116-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Wamelaaniwa Wanaopiga Chale (Tattoo), Wanaochonga Nyusi Na Meno

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 116  

 

Wamelaaniwa Wanaopiga Chale (Tattoo), Wanaochonga Nyusi Na Meno

 

 

 

 

عَنْ عَبْد الله ابْن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: لَعَنَ اللَّهُ الْوَاشِمَاتِ وَالْمُوتَشِمَاتِ وَالْمُتَنَمِّصَاتِ وَالْمُتَفَلِّجَاتِ لِلْحُسْنِ، الْمُغَيِّرَاتِ خَلْقَ اللَّهِ، فَقَالَتْ لَهُ امْرَأَةٌ فِي ذَلِكَ، فَقَالَ: "وَمَا لِي أَلْعَنُ مَنْ لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَهُوَ فِي كِتَابِ اللَّهِ؟ قَالَ الله تَعَالى: ((وَمَا آتَاكُمْ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا)) متفق عليه

‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) alisema: “Allaah Anawalaani wanaopiga chale na wanaotaka kupigwa chale, na wanaochonga nyusi na wanaochonga meno wakaacha mwanya kwa sababu ya uzuri, wanaobadilisha maumbile Aliyoyaumba Allaah.” Mwanamke mmoja akamlaumu juu ya jambo hilo (la kulaani). Akasema (‘Abdullaah): “Kwa nini nisimlaani aliyelaaniwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na ilhali iko ndani ya Kitabu cha Allaah? Allaah Aliyetukuka Anasema: ((Na lolote analokupeni Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr (59: 7)])). [Al-Bukhaariy na Muslim] Na katika riwaayah nyingine imetajwa: “Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amemlaani mwenye kuunga na mwenye kuungwa (nywele)…” [Al-Bukhaariy]

 

Kupiga chale ni kuikwangua ngozi itoke damu, kisha apake wanja au kitu kingine kisha inakuwa rangi ya kijani (tattoo).

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Haramisho la kujibadilisha chochote katika umbo la mtu kwa ajili ya kujipamba ikiwa ni kuzidisha au kupunguza, isipokuwa ikiwa kuna dharura ya matibabu.

 

 

2. Haramisho kwa wanawake kunyoa nyusi na kwamba wanaotoa na wanaotolewa watapata laana ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

3. Haramisho la kuunga nywele na kuvaa mabaruka (wigi), kwani ni kubadilisha maumbile ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

 4. Kupiga chale, kuchonga nyusi na meno, yote hayo ni miongoni mwa madhambi makubwa, kwa vile yametajiwa laana ya Allaah (سبحانه وتعالى) ambayo ni kuwekwa mbali na Rahma Yake.

 

 

5. Makatazo hayo ni katika mila za makafiri ambazo haipasi Muislamu kuwaiga, kwani wao wanadhamiria mno Waislamu kuwaiga mila zao na wanapenda mno kuona Muislamu ameacha Dini yake. Allaah (سبحانه وتعالى) Anatahadharisha:

 

 وَلَن تَرْضَىٰ عَنكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَىٰ حَتَّىٰ تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ ۗ

Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswaara mpaka ufuate mila zao. [Al-Baqarah (2: 120)]

 

 

6. Kujibadilisha umbo ni hila za shaytwaan anayemtia mtu matamanio ya nafsi. [An-Nisaa (4: 117-121)].

 

Rejea Hadiyth namba (113).

 

 

Share