Kusikiliza Qur-aan Huku Unafanya Kazi Zako

 

SWALI

Jee unaweza kusikiliza Qur-an kwa makini huku unafanya kazi zako jikoni kama kupika au kukosha vyombo ingawa akili yako yote iko katika kile kisomo? 

 


 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Hii haina shaka kwani kusikiliza huko kwa makini ndiko kumesisitizwa zaidi. Na linalochukiza kwa baadhi ya Maulamaa ni kuzungumza na huku Qur-aan inasomwa kwa ushahidi wa aya hii:

}}وَإِذَا قُرِىءَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُواْ لَهُ وَأَنصِتُواْ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ{{

{{Na isomwapo Qur-aan isikilizeni na nyamazeni ili mpate kurehemewa}} Al-A'araaf:204

Hata hivyo pamoja na baadhi ya wanachuoni kusema kuwa aya hiyo makusudio ni popote, ila wanachuoni wengi na wafasiri kama Ibn Kathiyr katika tafsiri yake kasema: "Maana yake ni ukiwa ndani ya Swala ya Jamaa'ah, pindi Imamu anaposoma kwa sauti (swala za Alfajiri, Maghrib na 'Ishaa') kama ilivyopokewa na  Imaam Muslim kwenye Sahiyh yake kutoka katika hadithi ya Abu Musa Al-Ash'ariy aliyesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) amesema:  ((Imaam amewekwa ili afuatwe, kwa hivyo akisema: "Allaahu Akbar nanyi mfuateni kwa kusema kama yeye na akianza kusoma, nyinyi nyamazeni))

 

 Vile vile akasema tena Ibn Kathiyr: Ibraahiym Ibn Muslim Al-Haajriy amepokea kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Wao (maswahaba) walikuwa wakizungumza na hali ya kuwa wamo ndani ya swala, kwa hivyo ilipoteremshwa aya hii ... waliamrishwa wawe kimya.

Naye Imam At Twabariy kwenye tafsiri yake anasema kwamba  Ibn Mas'uud amesema: Tulikuwa tukipeana salamu miongoni mwetu tukiwa ndani ya swala, kisha ikaja katika Qur-aan: Na isomwapo Qur-aan isikilizeni na nyamazen.

Kwa hoja hizo inaonyesha aya hiyo haihusiani na Qur-aan isomwayo maredioni na kwenye matelevisheni makompyuta au na watu nje ya swala, hata hivyo kwa kuyapa heshima maneno ya Mwenyeezi Mungu ni bora kunyamaza isomwapo au kuizima kama huwezi kusikiliza. Wa Allaahu A'alam

 

Nasiha Ya Kufuata Adabu Za Tilawa (Kusoma) Qur-aan ;

Kwa hali yeyote ilivyo, ni bora kuipa heshima Qur-aan kwa kutimiza adabu za kusoma  Qur-aan kwani ni maneno ya Allaah سبحانه وتعالى  na kuyatukuza ni wajibu:  Nazo ni:  

1)        Kupiga mswaki

2)   Kuwa na wudhuu

3)   Kujifunika  vizuri (mwanamke)

4)   Kuelekea kibla

5)   Kusoma kwa kutafakari

6)   Kusoma kwa Tajwiid na kufuata sheria zake.

 

 

Share