041-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Alama Tatu Za Kupata Utamu Wa Iymaan

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya   41

Alama Tatu Za Kupata Utamu Wa Iymaan

 

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((ثَلاَثٌ مَنْ كُنَّ فِيهِ وَجَدَ حَلاَوَةَ الإِيمَانِ: أَنْ يَكُونَ اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَحَبَّ إِلَيْهِ مِمَّا سِوَاهُمَا، وَأَنْ يُحِبَّ الْمَرْءَ لاَ يُحِبُّهُ إِلاَّ لِلَّهِ, وَأَنْ يَكْرَهَ أَنْ يَعُودَ فِي الْكُفْرِ كَمَا يَكْرَهُ أَنْ يُقْذَفَ فِي النَّارِ)) متفق عليه

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mambo matatu atakayekuwa nayo, atapata utamu wa imaan: Allaah na Rasuli Wake wawe vipenzi zaidi kwake kuliko wengineo, ampende mtu na wala asimpende isipokuwa kwa ajili ya Allaah, na achukie kurudi katika ukafiri baada ya Allaah kumwokoa kutoka huko kama anavyochukia kuingizwa motoni. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Muumin mwenye Iymaan ya kweli ni mwenye kumpenda Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuliko hata nafsi yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ

Nabiy ana haki zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao [Al-Ahzaab (33: 6)]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ

Na miongoni mwa watu wako wenye kuchukua asiyekuwa Allaah na kuwafanya kuwa ni wanaolingana (na Allaah) wanawapenda kama kumpenda Allaah. Na wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah. [Al-Baqarah (2: 165)]

 

Na Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عَنْ أَنَسٍ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى أَكُونَ أَحَبَّ إِلَيْهِ مِنْ وَلَدِهِ وَوَالِدِهِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ)) أَخْرَجَاهُ

 

Imepokewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mmoja wenu hawi Muumini mpaka anipende mimi kuliko watoto wake na baba yake na watu wote)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 2. Allaah (سبحانه وتعالى) Ameonya kwamba Waumini wasipompenda au wasipofuata amri Zake au wakikengeuka, Atawaondoshelea mbali duniani, kisha Awalete waliobora zaidi yao na wampende Yeye zaidi.

 

[Rejea: Muhammad (47: 38), Al-Maaidah (5: 54)]

 

 

3. Utamu wa Iymaan unapatikana pale Muislamu atakapofuata amri za Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuacha matamanio ya nafsi kando [Rejea: Aal-‘Imraan (3: 31)].

 

 

4. Utamu wa Iymaan unapatikana kutokana na kupenda kutekeleza ‘Ibaadah, Muumini anapozidisha ‘amali za Sunnah kama Swalaah, Swawm, sadaka hufikia daraja ya kupendwa na Allaah (سبحانه وتعالى).

 

[Hadiyth Al-Qudsiy: ((Yeyote yule atakayefanya uadui kwa walii Wangu, Nitatangaza vita dhidi yake. Mja Wangu hanikaribii na kitu chochote Ninachokipenda kama ‘amali Nilizomfaridhishia, na mja Wangu huzidi kunikaribia kwa ‘amali njema za Sunnah ili Nimpende. Ninapompenda, huwa masikio yake yanayosikilizia, macho yake anayoonea, mikono yake anayopigania, miguu yake anayotembelea nayo, lau angeniomba kitu bila shaka Ningempa, lau angeniomba himaya bila shaka Ningelimkinga, na Sisiti juu ya kitu chochote kama Ninavyosita [kuichukua] roho ya mja Wangu Muumin: Anachukia mauti, Nami Nachukia kumdhuru)) [Al-Bukhaariy]

 

5. Inapasa kujenga mapenzi ya ikhlaasw pamoja na waja wema na kuandamana nao katika vikao vyao, kwani mapenzi yao ni kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى), na ndipo Muislamu atakapopata manufaa ya Dini yatakayomfikisha daraja ya Al-Walaa Wal-Baraa (Kupendana kwa ajili ya Dini ya Allaah na kuchukiana au kutengana kwa ajili yake) kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

((أَوْثقُ عُرَى الإِيمان: الموالاَةُ في الله والمعاداةُ في الله، والحب في الله، والبغضُ في اللَّه عز وجل))   

((Shikizo thabiti kabisa la iymaan ni kuwa na urafiki wa karibu kwa ajili ya Allaah na kujitenga kwa ajili ya Allaah, na kupenda kwa ajili ya Allaah, na kuchukia kwa ajili ya Allaah عزّ وجلّ)) [Hadiyth ya Ibn ‘Abaas (رضي الله عنهما) : Atw-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr na ameisahihisha Al-Abaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (2539)]

 

 Na pia:

 

عَنْ أَبِي أُمَامَةَ ، قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ :  ((مَنْ أَحَبَّ فِي اللَّهِ وَأَبْغَضَ فِي اللَّهِ وَأَعْطَى لِلَّهِ وَمَنَعَ لِلَّهِ فَقَدِ اسْتَكْمَلَ الإِيمَانَ))  

Amesimulia Abuu Umaamah  (رضي الله عنه):  “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: “Atakayependa kwa ajili ya Allaah, akachukia kwa ajili ya Allaah, akatoa kwa ajili ya Allaah, na akazuia kwa ajili ya Allaah, basi atakuwa amekamilisha imaan.”  [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy (4681)]

 

6. Kuchukia kufru na ufasiki na watu wake hata kama mtu ana uhusiano wa damu, kwani kafiri na fasiki huenda akamrudisha mtu katika kufru na ufasiki. [Rejea: Al-Mujaadalah (58: 22)].

 

 

 

 

 

 

Share