Wanaogopa Kuvaa Hijaab Wasije Kufelishwa Mitihani

 

SWALI:

 

A.a. kwanza napenda kuwapongeza kwa kuelimisha jamii kupitia website hii. Napenda kuuliza swali lifuatalo. Mimi ni mwanafunzi nasoma nje ambapo chuoni (university) kwetu miaka mingi tulikuwa haturuhusiwi kuvaa hijabu wasichana kutokana na sheria ya nchi, ila sasa hii sheria wameiondosha tunaruhusiwa ila walimu wetu wengi wanapinga na kutokana na pingamizi za walimu hawa sie tunaogopa kuvaa hijabu tukiwa darasani kwa kuhofia kufelishwa...je hukmu yetu nini??? Na sisi kama waschana tunatarajia kuwa wasomi na kuendeleza jamii yetu ya kiislaam. Naomba ushauri wenu.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuvaa hijabu darasani. Tunadhani kulingana na swali lako unaashiria kuwa unasoma Uturuki.

Hakika ni makosa ambao madada wengi hufanya kwa kwenda kusoma katika vyuo ambavyo havimtambui Allaah Aliyetukuka mbali na kwamba wao wenye hizo nchi na vyuo hivyo wanajiita ni Waislamu. Si hayo tu bali wanapigana na kupingana na shariy'ah ya Allaah Aliyetukuka.

Amri ya Hijaab ni ya kutoka kwa Mola Muumba ambaye ndiye Mwelewa kwa maslahi yetu hapa duniani. Anasema Aliyetukuka:

Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe” (33: 59).

 

Katika amri inayotoka kutoka kwa Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tufahamu kuwa huwa hatuna tena khiyari. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allaah na Mtume Wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi” (33: 36).

 

Hivyo, hilo suala lenu lishaamuliwa khiyari ni yenu sasa mnahofia kufeli hapa duniani au kufeli kesho Akhera.

 

Mara nyingi huwa sisi tuna khofu kwa jambo lisilokuwepo na lisilo la msingi na tukasahau kuwa Msaidizi wa kihakika ni Allaah Aliyetukuka na si mwalimu wa chuo fulani hapa duniani, mwalimu ambaye mwenyewe ana yake ya kwenda kumjibu Muumba kwa kuchukua madaraka Yake hapa ulimwenguni.

 

Ushauri wetu mwanzo ni kuwa maadamu dola yenyewe ishapitisha kuwa mnaweza kuvaa Hijaab chuoni inatakiwa uondoe uoga na ufuate amri ya Allaah Aliyetukuka. Bila shaka, Yeye Atawatolea njia njema kwa Imani yenu.

 

Ingia katika kiungo kifuatacho:

 

Kuvaa Nywele Za Bandia Kufunika Nywele Turkey Kwa Sababu Ya Kukatazwa Hijaab

 

Tunawaombea tawfiki, istiqaamah na usaidizi kutoka juu, kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share