Zingatio: Milango Ipo Wazi

 

Naaswir Haamid

 

Ewe Muislamu, tambua wakati huu ambao milango ya toba ipo wazi, tofautisha na ule wakati ambao milango ya toba imefungwa, nao ni wakati ambao roho inatolewa. Jitahidi uulipize ule wakati ambao uliupoteza katika kutenda maasi. Jiweke karibu kwa Mola Mlezi hapo ndipo utakaa mbali na Ibilisi. Kasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

 

{{Na tubieni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waislamu ili mpate kufaulu.}} [An-Nuur: 31]

 

Kutubia kwa Allaah ni katika sifa njema za Waumini. Kwani rahma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ilivyokuwa kubwa juu ya waja Wake Anawakubalia toba zao alimuradi bado hawajawa katika Sakaratul Mawt. Hapana toba kwa wenye kuchelewesha kutubia kwa makusudi hadi wakafikia kwenye mauti. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

{{Toba inayopokelewa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa upesi. Hao ndio Mwenyezi Mungu Huipokea toba yao…}} [An-Nisaa: 17]

 

Anaendelea kusema:

 

{{Hawana toba wale ambao hufanya maovu mpaka mauti yamemhudhuria mmoja wao, (hapo) akasema: “Hakika mimi sasa natubu.” Wala hawana (toba) wale ambao wanakufa katika hali ya ukafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo.”}} [An-Nisaa: 18]

 

Basi nakunasihi ndugu yangu Muislamu, turejee pamoja kwa Mola wetu kabla ya kufumba jicho. Tufanye haraka kwani hatujui mauti yatatukuta tukiwa wazima au wagonjwa. Tutambue kwamba hakuna mja asiyemkosea Mola wake Mlezi wa Mbingu na Ardhi, lakini mbora wetu ni yule mwenye kurudi kwa haraka akiwa na majuto. Basi hapo Mwenyezi Mungu Huwa na furaha kubwa juu ya mja kama huyu anayetubia toba ya kweli kweli. Tuangalie kwenye Hadiyth ifuatayo namna Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alivyo na huruma kupita mapenzi ya mama kwa mwana:

 

Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kutolewa na Imaam al-Bukhaariy na Muslim:

 

“Furaha ya Mwenyezi Mungu kwa mja Wake Muumini ni kubwa pale atakapotubu, kuliko furaha ya mtu alioko katika jangwa, naye ana kipando chake, na mnyama huyo kabeba chakula na maji ya kunywa. Mtu huyo akafika pahala akalala, alipoamka hakumkuta yule mnyama wake, akaanza kumtafuta mpaka akachoka, akashikwa na kiu. Akasema: Bora nirudi pahala pangu nilipokuwa na nilale mpaka nife. Akalala (akingojea mauti), baada ya muda akazindukana na mnyama wake yuko chini yake pamoja na chakula chake na maji yake…

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anamalizia kwa kueleza kwamba furaha ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) huwa kubwa zaidi kuliko huyo aliyepotelewa na mnyama:

 

…Basi Mwenyezi Mungu Huwa na furaha zaidi kwa mja Wake Muumini atakapotubu kuliko huyu mtu aliyepotelewa na mnyama wake kisha akamuona.”

 

Share