Utaipata Wapi Tena Fursa Hii?

Utaipata Wapi Tena Fursa Hii?

Naaswir Haamid

 

Ramadhaan ndio inaondosha nanga na hakuna ajuaye nani ataipata tena fursa hii ‘adhiym. Hili ni kundi la mwisho lenye Laylatul Qadr ndani yake na hivyo tujiweke vizuri kushinda bila ya kujali muda. Hatuna nafasi ya kusubiri ila ni hii.

 

Huu ndio mwezi wa kuoneshana mapenzi ili kutaraji Rahma mbele ya Allaah. Hili linadhihirishwa kwa kumtumikia Mola Mlezi wa Mbingu na Ardhi. Tusiwe ni wenye kutenda mema mwezi huu tukayaacha miezi iliyobaki nyuma ya migongo yetu. Hio itakuwa ni sawa na shirk, kwani tulimuabudu Ramadhaan na kumuacha Mola wa Haki.

 

Ramadhaan ni mwezi wa kusoma, kukutana katika kheir, kuhurumiana, kuacha fitna na mengineyo. Haya yote yawe mara tatu zaidi kwenye kipindi hichi cha siku za mwisho za Ramadhaan.

 

Basi, huu sio wakati wa kulegeza kamba kwa kuweka matumaini ya kukutana na Bwana ‘Iyd kwenye pombe, zinaa, kamari na mengineyo maovu. Ni lazima kumuheshimu Mola Mlezi ili tupate kujiheshimu mbele ya wanaotuzunguka kwa matendo, matamshi na kivazi. Kujiheshimu huku kuwe kwa siri na kwa dhahiri.

 

Huu ni mwezi wa ibada na katu sio mwezi wa mchezo. Huu ni mwezi wa kujifunza ucha Mungu ili tuwe Wacha Mungu kipindi chote cha miezi 11 iliyobaki. Sio uungwana kuwa wacha Mungu mwezi wa Ramadhaan na kugeuka mnyama miezi kumi na moja.

 

Siku zilizobaki sio za kwenda kufanya manunuzi ya mambo yasiyo maana, hizi ni siku za kukaa itikafu msikitini kwa kutubu na kutaraji malipo mema mbele ya Mola Mlezi. Ustahamilie usingizi wako kwenye mwezi huu mmoja na uyaheshimu masiku yaliyobaki kwa lengo la kupata Jannah. Tukumbuke kwamba moja miongoni mwa siku hizi kuna siku iliyo bora, nayo ni Laylatul Qadr yenye ubora wa miezi alfu moja. Na mwenye kunyimwa kheir ya siku hii, amenyimwa kheir zote.

 

Imepokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwamba amesema: ((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu.  Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri])) [Imepokewa na Imaam Ahmad]

 

Kwa wale waliowaasi wazee wao, huu ndio wakati wa kurudi kabla ya kuzikosa radhi zao zitakazopelekea kukosa radhi za Muumba. Hivyo, turudi kwa wazee tuliowaasi, tuombeane radhi na dua zenye kheir.

 

Ama kwa wanandoa waliofarikiana kwa sababu zisizo na msingi, hizi ni siku za kuombeana radhi na kurudiana kwa wema. Kwani haitokuwa na maana kufarikiana ilhali killa mmoja anaishi na kimada.

 

Kumi hili sio la kujilazimisha kuacha kula na kunywa. Hizi ndio siku za kukaza kamba, kujipinda barabara kwa kumfurahisha Mola Mlezi. Malipo ya Pepo sio mepesi. Yanahitaji kazi, na bila ya shaka kazi yake ipo hapa Duniani, na inaanzia kwa kumtumika Mola Mtukufu na sio Ramadhaan pekee.

Share