Nimeshauriwa Kuzuia Uzazi Na Daktari


 

SWALI:

Mimi mama wa watoto watatu, miaka 7, miaka 4 na miezi 8, na mwaka na miezi 10. Nikiwa na mimba afya yangu hudhofu, ni kawa nimwenye kulazwa hospitali mara kadhaa hata nizaapo.

Nimetumia contraceptive method nyingi, Norplant, sindano, Coils na pills, lakini Allaah mkubwa, I still get pregnant. Sasa nina mimba tena miezi 6, na daktari amenishauri kwa sababu ya afya yangu, sio kifedha (nashkuru Subhana, hatuna shida kifedha) nikishazaa huyu wanne nifanye Tubal Ligation. Sijui nitakua nafanya the right thing or not naogopa kumuasi Allaah, na Daktari nae ananiambia sifai kubeba mimba nyengine, hata hii niliyonao sasa alikuwa ataka kunitoa, lakini mimi na mume wangu tulikataa kabisa.

Nijibu please I am desparate kujua kwa sababu hata usiku silali nina wasiwasi.

 

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa dada yetu kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala haya ya ubebaji mimba. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akusahilishie uzae kwa salama u salimini. Kwa hakika ni uamuzi mzito muliouchukua wewe na mume wako katika hali kama hiyo ambapo wengi wangeweza kuona njia ya pekee labda ni kukitoa kiumbe ambacho tayari kimekamilika.

Kwa uamuzi huu wa Imani Insha Allaah, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hatakuacha bali Atakusaidia na utazaa salama kwa idhini yake. Suala hili ni nyeti sana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huumba Atakacho na hakuna wakumuuliza lolote wala chochote.

Dawa zote za kuzuia uzazi hazina uhakika wa mia kwa mia (100%), kwani ipo asili mia kadhaa ya kutofaulu na kadhiya yako ni ushahidi wa hilo.

Wakati wa Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam), Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) walikuwa wakifanya ‘Azl (Coitus interruptus – kumwaga nje) na Qur-aan ilikuwa inashuka na Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asiwakataze. Hii ilikuwa ni njia ya kuafikiana baina ya mume na mke ili kuweza kupanga watoto na kumpatia muda wa mtoto kunyonya na kukua, lakini Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia kile akitakacho Mola kiingie kitaingia na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wengine.

Ieleweke kuwa dawa nyingi hizi za kupanga uzazi zina madhara makubwa sana kwa mwanamke mwenye kuzitumia. Hivyo tutahadhari sana katika hilo.

Jambo ambalo tunaweza kumshauri dada yetu na mumewe kuwa waende kwa daktari Muislamu mwanamke, mcha Mungu ambaye ni mtaalamu wa mambo na magonjwa ya kike wapate ushauri kutoka kwake pia. Ikiwa hawapatikani wataalamu hao ambao ni Waislamu wanawake au wanaume, mnatakiwa kwenda kwa madaktari ambao ni waaminifu na wataalamu katika nyanja hiyo. Inatakiwa muende kwa wataalamu hao kiasi cha watatu hadi watano na kusikiliza ushauri wao, kwani ushauri wa mmoja unaweza kuwa ni wa makosa kwa njia moja au nyengine. Ikiwa ushauri wa wote hao ni sawa, ya kwamba ufanye Tubal Ligation au ufunge kizazi kabisa basi unaweza kufanya hivyo na hutakuwa na makosa katika sheria ya Kiislamu.

Usivunjike moyo dada yetu, kwani huu ni mtihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na mwenye kusubiri katika mtihani au mitihani basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Humjazi na kumlipa mema. Kuwa na subira na uzidi kumuomba Mola wako kwani watu huwa na maradhi zaidi ya ya kwako kisha wakapona kama kwamba hawakuwa na magonjwa.

Tunazidi kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akusahilishie uzae kwa salama na akuondolee taabu hiyo ili muweze kuzaa watoto wema na wazuri, Aamiyn. 

Na Allaah Anajua zaidi

Share