Mtu Asiye Swali Kuitwa Kafiri

SWALI:

Inshallah Mwenyezi Mungu awajalie kila la kheri. Ninataka kuuliza kuhusu hukumu ya mtu aliacha swalah. Katika Mawaidha yaliotolewa na Sheikh Naasir Bachu ameeleza kuwa mtu aliacha swalah ni kafiri na hukumu yake kuuwawa.

Swali langu ni Kama makafiri ambao hawakuamini Uislam hawapasi kuuwawa, vipi mtu/muislam aleye iacha swala auwawe.

Tashukuru sanakama mtanifafanulia zaidi. Inshallah Mwenyezi Mungu atuongeze katika haki. Amini 

 

 JIBU:

Wa Alaikumu Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Kulingana na suali lako, makafiri ambao hawakuamini Uislamu hawapasi kuuawa, vipi Muislamu aliyeacha Swalah auawe?

Ni kwa sababu kafiri halazimishwi kuingia katika Uislamu kama alivyosema Allaah سبحانه وتعالى

}}لاَ إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ{{

 {{ Hakuna kulazimishwa (mtu kuingia) katika Dini}}

Al-Baqarah 2:256

Lakini mtu akishasilimu au akiwa ni Muislamu harusiwi tena kutoka.  Dini si kitu cha mchezo, mtu kuingia na kutoka atakavyo. Mwenye kutoka katika Uislamu huitwa “murtad” na hukmu yake ni kuuliwa. Kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   

  ‏((‏من بدل دينه فاقتلوه))

  ((Mwenye kubadilisha dini yake (ya Kiislamu) muueni )).

(Al Bukhari 6922, Abu Dawuud 4329, At-Tirmidhiy 1483).

Ama kuhusu mtu asiyeswali (Taariku Swalah), Ma'ulamaa wame wagawanya vikundi viwili:

a.  Mwenye kuacha kwa kukanusha uwajibikaji wa Swalah; huyu ni kafiri kwa makubaliano ya Ma'ulamaa wote.

b.  Mwenye kuacha kwa uvivu au kwa kupuuza pamoja na kuwa anaamini kuwa Swalah ni nguzo miongoni mwa nguzo tano za Kiislamu, na kuwa ni wajibu kwake kuswali.

  Huwa yeye ni kafiri. Wamethibitisha kauli yao hii kwa hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliposema:

((بين الرجل وبين الشرك والكفر ترك الصلاة)) مسلم

((Baina ya mtu na ukafiri na shirki, ni kuiacha Swalah)) (Muslim).

 Na pia akasema:

  ‏ ((‏إن العهد الذي بيننا وبينهم الصلاة فمن تركها فقد كفر)) أحمد

((Ahadi ambayo iko baina yetu na baina yao (makafiri) ni Swalah, na mwenye kuiacha basi amekufuru)) (Ahmad ).

Kuwa ni 'asi au faasiq. Kwa kuwa mara anaswali na mara anaacha, anaswali kwa wakati anaotaka yeye, kwa kuchelewa kuswali bila ya sababu za kisheria, na kadhalika. Kikundi hiki wamethibitisha maneno yao kwa kauli ya  Allaah سبحانه وتعالى

}}فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ{{   }} الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ{{

      {{Adhabu kali itawathubutikia wanao swali}}.

      {{Ambao wanapuuza Swalah zao (kwa kutoswali wakati ulio pangwa)}}.

      Al-Ma'uun 107: 4-5

Hivyo, akiwa mtu yu katika kundi hili atakuwa bado hajatoka katika Uislamu na anaporudi kutekeleza ibada huwa hana haja ya kutoa shahada nyengine.

Wa Allaahu A'alam

 

Share