Kuwatambulisha Watoto Bila DNA

 

 

 

SWALI:

Subject: Sallam aleikum sheikhe. swali yangu ni katika dina kama mama wawili wamechanganisha watoto wachanga na kila mama anadai amezaa mtoto mvulana. Je dini inaweza kuwatowanishaje ukiondoa kuchukuliwa DNA. Naomba unijibu kutokana kwa Quran na sunna.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako kuhusu mas-ala hayo japokuwa hukubainisha utata huo ulitokeaje? Ikiwa watoto hao wamezaliwa na kina mama wakawaona watoto wao shida hiyo haitakuwepo lakini ikiwa wamezaliwa na hao wamama wakawa hawajawaona ndio tatizo hilo litakuwepo.

Mama wa waumini ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahuanha) anatufahamisha ya kwamba kabla ya kutumilizwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakaazi wa Makkah walikuwa na ndoa aina NNE. Moja wapo kati ya hizo ni wanaume wengi kumuingilia mwanamke mmoja na kila mmoja katika wanaume wanafahamu hilo. Mwanamke huyo anapojifungua mtoto wanaume wote waliolala naye wanaitwa na hakuna hata mmoja anayekataa kuja. Wanapojumuika wote anaitwa mtu ambaye ni mjuzi katika kufananisha mtoto kwa mzazi. Anayechaguliwa kuwa baba wa mtoto huyo, na wote hukubali uamuzi huo. (Al-Bukhaariy).

Huu ni ujuzi ambao upo mpaka wakati wetu wa leo. Wapo watu wakimuona tu mtoto atakuambia kuwa mtoto anafana na baba au mama. Wakati mwengine anakufahamisha mdomo huu ni kama wa babu yake, pua ni kama ya mama, macho yake ni kama shangazi yake na mfano wake.

Ikiwa tatizo hilo lipo basi mjuzi wa aina hiyo anaweza kutatua tatizo hilo mara moja bila ya kuendea njia za kisasa za kutumia DNA (deoxyribonucleic acid) [DNA ni kitu (molekyuli) cha kiini ya seli ambacho kinakuwa na maelezo ya kijenetiki (vinasaba), inatambua muundo, utendaji na tabia ya seli.]

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share