Je, Inafaa Mume Kumlazimisha Mke Kuvaa Niqaab?
SWALI:
Asalam Aleykum Warahmatullah Wabarakat
Ninavyojua ni kwamba mwanamke anafaa kujistiri kila pahali isipokuwa uso na vitanga vya mikono. Sasa nataka kuuliza ni nini hukumu ya kuvaa hijab na niqab, na jee inafaa mume wako kukulazimisha kuvaa niqab?
Shukran.
JIBU:
BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa
Kuna ikhtilaaf za wanachuoni kuhusu mas-ala haya, kuna waliosema kwamba kujifunika kwa mwanamke ni kujifunika kila sehemu ya mwili isipokuwa uso na viganja vya mikono. Lakini wengine wameona kwamba ni wajib mwanamke kujifunika kila kitu mpaka uso kutokana na dalili katika Qur'aan na Sunnah. Dalili kutoka katika Qur'aan ni kutokana na maneno ya Allaah سبحانه وتعالى yafuatayo:
((يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا))
((Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Al-Ahzaab:59]
Jilbaab ni nguo ambayo mwanamke anaivaa juu ya khimaar kutoka kichwani na inashuka kumfunika uso wake.
'Aliy bin Abi Talhah amerepoti kwamba Ibn 'Abbaas amesema kwamba Allaah سبحانه وتعالى Amewaamrisha wanawake waumini wajifunike nyuso zao kutoka vichwani mwao wakiacha jicho moja tu, wanapotoka nje ya nyumba zao kwa ajili ya kutafuta mahitajio
Kuna Hadiyth nyingi zinazoonyesha kwamba maana ya kujifunika kwa wanawake ni kujifunika kila kitu mpaka uso:
((Bibi 'Aishah رضي الله عنها amesema ilipoteremeshwa aya:
((...وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ...))
((….Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao….)) [An-Nuur 24.31]
Wanawake wa Ki-Muhaajirina walichana na kukata sketi zao pembeni ili kufunikia nyuso zao )) [Al-Bukhaariy]
Vile vile Hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliyosema ((Haifai mwanamke kujifunika uso wake katika Ihraam au kuvaa burqa)) Hii inaonyesha kwamba wanawake walipokuwa nje ya Ihraam walikuwa wakijifunika nyuso zao.
Hadiyth nyingine kutoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها kwamba ((Tulikuwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika Ihraam, na ilikuwa kila wakipita wanaume tulikuwa tukiteremsha khimaar zetu vichwani kufunika nyuso zetu na walipopita tukijifunua))
Kwa hiyo mche Allaah سبحانه وتعالى kwa kuitikia amri mbili; amri kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى na amri kutoka kwa mume wako. Bila shaka hii ni kheri kwako, kwani mumeo hakuamrishi jambo ovu bali ni jambo jema la stara zaidi na halali. Kwa hivyo, ni bora kumtii na kumridhisha kuliko angekuwa anakulazimisha katika jambo la kumuasi Mwenyeezi Mungu.
Na kumtii mume wako bila shaka itampa furaha mumeo na azidi kuwa na mapenzi na wewe na uzidi kuijenga nyumba yako katika furaha na amani. Na pia utakapotekeleza amri hizo utakuja kutambua faida nyinginezo na kuridhika nafsi yako. Kuna wangapi waliokuwa hawajifuniki mwanzo uso, na baada ya kuanza kujifunika wanajuta kwanini wamechelewa muda wote huo kujifunika!
Vile vile hii ni njia mojawapo ya njia za kufunga milango ya shaytwaan kwani itakupunguzia usumbufu na maudhi majiani kwa wale wahuni na wenye uchu wa haramu. Na wewe ndiye utakayekuwa ni sababu ya kuwazuia kutazama yaliyo haramu kwao hivyo utajiepusha na dhambi hizo.
Na Allah Anajua zaidi.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


