Nini Hukmu Ya Sajdatut-Tilaawah (Sajda Ya Kisomo)

SWALI:

Assalam alaykum. Kwanza napenda kumshukuru Allah kwa kunipa uzima na kuniwezesha kupata fursa hii ya kuuliza maswali Na kwa uhakika shukurani zote in zake. Na alafu napenda kuwashukuru maustadh wote ambao wamechangia kwa kuendesha hichi kiungo. Swali langu ni je tunatakiwa kusujudu wakati tukisikia Quran? na kama ni kweli mbona jambo hili halifanywi katika jamii? Au ni bora kusujudu wakati mtu akisikia Quran na si lazima?.  Sijawahi kusikia mtu au swahaba kusujudu katika enzi za kipenzi chetu (SWA) baada ya kusikia Quran. Inawezekana maswahaba walikuwa wanasujudu lakini sijasikia mimi tu. kwahiyo inabidi sasa niulize je maswahaba walikuwa wakisujudu?. Na kama ni kweli basi naomba nielezelewe hivyo visa. Lakini nahisi kutokana na hizi aya kuwa waislam wanatakiwa kusujudu wakati wakisomewa Quran lakini sina uhakika. Na kama hisia zangu ni sahihi mbona hili jambo halifanywi? na watu wanalinyamazia?. Kama sikosei aya 21 ya inshaqaaq  inaelekea  inawahusu makafiri ambalo wanaosikia Quran alafu hawasujudu wakajisalimisha kwenye Uislam. lakini na aya ya 15 ya suratul assajdah si inahusu waislam? 

INSHAQAAQ

21. Na wanapo somewa Qur'ani hawasujudu?   

Assajdah

15. Hakika wanao ziamini Aya zetu ni hao tu ambao wakikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi, nao hawajivuni.

  

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ahli zake, Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Sajdatut-tilaawa (sajda ya kusoma Qur-aan) ni kitendo cha Sunnah, na kitendo chochote cha Sunnah humpatia mwenye kutenda thawabu. Ni bora zaidi kujitahidi kutimiza Sunnah ambazo nyepesi kama hizo ili kupata yafuatayo:

1. Thawabu kwa kutenda kitendo cha Sunnah.

2. Kupata fadhila za kufanya sijdah hiyo.

3. Kudhihirisha mapenzi ya Allaah  na Mtume Wake  صلى الله عليه وآله وسلم.

4. Kuzidumisha Sunnah za Mtume.

5. Kujidhalilisha kwa Allaah  kwa kuweka kipaji chako cha uso chini kwenye ardhi na kusema 'Subhaana Rabbiyal-a'laa' (Ametakasikia Mola wangu Aliye juu).     

Aayah hizo ulizozitaja kama ulivyoona kwamba ya kwanza inawahusu makafiri na ya pili inawahusu waumini, lakini hazileti tofauti katika hukmu ya kusujudu kwa ajili ya kusoma Qur-aan inapofika sehemu yenye alama ya kusujudu.

Maswahaba walikuwa wakifuata Sunnah za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hivyo na sisi ni vizuri kufuata nyendo zao

Vile vile tutambue kuwa kila kitu kinamsujudia Allaah سبحانه وتعالى vilivyohai na visivyo hai, sasa vipi sisi binaadamu tusimsujudie?

 ((أَوَ لَمْ يَرَوْاْ إِلَى مَا خَلَقَ اللّهُ مِن شَيْءٍ يَتَفَيَّأُ ظِلاَلُهُ عَنِ الْيَمِينِ وَالْشَّمَآئِلِ سُجَّدًا لِلّهِ وَهُمْ دَاخِرُونَ))  

 (( وَلِلّهِ يَسْجُدُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ مِن دَآبَّةٍ وَالْمَلآئِكَةُ وَهُمْ لاَ يَسْتَكْبِرُونَ))  

 ((يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ))  

48. Je! Hawavioni vitu Alivyoviumba Allah - vivuli vyao vinaelekea kushotoni na kuliani, kumsujudia Allah.

49. Na vyote vilivyomo katika mbingu na katika ardhi, tangu wanyama mpaka Malaika, vinamsujuidia Allah na wala havitakabari.

50. Vinamkhofu Mola wao Mlezi aliye juu yao, na vinafanya vinavyoamrishwa. [An-Nahl-48-50]

Pia katika Suratur-Ra'd,

((وَلِلّهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالآصَالِ))

((Na vilivyomo mbinguni na katika ardhi vinamsujudia Mwenyezi Mungu tu vikitaka visitake. Na pia vivuli vyao asubuhi na jioni)) [Ar-Ra'd]

Na katika Hadiyth ifuatayo,

((عن أبي ذر، رضي الله عنه، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: "أتدري أين تذهب هذه الشمس؟". قلت : الله ورسوله أعلم. قال: "فإنها تذهب فتسجد تحت العرش، ثم تستأمر فيوشك أن يقال لها: ارجعي من حيث جئت " )) مسلم   

((Imetoka kwa Abu Dharr رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: "Unajua jua hili linakwenda wapi?" Nikasema: "Allah na Mjumbe Wake Wanajua ". Akasema : "Linakwenda na kusujudu chini ya 'Arsh, kisha linasubiri amri. Na karibuni litaambiwa: Rudi ulikotoka"))  [Muslim]

((وعن ابن عباس قال: "جاء رجل فقال: يا رسول الله، إني رأيتني الليلة وأنا نائم، كأني أصلي خلف شجرة، فسجدتُ فسجَدَت الشجرة لسجودي، فسمعتُها وهي تقول: اللهم، اكتب لي بها عندك أجرًا، وضع عني بها وزرًا، واجعلها لي عندك ذخرًا، وتقبلها مني كما تقبلتها من عبدك داود. قال ابن عباس: فقرأ   النبي صلى الله عليه وسلم سجدة ثم سَجَد، فسمعته وهو يقولُ مثلَ ما أخبره الرجل عن قول الشجرة.(( رواه الترمذي، وابن ماجه، وابن حبّان في صحيحه

 ((Na Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما amesema: "Mtu moja alikuja na kusema: "Ewe Mjumbe wa Allah, nilijiona katika ndoto jana usiku nikiswali nyuma ya mti. Niliposujudu na mti ukawa unasujudu. Kisha nikausikia unasema: Ewe Mwenyezi Mungu  Niandikie kwako kwa sijda hii malipo, na Nifutie kwayo madhambi, na Ijaalie kwangu mbele yako ni akiba, na Nikubalie kama ulivyomkubalia mja wako Daawuud" Ibn 'Abbaas akasema: "Mjumbe wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم akasoma ayah inayotaja kusujudu kisha akasujudu na nikamsikia akisema maneno hayo hayo aliyosimulia mtu yaliyotajwa na mti")) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ibn Hibbaan katika sahiyh yake]   

 Na ndio maana Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

((أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يَسْجُدُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ وَالنُّجُومُ وَالْجِبَالُ وَالشَّجَرُ وَالدَّوَابُّ وَكَثِيرٌ مِّنَ النَّاسِ وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ الْعَذَاب))

((Je! Huoni kwamba vinamsujudia Allah vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu)) [Al-Hajj: 18]

Hata makafiri walikuwa wakiathirika na Qur-aan walipokuwa wakiisikia hadi kwamba iliposomwa kwao Suratun-Najm Aayah za mwisho ambazo zimetaja kumsujudia Allaah سبحانه وتعالى , walisujudu bila ya kujijua:

((أَفَمِنْ هَذَا الْحَدِيثِ تَعْجَبُونَ))  

  ((وَتَضْحَكُونَ وَلَا تَبْكُونَ))

    ((وَأَنتُمْ سَامِدُونَ))

   ((فَاسْجُدُوا لِلَّهِ وَاعْبُدُوا))

 ((Je! Mnayastaajabia maneno haya?))   

  ((Na mnacheka, wala hamlii?))   

 (( Nanyi mmeghafilika?))  

 ((Basi msujudieni Allah, na mumuabudu)) [An-Najm: 59-62]    

Wakati huo Maswahaba walifanya Hijrah (kuhama)  ya kwanza kwenda Ethiopia, nyuma yao katika mji wa Makkah, ziliteremshwa Aayah hizo, na Makafiri walipoathirika nazo hizo Aayah na kusujudu bila ya kujijua, habari zilienea kote hadi kuwafikia Maswahaba waliokuwa Abisynia (Ethiopia) kuwa Maquraysh wote wameingia Uislam, wakarudi Makkah. Walipokuwa wanakaribia Makkah kwa muda wa msafara wa saa moja tu kutoka Makkah ikadhihirika kwao ukweli ulivyokuwa. Baadhi yao wakarudi Abisynia na wengine wao wakaingia kwa siri mjini Makkah [Ar-Rahiyq Al-Makhtuum]

Kwa maelezo zaidi kuhusu hukmu na fadhila za Sajdatut-tilaawa, ingia katika kiungo kifuatacho:

Bonyeza hapa:

Kusujudu Kwa Ajili Ya Kusoma Aayah

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share