02-Maamkizi Ya Kiislam: Kuwajibika Kwake

 

Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake

 

02-Kuwajibika Kwake

 

Alhidaaya.com

 

 

Maamkizi ya Kiislamu yamewajibika kwetu kutokana na amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa dalili zifuatazo:

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

  

لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَلَا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَن تَأْكُلُوا مِن بُيُوتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ آبَائِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أُمَّهَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ إِخْوَانِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخَوَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَعْمَامِكُمْ أَوْ بُيُوتِ عَمَّاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخْوَالِكُمْ أَوْ بُيُوتِ خَالَاتِكُمْ أَوْ مَا مَلَكْتُم مَّفَاتِحَهُ أَوْ صَدِيقِكُمْ ۚ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَأْكُلُوا جَمِيعًا أَوْ أَشْتَاتًا ۚ فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٦١﴾

Si vibaya kwa kipofu, na wala si vibaya kwa kilema, na wala si vibaya kwa mgonjwa, na wala nyinyi wenyewe kama mtakula majumbani mwenu, au majumbani mwa baba zenu, au majumbani mwa mama zenu, au majumbani mwa kaka zenu, au majumbani mwa dada zenu, au majumbani mwa ‘ammi zenu, au majumbani mwa shangazi zenu, au majumbani za wajomba wenu, au majumbani mwa makhalati zenu au za mliowashikia funguo zao, au rafiki yenu. Hakuna ubaya kama mkila pamoja au mbali mbali. Mtakapoingia majumbani toleaneni salaam; maamkizi kutoka kwa Allaah, yenye Baraka, mazuri. Hivyo ndivyo Anavyokubainishieni Allaah Aayaat ili mpate kutia akilini. [An-Nuwr: 61]

 

Aayah tukufu hiyo inaashiria jinsi maamkizi ya Kiislamu yalivyokuwa na umuhimu mkubwa hadi kwamba tunapoingia majumbani mwa wenzetu au hata majumbani mwetu na ikawa hakuna mtu tunapaswa kusalimia kwani kufanya hivyo ni kujitakia kheri na Baraka kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Pia Hadiyth zifuatazo za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن أنس رضي الله عنه قال‏:‏ قال لي رسول الله صلى الله عليه وسلم ‏:‏ ((‏يا بُني، إذا دخلت على أهلك، فسلم، يكن بركة عليك، وعلى أهل بيتك‏))"‏ ‏(‏‏(‏رواه الترمذي وقال‏:‏ حديث حسن صحيح‏)‏‏)‏‏.‏  

 Kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ee mwanangu! Unapoingia nyumbani mwako toa salaam itakuwa Baraka kwako na kwa watu wa nyumbani mwako)). [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth hii ni Hasan Swahiyh]

 

Jambo la mwanzo alilofunzwa Nabiy Aadam (‘Alayhis Salaam) baada ya kuumbwa lilikuwa ni maamkizi ya Kiislamu kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

 عن أبـي هريرة رضي الله عنه عن النبـي صلى الله عليه وسلم قال: «خَـلَقَ اللَّهُ عَزَّ وجَلَّ آدَمَ علـى صُورَتِهِ طُولهُ سِتُّونَ ذِراعاً، فَلَـمَّا خَـلَقَهُ قال: اذْهَبْ فسَلِّـمْ علـى أولئِكَ: نَفَرٍ مِنَ الـمَلائِكَةِ جُلُوسٍ فـاسْتَـمعْ ما يُحَيُّونَكَ فإنَّها تَـحِيَّتُكَ وتـحِيَّةُ ذُرِّيَّتِكَ، فقالالسَّلامُ عَلَـيْكُمْ، فقالوا: السَّلامُ عَلَـيْكَ وَرَحْمَةُ اللَّهِ فَزَادُوهُ: وَرَحمَةُ اللَّهِ )) البخاري و مسلم

 

Kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Amemuumba Aadam ('Alayhis Salaam) katika umbo Lake, akiwa urefu wa dhiraa sitini. Alipomaliza kumuumba, alimwambia: Nenda ukawaamkie kundi la Malaika waliokaa na Usikilize watakavyokuamkia, kwani hayo ndio yatakavyokuwa maamkizi yako na ya kizazi chako. Akasema (Aadam): "Assalaamu 'Alaykum". Wakajibu: "Assalamu 'Alayka wa RahmatuLLaah." Wakazidisha: 'Wa RahmatuLLaah')) [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Pia maamkizi ya Kiislamu ni haki ya Muislamu kwa Muislamu mwenzake kurudisha maamkizi hayo. Kwa maana mtu anapoanza kukuamkia kwa maamkizi ya Kiislamu inakupasa nawe urudishe kumuamkia la sivyo itakuwa hukumtizimia haki yake:

 

 عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صبى الله عليه وسلم قال: ((حق المسلم على المسلم خمس رد السلام وعيادة المريض واتباع الجنائز وإجابة الدعوة وتشميت العاطس))  متفق عليه

 Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Haki ya Muislamu kwa Muislamu ni mambo matano; kurudisha salaam, kumtembelea mgonjwa, kusindikiza jeneza, kuitikia mwaliko, na kumuombea Rahma mwenye kupiga chafya)). [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Juu ya hivyo mwenye kuamkiwa inampasa arudishe maakimizi ambayo ni bora zaidi kuliko ya yule aliyemuamkia. Tutazame namna gani tunatakiwa kurudisha maamkizi ya Kiislam:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَإِذَا حُيِّيتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا ﴿٨٦﴾

Na mtapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo au yarudisheni hayo hayo. Hakika Allaah daima ni Mwenye kuhesabu kila kitu. [An-Nisaa: 86]

 

 

 

Ina maana kwamba ikiwa mtu atakuamkia kwa kusema: "Assalaamu 'Alaykum" basi ni vizuri wewe kuitikia: "Wa 'Alaykumus Salaam wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh". Hata ukijibu "Wa 'Alaykumus Salaam" pia inatosha ila ya mwanzo ni bora zaidi kutokana na mafunzo ya Allaah tuliyoyapata katika Aayah hiyo.

 

Na pia kila unapozidisha kuongeza maamkizi ya salaam, basi thawabu zinazidi zinazidi kwa dalili:

 

عن عمران بن حصين رضي الله عنهما قال :جاء رجل الى النبي صلى الله عليه وسلم فقال: "السلام عليكم" فرد عليه السلام ثمجلس فقال النبي صلى الله عليه وسلم: ((عشر)) ثم جاء رجل اخر فقال: "السلام عليكم ورحمة الله"  فرد عليه فجلس فقال: ((عشرون)) ثم جاء رجل اخر فقال: "السلام عليكم ورحمة الله وبركاته" فرد عليه فقال ((ثلاثون))  رواه ابو داود والترمذي و قال حديث حسن

'Imraan bin Al-Huswayn (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesimulia: "Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamkia: "Assalaamu 'Alaykum.” Akamrudishia (Salaam) kisha yule mtu akaketi. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Kumi)) [Kwa maana amepata thawabu kumi]. Kisha akaja mtu mwengine, akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaah." Naye akamrudishia, kisha yule mtu akaketi, Nabiy akasema: ((Ishirini)). Kisha akaja mtu mwingine akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh." Naye akamrudishia kisha akasema ((Thelathini)) [Imesimuliwa na Abu Daawuwd na At-Trimidhiy na akasema Hadiyth Hasan].

 

 

Share