Kumnyonyesha Mtoto Ambaye Sio Wa Kumzaa

SWALI:

Assalamu alaikum warahmatullwahi wabarakatuh


Naomba kupata maelezo ya kina juu ya mwanamke kumnyonyesha mtoto ambae si wa kumzaa. Ahsante


JIBU:

Shukrani zote Anastahiki Allah, sala na salamu zimfikie kipenzi Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Ahsanta kwa kaka yetu yetu kuuliza swali hili ambalo ni zuri na mara hutokea matatizo katika mas-ala ya ndoa ikiwa habari kuhusu mas-ala ya kunyonya hayajaeleweka. Jambo hili la kunyonyeshwa mtoto na mama mwengine lilikuwepo hata kabla ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alinyonyeshwa na Thuwaybah na baadae Haalimah As-Sa‘adiyah.

Na hata katika miji ya Waislamu hapa kwetu Afrika Mashariki jambo hili lilikuwa likifanywa kwa kiwango kikubwa hasa katika mji wa Amu mpaka katika kipindi cha uhuru. Kwa hivyo ni jambo ambalo lipo katika Uislamu. Ndio Allah Akatuekea kanuni za kuoa na watu ambao hatuwezi kuwaoa pale aliposema:

“Na mama zenu waliokunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya” ().

 Na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: “Kilichokuwa haramu kwa nasaba ni haramu kwa kunyonya” (Al-Bukhari na Muslim).

Ni haramu kwa Muislamu kumuoa mwanamke aliyemnyonyesha akiwa mchanga kabla hajaacha kunyonya na maziwa yakiwa ndio chakula cha pekee. Na kwa mujibu wa Hadithi zilizoko zinaonyesha kuwa mtoto ambaye atanyonya mara tano mpaka kushiba basi hataweza kumuoa mwanamke yule wala mabinti zake na akiwa ni msichana basi vijana vya yule mama. Hivyo, mtoto kunyonyeshwa na mama mwengine haina tatizo kabisa katika Uislamu, lakini inatakiwa mama awaeleze watoto wake kuwa amemnyonyeshaa mtoto Fulani ili isije watu hao kutangamana katika ndoa.

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share