01-Maamkizi Ya Kiislam: Umuhimu Na Baadhi Ya Fadhila Zake

 

Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake

 

01-Umuhimu Na Baadhi Ya Fadhila Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Kutoa salaam ni funzo muhimu tulilofundishwa na kuamrishwa katika Dini yetu, lakini tunaona kwamba limechukuliwa kuwa ni jambo jepesi lisilotiliwa hima na ilhali lina fadhila nyingi na kubwa sana, mojawapo ni kumuingiza mtu Peponi kwa dalili Hadiyth ifuatayo:

 

عن أبـي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((لا تَدْخُـلُوا  الـجَنَّةَ حتـى  تُؤمِنُوا،  ولا تُؤمِنُوا  حتـى تَـحابُّوا  أوَلا أدُلُّكُمْ علـى شَيءٍ  إذا فَعَلْتُـمُوهُ تَـحَابَبْتُـمْ؟  افْشُوا السّلامَ  بَـيْنَكُمْ)). صحيح مسلـم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hamtoingia Jannah hadi muamini, na wala hamuwezi kuamini hadi mpendane. Je, nikujulisheni jambo ambalo mtakapolifanya mtapendana? Toleaneni Salaam baina yenu)) [Muslim]

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah, mafunzo ya maamkizi ya salaam yalikuwa ni katika mafunzo ya mwanzo kabisa kuwapa Maswahaba alipoyatoa katika khutba zake za mwanzo huko aliposema:   

 

((ايها الناس ،أفشوا السلام، وأطعموا الطعام، وصلّوا  بالليل والناس  نيام  تدخلوا  الجنة  بسلام)) رواه الترمذي، حديث صحيح

((Enyi watu, enezi (amkianeni kwa) salaam, na lisheni chakula, na Swalini watu wakiwa wamelal (Tahajjud), mtaingia Jannah kwa amani)) [At-Tirmidhiy – Hadiyth Swahiyh]

 

Waislamu wanapokutana au kuwasiliana kwa njia yoyote inawapasa kusalimiana kwa maamkizi ya Kiislamu kama tulivyoamrishwa; yaani kusema:  "Assalaamu 'Alaykum." Haya ndio maamkizi ya Kiislamu yanayopaswa kuanziwa katika kuamkiana. Lakini aghlabu wa wasiojua umuhimu wake huanzia kwa kauli kama: "Hujambo? "Habari gani?" "Hali?" "Vipi mzima?" "Habari za asubuhi" au 'Swabaahal-khayr" "Ahlan" "Marhaba".  

 

Maamkizi haya ya Kislamu hayapasi kufupishwa hata katika maandishi, mfano ambayo yanafupishwa katika mawasiliano ya kimaandishi ni: A.A, au A.A.W, au A.A.W.W.B.

 

Hakika kufupisha maamkizi ya Kiislamu ni kukosa fadhila zake kubwa. Kuandikia kikamilifu haimchukui mtu hata dakika moja.  Inavyopaswa ni kuandika: 'Assalaamu 'Alaykum' au Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh'.

 

Tunatumai kwamba baada ya kuzijua fadhila zake katika Makala hizi Waislamu tutaweza kuthamini maamkizi ya Kiislamu kama yalivyokuja katika Shariy’ah.

 

Zifuatazo ni Aayah na Hadiyth zenye amri na mafunzo muhimu ya maamkizi ya Kiislamu:

 

Tunapoingia majumbani mwa wenzetu tunatakiwa tuanze kusalimia kwa maamkizi ya Kiislamu:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَىٰ أَهْلِهَا ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٢٧﴾

Enyi walioamini! Msiingie nyumba zisizokuwa nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee salamu wenyewe. Hivyo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka. [An-Nuur: 27]

 

Tuna mifano kutoka kwa Malaika pindi Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alipoingia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiweko Mama wa Waumini: kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

 عن عائشة رضي الله عنه قالت‏:‏ قال لي رسول الله صلى الله عليه وسلم‏:‏ ((هذا  جبريل  يقرأ عليك  السلام))  قالت‏:‏  قلت‏:‏ ‏"‏وعليه السلام ورحمة الله وبركاته‏"‏‏ ‏متفق عليه

Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Huyu Jibriyl anakutolea salaam)) Nikamjibu: "Wa ‘Alayhis-Salaam wa RahmatuLLaahi Wa Barakaatuh" [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Pia kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuhusu Malaika walipopita nyumbani kwa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) kuelekea mji wa Nabiy Luutw (‘Alayhis-Salaam) kuuangamiza kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ﴿٢٤﴾

Je, imekufikia hadithi ya wageni wahishimiwao wa Ibraahiym?

 

إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا ۖ قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ﴿٢٥﴾

Walipoingia kwake wakasema: “Salaam! Akasema: “Salaam watu wasiotambulikana.” [Adh-Dhaariyaat: 24-25]

 

 

   

Share