053-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Anayelia Kwa Kumkhofu Allaah Hatoingia Motoni

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 53

Anayelia Kwa Kumkhofu Allaah Hatoingia Motoni

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لاَ يَلِجُ النَّارَ رَجُلٌ بَكَى مِنْ خَشْيَةِ اللَّهِ حَتَّى يَعُودَ اللَّبَنُ فِي الضَّرْعِ. ولاَ يَجْتَمِعُ غُبَارٌ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَدُخَانُ جَهَنَّمَ)) رواه الترمذي وقال: حديث حسن صحيح

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hatoingia motoni mtu anayelia kwa sababu ya kumkhofu Allaah mpaka maziwa yarudi katika chuchu. Wala haliwezi kujumuika vumbi katika Njia ya Allaah na moshi wa Jahannam)). [At-Tirmdihiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Chozi la kumkhofu Allaah (سبحانه وتعالى) lina fadhila kubwa ya kuepushwa na moto.

 

 

2. Mifano anayopiga Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) ni ya aina ya pekee yenye mazingatio makubwa, sawa na mifano Anayopiga Allaah (سبحانه وتعالى) katika Qur-aan kama Anavyosema:

 

وَلَقَدْ ضَرَبْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٢٧﴾

Na kwa yakini Tumewapigia watu mifano ya kila aina katika hii Qur-aan ili wapate kukumbuka.

 

قُرْآنًا عَرَبِيًّا غَيْرَ ذِي عِوَجٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿٢٨﴾

Qur-aan ya Kiarabu isiyokuwa kombo ili wapate kuwa na taqwa. [Az-Zumar (39: 27-28)]

 

Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَقَدْ صَرَّفْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ فَأَبَىٰ أَكْثَرُ النَّاسِ إِلَّا كُفُورًا ﴿٨٩﴾

Na kwa yakini Tumesarifu namna kwa namna hii Qur-aan kwa watu, kwa kila mfano, lakini watu wengi wamekataa kabisa (haki; hawakukubali) isipokuwa kukufuru tu. [Al-Israa (17: 89)]

 

Na pia Anasema (سبحانه وتعالى):

 

وَلَقَدْ صَرَّفْنَا فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ لِلنَّاسِ مِن كُلِّ مَثَلٍ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ أَكْثَرَ شَيْءٍ جَدَلًا ﴿٥٤﴾

Na kwa yakini Tumesarifu namna kwa namna katika hii Qur-aan kwa watu, kwa kila mifano. Lakini binaadamu amezidi kuliko kila kitu kwa ubishi. [ Al-Kahf: 54]

 

Baadhi ya mifano hiyo Aliyoipiga Allaah (سبحانه وتعالى) katika Qur-aan: Al-Baqarah (2: 261-266) Al-A’raaf (7: 40), (175-177), Yuwnus (10: 24), Ibraahiym (14: 24-27), An-Nahl (16: 75-76), Al-Hajj (22: 73), An-Nuwr (24: 35), (39-40), Az-Zumar (39: 29), Al-Hadiyd (57: 20), Al-‘Ankabuwt (29: 41), Huwd (11: 24), Al-Jumu’ah (62: 5)].

 

 

3. Umuhimu wa Muislamu kufahamu kauli za Allaah (سبحانه وتعالى) katika Qur-aan, na anapoisoma awe anazingatia na kupata mafunzo pamoja na mawaidha, na imzidishie iymaan hata atokwe na machozi khasa pale anapopitia adhabu Zake aingiwe na khofu kwazo.

 

 

4. Fadhila za mtu kutoka ili kupigana katika Njia ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Share