakati ambapo hakuwa na haki aina yeyote.

 

Mwisho kabisa tunatoa tanbihi ya kwamba kwa ule utafiti uliofanywa Ufaransa takriban miaka sita – nane iliyopita inaonyesha ya kwamba kondomu hazizuii mimba kabisa kwa sababu tundu zilizomo katika mpira ni kubwa. Sasa ikiwa kondomu haizuii mimba, je, virusi vya ukimwi. Na inafahamika kuwa virusi vidogo sana kuliko manii.

 

Na ieleweke kuwa siku hizi katika nchi za ulimwengu wa tatu kondomu zinatolewa bure. Tunaweza kujiuliza kwa nini? Sababu kubwa ni watu wazame katika maasi ya   ngono na hivyo wasifikirie jengine isipokuwa kukidhi uchu wao. Hali hii inaleta maafa makubwa sana katika jamii  kama  watoto wa nje ya ndoa ambao wanazurura mitaani, wanaoambukizwa ukimwi kuongezeka, ujambazi kuzidi, na maafa mengine mbali mbali.

 

Wa Allaahu A’lam

 

Share