04-Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake: Nyakati Bora Za Kuomba Tawbah

Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake

 

04-Nyakati Bora Za Kuomba Tawbah

 

 

 

1-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Wakati Wowote Ule:

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hupokea tawbah zetu wakati wowote kama alivyotuelezea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي مُوسَى عَبْدِ الله بنِ قَبَسٍ الأَشْعَرِيِّ  (رضي الله عنه) عن النَّبيّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قال: ((إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا)) رواه مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Muwsaa ‘Abdillaah bin Qays Al-Ash‘ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu)   kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallamamesema: ((Hakika Allaah Anakunjua Mkono Wake usiku ili Apokee tawbah ya mkoseaji mchana. Na Anakunjua Mkono Wake mchana ili Apokee tawbah ya mkoseaji usiku mpaka jua lichomoze Magharibi [mahali linapokuchwa])) [Muslim]

 

 

2-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kabla Ya Alfajiri:

 

Lakini wakati mzuri kabisa wa kuomba maghfirah na tawbah ni nyakati za kabla ya Alfajiri kama Anavyowasifu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) waja wema wafanyao hivo; Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ﴿١٧﴾

Wenye kusubiri na wasemao kweli, na watiifu, na watoaji mali katika njia ya Allaah na waombao maghfirah kabla ya Alfajiri. [Aal-‘Imraan: 17]

 

 

Vilevile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewasifu waje Wake Waumini wanao omba maghfirah kabla ya Alfajiri. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿١٨﴾

Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah. [Adh-Dhaariyaat: 18]

 

3- Kuomba Maghfirah Na Tawbah Usiku Wa Manane:

 

Kuamka usiku na kufanya 'Ibaadah kama hii ya kuomba maghfirah na tawbah kunapatikana ndani yake fadhila adhimu kabisa, mojawapo ni mja kukaribiana na Rabb wake. Hadiyth ifuatayo imetuthibitikia kuteremka Kwake usiku kuja katika mbingu ya kwanza kupokea tawbah:

 

  عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم    

 

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani Ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Hii ni neema kubwa kwetu kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) Anateremka katika mbingu ya kwanza kutupokelea haja zetu na kutughufiria. Basi nani ambaye ataacha neema hii impitie ilhali binaadamu anaingia madhambini kila siku?  

 

 

Faida: Swala hili la 'Aqiydah ni muhimu kulijua kuhusu kuteremka Kwake Allaah ('Azza wa Jalla) kwamba: Kuteremka Kwake kunalingana na Utukufu Wake na sisi hatujui ni vipi uteremkaji huo unakuwa, wala hatupaswi kuhoji.

 

 

Share