013 - Ar-Ra'd

 

 

 الرَّعْد

 

013-Ar-Ra’d

 

013-Ar-Ra'd: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

 

المر ۚ تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ ۗ وَالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ﴿١﴾

1. Alif Laam Miym Raa.[1] Hizi ni Aayaat za Kitabu. Na yale yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka kwa Rabb wako ni haki, lakini watu wengi hawaamini.

 

 

 

 

اللَّـهُ الَّذِي رَفَعَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُم بِلِقَاءِ رَبِّكُمْ تُوقِنُونَ ﴿٢﴾

2. Allaah Ambaye Ameinua mbingu bila ya nguzo mnaziona, kisha Akawa juu[2] ya ‘Arsh. Na Akavitiisha jua na mwezi, vyote vinakwenda mzunguko hadi muda maalumu uliokadiriwa. Anadabiri mambo, Anazifasili waziwazi Aayaat (Ishara, Dalili) ili mpate kuwa na yakini ya kukutana na Rabb wenu.

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي مَدَّ الْأَرْضَ وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنْهَارًا ۖ وَمِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ جَعَلَ فِيهَا زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ ۖ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٣﴾

3. Na Yeye Ndiye Aliyetandaza ardhi na Akajaalia humo milima thabiti na mito, na kila aina ya mazao Amejaalia humo jozi mbilimbili (za kiume na kike). Anafunika usiku juu ya mchana. Hakika katika hayo kuna Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa watu wanaotafakari.

 

 

 

وَفِي الْأَرْضِ قِطَعٌ مُّتَجَاوِرَاتٌ وَجَنَّاتٌ مِّنْ أَعْنَابٍ وَزَرْعٌ وَنَخِيلٌ صِنْوَانٌ وَغَيْرُ صِنْوَانٍ يُسْقَىٰ بِمَاءٍ وَاحِدٍ وَنُفَضِّلُ بَعْضَهَا عَلَىٰ بَعْضٍ فِي الْأُكُلِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٤﴾

4. Na katika ardhi kuna vipande vyake tofauti vinavyopakana, na mabustani ya mizabibu na mazao (mengineyo), na mitende inayochipuka katika shina moja na isiyochipuka katika shina moja, vinanyweshezwa kwa maji ya aina moja, na Tunavifanya baadhi kuwa bora zaidi kuliko vingine katika ladha na lishe. Hakika katika hayo kuna Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa watu wanaotia akilini.[3]

 

 

 

وَإِن تَعْجَبْ فَعَجَبٌ قَوْلُهُمْ أَإِذَا كُنَّا تُرَابًا أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ ۖ وَأُولَـٰئِكَ الْأَغْلَالُ فِي أَعْنَاقِهِمْ ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٥﴾

5. Na ukistaajabu (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi cha ajabu ni kauli yao: Je, tukiwa mchanga, hivi kweli sisi tutakuja kuwa katika umbo jipya?[4] Hao ndio wale waliomkufuru Rabb wao. Hao watafungwa minyororo katika shingo zao.[5] Na hao ndio watu wa motoni, wao humo watadumu.

 

 

 

وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ وَقَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِمُ الْمَثُلَاتُ ۗ وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ لِّلنَّاسِ عَلَىٰ ظُلْمِهِمْ ۖ وَإِنَّ رَبَّكَ لَشَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٦﴾

6. Na wanakuhimiza kwa maovu kabla ya mazuri, na hali imekwishapita kabla yao mifano ya adhabu. Na hakika Rabb wako Ni Mwenye Maghfirah kwa watu juu ya dhulma zao, na hakika Rabb wako Ni Mkali wa Kuakibu.

 

 

 

وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ ۗ إِنَّمَا أَنتَ مُنذِرٌ ۖ وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ ﴿٧﴾

7. Na wanasema wale waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Aayah (Muujiza) kutoka kwa Rabb wake? Hakika wewe ni mwonyaji tu na kila kaumu ina mwenye kuongoza.

 

 

 

اللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَحْمِلُ كُلُّ أُنثَىٰ وَمَا تَغِيضُ الْأَرْحَامُ وَمَا تَزْدَادُ ۖ وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾

8. Allaah Anajua mimba abebayo kila mwanamke na yanayokipunguza matumbo ya uzazi na yanayokizidisha (muda au umbile). Na kila kitu Kwake ni kwa kipimo.

 

 

 

 

عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ ﴿٩﴾

9. Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, Mkubwa kabisa Mwenye Uluwa.

 

 

 

سَوَاءٌ مِّنكُم مَّنْ أَسَرَّ الْقَوْلَ وَمَن جَهَرَ بِهِ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍ بِاللَّيْلِ وَسَارِبٌ بِالنَّهَارِ ﴿١٠﴾

10. Ni sawa (Kwake) mmoja wenu akisema maneno yake kwa siri au kwa sauti, na anayenyemelea usiku na anayetembea mchana kwa uhuru.

 

 

 

لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ ۚ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ ﴿١١﴾

11. Ana Malaika wanaofuatana kwa zamu mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa Amri ya Allaah.[6] Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. Na Allaah Akiwakusudia watu adhabu, basi hakuna wa kuirudisha. Nao hawana mlinzi yeyote ghairi Yake.

 

 

 

هُوَ الَّذِي يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنشِئُ السَّحَابَ الثِّقَالَ ﴿١٢﴾

12.  Yeye Ndiye Anayekuonyesheni umeme mkaingiwa khofu (ya radi na mvua kubwa za kuharibu) na mkapata matumaini (ya manufaa na kheri zake), na Anaanzisha mawingu mazito.

 

 

 

وَيُسَبِّحُ الرَّعْدُ بِحَمْدِهِ وَالْمَلَائِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِ وَيُرْسِلُ الصَّوَاعِقَ فَيُصِيبُ بِهَا مَن يَشَاءُ وَهُمْ يُجَادِلُونَ فِي اللَّـهِ وَهُوَ شَدِيدُ الْمِحَالِ ﴿١٣﴾

13. Na radi inamsabihi (Allaah) na kumhimidi na Malaika pia (wanamsabihi) kwa sababu ya kumkhofu[7], na Anatuma radi na umeme angamizi, Akamsibu kwayo Amtakaye, nao huku (makafiri) wakiwa wanabishana kuhusu Allaah, Naye ni Ni Mkali na Mwenye nguvu za kuhujumu.

 

 

 

لَهُ دَعْوَةُ الْحَقِّ ۖ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُم بِشَيْءٍ إِلَّا كَبَاسِطِ كَفَّيْهِ إِلَى الْمَاءِ لِيَبْلُغَ فَاهُ وَمَا هُوَ بِبَالِغِهِ ۚ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ ﴿١٤﴾

14.  Yeye Ndiye wa haki kuombwa (na kuabudiwa).[8] Na wale wanaowaomba badala Yake, hawawaitikii kwa chochote isipokuwa kama anayenyoosha viganja vyake viwili vya mikono kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, na wala hayafikii hata kidogo. Na duaa za makafiri hazipo ila katika upotofu.[9]   

 

 

 

وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ۩﴿١٥﴾

15. Na waliomo mbinguni na ardhini humsujudia Allaah Pekee wakipenda wasipende na vivuli vyao pia (vinamsujudia) asubuhi na jioni.[10]

 

 

 

قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ ۚ قُلْ أَفَاتَّخَذْتُم مِّن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ ۗ أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚ قُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿١٦﴾

16.  Sema: Ni nani Rabb wa mbingu na ardhi? Sema: Ni Allaah. Sema: Je, mnawafanya wengineo badala Yake kuwa rafiki walinzi na hali hawamiliki manufaa wala dhara kwa nafsi zao? Sema: Je, kipofu analingana sawa na mwenye kuona, au je, viza vinalingana sawa na nuru? Au wamemfanyia Allaah washirika walioumba kama uumbaji Wake, kisha ukafanana uumbaji kwao (wakakanganyikiwa)?[11]  Sema: Allaah Ni Muumbaji wa kila kitu, Naye Ni Mmoja Pekee, Asiyepingika.

 

 

 

أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌ بِقَدَرِهَا فَاحْتَمَلَ السَّيْلُ زَبَدًا رَّابِيًا ۚ وَمِمَّا يُوقِدُونَ عَلَيْهِ فِي النَّارِ ابْتِغَاءَ حِلْيَةٍ أَوْ مَتَاعٍ زَبَدٌ مِّثْلُهُ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْحَقَّ وَالْبَاطِلَ ۚ فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَاءً ۖ وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ ﴿١٧﴾

17. (Allaah) Ameteremsha kutoka mbinguni maji na mabonde yakatiririka kwa kadiri yake, kisha mbubujiko ukabeba mapovu ya takataka yanayopanda juu yake. Na katika vile wanavyoviwashia moto ili kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Hivyo ndivyo Anavyopiga Allaah (mfano wa) haki na batili. Basi povu la takataka linapita bure bila ya kufaa. Lakini vile vinavyowafaa watu hubakia ardhini. Hivyo ndivyo Allaah Anavyopiga mifano.[12]

 

 

 

لِلَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَالَّذِينَ لَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُ لَوْ أَنَّ لَهُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ سُوءُ الْحِسَابِ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمِهَادُ﴿١٨﴾

18. Wale waliomuitikia Rabb wao watapata Al-Husnaa (Jannah). Na wale wasiomuitikia hata kama wangelikuwa wana vyote viliomo ardhini na mfano wa kama hivyo pamoja, wangelivitoa kujikombolea navyo. Hao watapata hesabu mbaya, na makazi yao ni Jahannam. Ni mahali pabaya mno pa kupumzikia.

 

 

 

أَفَمَن يَعْلَمُ أَنَّمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰ ۚ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٩﴾

19. Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka kwa Rabb wako ni haki, (je,) ni sawa na ambaye yeye ni kipofu? Hakika wanazingatia wenye akili tu.

 

 

 

الَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَلَا يَنقُضُونَ الْمِيثَاقَ ﴿٢٠﴾

20.  Ambao wanatimiza Ahadi ya Allaah,[13] wala hawavunji fungamano.

 

 

 

وَالَّذِينَ يَصِلُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوءَ الْحِسَابِ ﴿٢١﴾

21. Na ambao wanaunga yale Aliyoamrisha Allaah kuungwa[14] na wanamkhofu Rabb wao, na wanakhofu hesabu mbaya.

 

 

 

وَالَّذِينَ صَبَرُوا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٢﴾

22. Na ambao wamesubiri kutaka Wajihi wa Rabb wao, na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa katika yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri, na wanaepusha ovu kwa zuri, hao watapata hatima njema ya makazi ya Aakhirah.

 

 

 

 

جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ﴿٢٣﴾

23. Jannaat za kudumu milele wataingia pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao na wake zao na dhuria zao.[15] Na Malaika wanawaingilia katika kila milango (wakiwaamkua).

 

 

 

سَلَامٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٤﴾

24. Salaamun ‘Alaykum! (Amani iwe juu yenu) kwa subira mliyoshikamana nayo. Basi uzuri ulioje hatima njema ya makazi ya Aakhirah!  

 

 

 

وَالَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ ۙ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ ﴿٢٥﴾

25.  Na wale wanaovunja Ahadi ya Allaah baada ya kufungamana kwake na wanakata yale Aliyoyaamrisha Allaah kuwa yaungwe na wanafanya ufisadi katika ardhi, hao watapata laana na watapata makazi mabaya (motoni).

 

 

 

اللَّـهُ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ وَفَرِحُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا مَتَاعٌ ﴿٢٦﴾

26. Allaah Anamkunjulia riziki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Nao wamefurahia uhai wa dunia, na hali uhai wa dunia kulingana na Aakhirah si chochote ila ni starehe ya muda tu.  

 

 

 

وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ ۗ قُلْ إِنَّ اللَّـهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَنْ أَنَابَ ﴿٢٧﴾

27. Na wanasema wale waliokufuru: Mbona basi asiteremshiwe Aayah (Muujiza) kutoka kwa Rabb wake? Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم):  Hakika Allaah Anampotoa Amtakaye na Anamuongoza kuelekea Kwake anayerudi kutubia. 

 

 

 

 

الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾

28. Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa Dhikru-Allaah. Tanabahi!  Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia![16]

 

 

 

 

الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ طُوبَىٰ لَهُمْ وَحُسْنُ مَآبٍ ﴿٢٩﴾

29. Wale walioamini na wakatenda mema watapata mazuri ya kuwafurahisha na kutuza nyoyo na marejeo mazuri (Jannah).

 

 

 

 

 

كَذَٰلِكَ أَرْسَلْنَاكَ فِي أُمَّةٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهَا أُمَمٌ لِّتَتْلُوَ عَلَيْهِمُ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَـٰنِ ۚ قُلْ هُوَ رَبِّي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ مَتَابِ ﴿٣٠﴾

30.  Hivyo ndivyo Tumekutuma katika ummah ambao zimepita kabla yake nyumati (nyenginezo) ili uwasomee yale Tuliyokufunulia Wahy, nao wanamkufuru Ar-Rahmaan. Sema: Yeye Ndiye Rabb wangu, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Kwake natawakali na Kwake ni   marejeo yangu na tubio langu.

 

 

 

وَلَوْ أَنَّ قُرْآنًا سُيِّرَتْ بِهِ الْجِبَالُ أَوْ قُطِّعَتْ بِهِ الْأَرْضُ أَوْ كُلِّمَ بِهِ الْمَوْتَىٰ ۗ بَل لِّلَّـهِ الْأَمْرُ جَمِيعًا ۗ أَفَلَمْ يَيْأَسِ الَّذِينَ آمَنُوا أَن لَّوْ يَشَاءُ اللَّـهُ لَهَدَى النَّاسَ جَمِيعًا ۗ وَلَا يَزَالُ الَّذِينَ كَفَرُوا تُصِيبُهُم بِمَا صَنَعُوا قَارِعَةٌ أَوْ تَحُلُّ قَرِيبًا مِّن دَارِهِمْ حَتَّىٰ يَأْتِيَ وَعْدُ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿٣١﴾

31. Na kama ingelikuweko Qur-aan ambayo kwayo milima ingeliondoshwa au ardhi ikapasuliwa au wafu wakasemeshwa (basi ni Qur-aan hii hii), bali ni ya Allaah amri ya mambo yote. Je, hawakukata tamaa wale walioamini kwamba kama Angetaka Allaah bila shaka Angeliwahidi watu wote. Na hayatoacha kuwasibu wale waliokufuru maafa ya kuteketeza kwa sababu ya yale waliyoyatenda, au yakawateremkia karibu na nyumba zao, mpaka ifike Ahadi ya Allaah. Hakika Allaah Hakhalifu miadi.

 

 

 

وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِّن قَبْلِكَ فَأَمْلَيْتُ لِلَّذِينَ كَفَرُوا ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ عِقَابِ ﴿٣٢﴾

32. Na kwa yakini walifanyiwa istihzai Rusuli kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Nikawapa muhula wale waliokufuru, kisha Nikawachukua kuwaadhibu. Basi ilikuwaje Ikabu[17] Yangu!

 

 

 

 

 

أَفَمَنْ هُوَ قَائِمٌ عَلَىٰ كُلِّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۗ وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ قُلْ سَمُّوهُمْ ۚ أَمْ تُنَبِّئُونَهُ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي الْأَرْضِ أَم بِظَاهِرٍ مِّنَ الْقَوْلِ ۗ بَلْ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا مَكْرُهُمْ وَصُدُّوا عَنِ السَّبِيلِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٣٣﴾

33. Je, basi Anayeisimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, (ni sawa na waabudiwa wa uongo?). Hata hivyo wanamfanyia Allaah washirika. Sema: Watajeni! Au, mnampa khabari kwa yale Asiyoyajua katika ardhi, au ni kudhihirisha maneno ya uongo tu? Bali waliokufuru wamepambiwa njama zao na wamezuiliwa na njia (ya haki). Na ambaye Allaah Amempotoa, basi hana wa kumhidi.

 

 

 

لَّهُمْ عَذَابٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَقُّ ۖ وَمَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مِن وَاقٍ ﴿٣٤﴾

34. Watapata adhabu katika uhai wa dunia, na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni ya mashaka zaidi. Na hawatopata mbele ya Allaah wa kuwahami.

 

 

 

مَّثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ أُكُلُهَا دَائِمٌ وَظِلُّهَا ۚ تِلْكَ عُقْبَى الَّذِينَ اتَّقَوا ۖ وَّعُقْبَى الْكَافِرِينَ النَّارُ ﴿٣٥﴾

35. Mfano wa Jannah ambayo wameahidiwa wenye taqwa, inapita chini yake mito. Makulaji yake ya kudumu, na pia kivuli chake. Hiyo ndiyo hatima ya Aakhirah ya wale waliokuwa na taqwa. Na hatima ya makafiri ni moto.

 

 

 

وَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَفْرَحُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ ۖ وَمِنَ الْأَحْزَابِ مَن يُنكِرُ بَعْضَهُ ۚ قُلْ إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّـهَ وَلَا أُشْرِكَ بِهِ ۚ إِلَيْهِ أَدْعُو وَإِلَيْهِ مَآبِ ﴿٣٦﴾

36. Na wale Tuliowapa Kitabu (wakaamini) wanafurahia kwa yale yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na miongoni mwa makundi wako wanaoyakanusha baadhi yake. Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimwabudu Allaah, na nisimshirikishe. Kwake nalingania na Kwake ni marejeo yangu.

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ حُكْمًا عَرَبِيًّا ۚ وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُم بَعْدَ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ مَا لَكَ مِنَ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا وَاقٍ ﴿٣٧﴾

37.  Na hivyo ndivyo Tumeiteremsha (Qur-aan) kuwa ni Hukmu (Sharia) kwa Kiarabu. Na kama utafuata hawaa zao baada ya kukujia ilimu, basi hutokuwa na rafiki msaidizi yeyote wala mwenye kukuhami mbele ya Allaah.

 

 

 

 

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً ۚ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ لِكُلِّ أَجَلٍ كِتَابٌ﴿٣٨﴾

38. Na kwa yakini Tulituma Rusuli kabla yako, na Tukawajaalia wawe na wake na dhuria. Na haiwi kwa Rasuli yeyote kuleta Aayah (Muujiza) isipokuwa kwa Idhini ya Allaah. Kila kipindi kina hukmu iliyoandikwa.

 

 

 

 

يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ﴿٣٩﴾

39. Allaah Anafuta yale Ayatakayo na Anathibitisha (Ayatakayo), na Kwake kiko Ummul-Kitaab.[18]  

 

 

 

وَإِن مَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ ﴿٤٠﴾

40. Na kama Tutakuonyesha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) baadhi ya yale Tunayowaahidi (ya adhabu), au Tukikufisha (basi usijali), lako wewe ni kubalighisha (Risala) tu, na Letu Sisi ni hesabu.

 

 

 

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَأْتِي الْأَرْضَ نَنقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَا ۚ وَاللَّـهُ يَحْكُمُ لَا مُعَقِّبَ لِحُكْمِهِ ۚ وَهُوَ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴿٤١﴾

41. Je, hawaoni kwamba Tunaifikia ardhi Tukaipunguza mipaka yake? Na Allaah Anahukumu na hakuna wa kupinga Hukmu Yake. Naye Ni Mwepesi wa kuhesabu.

 

 

 

وَقَدْ مَكَرَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلِلَّـهِ الْمَكْرُ جَمِيعًا ۖ يَعْلَمُ مَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ ۗ وَسَيَعْلَمُ الْكُفَّارُ لِمَنْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٤٢﴾

42. Na kwa yakini walifanya makri wale wa kabla yao, basi Allaah Ana mipango yote ya kulipiza makri. Allaah Anajua yale yote yanayochumwa na kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani itakuwa hatima njema ya makazi ya Aakhirah.

 

 

 

وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَسْتَ مُرْسَلًا ۚ قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَمَنْ عِندَهُ عِلْمُ الْكِتَابِ﴿٤٣﴾

43.  Na wanasema waliokufuru: Wewe si Rasuli uliyetumwa. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Anatosheleza Allaah kuwa Ni Shahidi baina yangu na baina yenu, na pia (shahidi) yule mwenye ilimu ya Kitabu. 

 

 

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Istawaa اسْتَوَى

Yuko juu kwa namna inayolingana na Uadhama na Ujalali Wake Yeye Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-A'raaf (7:54) kwenye maelezo bayana ya maana yake, yenye kutofautiana na maana ya katika Suwrah Al-Baqarah (2:29) na Suwrat Fusswilat (41:11).

 

[3] Dalili Za Allaah (سبحانه وتعالى) Kwa Watu Wanaotia Akilini:

 

Na kwenye ardhi kuna sehemu zinazopakana. Kati ya hizo kuna zilizo nzuri zenye kuotesha mimea inayowafaa watu, na kati ya hizo kuna kavu zenye chumvi zisizootesha chochote. Na katika ardhi nzuri kuna mashamba ya zabibu, na Amejaalia humo aina tafauti za mazao na mitende iliyokusanyika mahali pamoja na isiyokusanyika hapo, vyote hivyo viko katika mchanga mmoja na vinakunywa maji mamoja, isipokuwa vinatafautiana katika matunda, ukubwa, utamu na mengineyo; hili ni tamu na hili ni kali, hili ni chungu, na mengine ni bora kuliko mengine katika kula. Katika hilo kuna dalili kwa mwenye moyo unaoyaelewa maamrisho ya Allaah (سبحانه وتعالى) na makatazo Yake. [Tafsiyr Al-Muyassar] Na Imaam As-Sa’diy ameuliza baada ya maelezo hayo:

 

“Je, tofauti hizo zinatokana na mimea yenyewe na asili zake, au hayo yote ni Qudura ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika Mwenye Kurehemu? [Tafsiyr As-Sa’diy]

Rejea pia Yaasiyn (36:38).

 

[4] Washirikina Hawakuamini Kuwa Watafufuliwa: 

 

Rejea Al-Israa (17:49) kwenye maelezo bayana na rejea mbali mbali.

 

[5] Makafiri Wataingizwa Motoni Na Kufungwa Minyororo Shingoni Mwao:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja kuwa makafiri watafungwa minyororo shingoni mwao. Hii ni ishara ya kifungo kama vile mtu anayefungwa gerezani. Rejea pia Yaasiyn (36:8), Saba-a (34:33), Ghaafir (40:71), na Al-Insaan (76:4). Allaah (سبحانه وتعالى) Anatumia maneno haya hapa na katika Aayah nyenginezo kimafumbo ili kuonyesha kuwa wao ni watumwa wa ujinga, ukaidi, na tamaa, na ni wafuasi vipofu wa mababu zao. Kwa vile mawazo yao yameathiriwa na chuki zao, hawawezi kuamini Aakhirah. Wanakanusha kufufuliwa na kuhesabiwa ilhali kuna kila sababu ya kuamini kwamba hayo hayaepukiki. Na wao walikuwa si chochote kabla ya kuumbwa, na Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) kuwafufua viumbe ni jambo jepesi mno Kwake. Rejea At-Taghaabun (64:7). Juu ya hivyo, Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) kuumba kiumbe ni jambo jepesi mno kuliko kuumba mbingu na ardhi. Rejea Ghaafir (40:57). Na kufufua viumbe na kuwaumba upya ni jambo jepesi mno Kwake Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Ar-Ruwm (30:27).

 

[6] Malaika Wanaolinda Waja Wa Allaah Usiku Na Mchana:  

 

Imaam As-Sa’diy amesema: Wanaulinda mwili na roho yake kutokana na kila anayemtakia mabaya, na wanachunga amali zake, na wanaambatana naye daima. Na juu ya kuwa Ilimu ya Allaah inamzunguka, pamoja na hivyo, Allaah Amewatuma Malaika hawa walinzi kwa Waja Wake, kwa namna ambayo hali zao na matendo yao haiwezekani kufichika, na hakuna chochote kinachosahaulika kutokana na hayo. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na Hadiyth ifuatayo imefafanua:

 

حَدَّثَنَا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ يُوسُفَ، قَالَ حَدَّثَنَا مَالِكٌ، عَنْ أَبِي الزِّنَادِ، عَنِ الأَعْرَجِ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ يَتَعَاقَبُونَ فِيكُمْ مَلاَئِكَةٌ بِاللَّيْلِ وَمَلاَئِكَةٌ بِالنَّهَارِ، وَيَجْتَمِعُونَ فِي صَلاَةِ الْفَجْرِ وَصَلاَةِ الْعَصْرِ، ثُمَّ يَعْرُجُ الَّذِينَ بَاتُوا فِيكُمْ، فَيَسْأَلُهُمْ وَهْوَ أَعْلَمُ بِهِمْ كَيْفَ تَرَكْتُمْ عِبَادِي فَيَقُولُونَ تَرَكْنَاهُمْ وَهُمْ يُصَلُّونَ، وَأَتَيْنَاهُمْ وَهُمْ يُصَلُّونَ ‏"‏‏.‏

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Wanakujieni kwa zamu; Malaika wa mchana na Malaika wa usiku, na wote wanajumuika wakati wa Swalaah ya Alfajiri na Swalaah ya Alasiri. Wale waliokesha nanyi usiku hupanda (mbinguni) na Allaah Huwauliza - Naye Allaah Anajua vyema hali yao-   Mmewaachaje Waja Wangu?  Malaika hujibu:  Tumewaacha wakiwa wanaswali, na tumewafikia wakiwa wanaswali.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

[7] Duaa Ya Kuomba Inapotokea Radi:

 

‘Abdullaah bin Zubayr (رضي الله عنه) alikuwa anaposikia radi, basi huacha mazungumzo na badala yake husema:

سُبْـحانَ الّذي يُسَبِّـحُ الـرَّعْدُ بِحَمْـدِهِ، وَالملائِكـةُ مِنْ خيـفَته.

Ametakasika Yule Ambaye radi zinamsabihi kwa Himdi Zake na Malaika pia (wanamsabihi) kwa kumkhofu. [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Zubayr (رضي الله عنه), Al-Muwattwa (2/992), na Al-Albaaniy (رحمه الله) amesema: Isnaad yake ni Swahiyh Mawquwfaa]

 

[8] Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee Ana Haki Ya Kuabudiwa:

 

Ni kumwabudu Yeye (Allaah) Pekee Asiye na mshirika, na kumtakasia Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) niyya katika duaa ya ibaada na maombi mengineyo; yaani Yeye Ndiye Anayepaswa kuelekezewa duaa, khofu, matarajio, mapenzi. raghba (utashi), kuogopwa, na kurejea Kwake, kwa sababu Uluwhiyyah (kumpwekesha Allaah katika ibaada) Kwake ndio Uluwhiyyah ya haki, na Uluwhiyyah kwa asiyekuwa Yeye ni batili. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[9] Duaa Za Washirikina Na Makafiri Kwa Waabudiwa Wao Haziitikiwi, Mfano Wa Maji Kutokuwafikia Vinywani Mwao Katika Kiu Kikali: 

 

Ni kama hali ya mtu mwenye kiu kikali mno anayenyoosha mkono wake kuyaelekea maji yaliyoko mbali ayachote yamfikie mdomoni mwake lakini hayamfikii! Na hii ndio hali ya makafiri na washirikina wanaowaomba waabudiwa wao lakini hawawaitikii kwa lolote wala  hawawapatii haja zao, kwa sababu wao wenyewe ni masikini wahitaji kama walivyo waabudiwa wao wanaowaomba, hawamiliki uzito wa chembe ardhini wala mbinguni. Rejea Saba-a (34:22), Faatwir (35:13-14).

 

[10] Kila Kiumbe Na Vitu Vyote Vinamsujudia Allaah (سبحانه وتعالى)  Na Kumsabbih:

 

Rejea An-Nahl (16:48-50), Al-Israa (17:44), Al-Hajj (22:18), Al-A’raaf (7:206), Ar-Rahmaan (55:6).

 

[11] Ufafanuzi Wa Washirikina Kwamba Wamechanganyikiwa Akili Hawatambui Walivyoumba Wao Na Alivyoumba Allaah (عزّ وجلّ):

 

Au ni kwamba wale wasimamizi wao wanaowafanya ni washirika wa Allaah (سبحانه وتعالى)  wanaumba kama Anavyoumba Allaah (سبحانه وتعالى)  vikawatatiza (na kuwachanganya akili) viumbe vya washirika na viumbe vya Allaah (سبحانه وتعالى) ndipo wakaitakidi kwamba wao wanastahiki kuabudiwa? [Tafsiyr Al-Muyassar].

 

Je, hawa washirikina wanaabudu miungu isiyokuwa Yeye (Allaah) inayoshindana Naye katika Alichokiumba? Je, waungu wao wa uwongo wameumba viumbe vinavyofanana na Alivyoviumba Allaah, na hivyo wamechanganyikiwa (akili) baina ya aina mbili za viumbe, bila ya kujua ni kipi kimeumbwa na wengine badala ya Allaah! [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Ni swali la kuwataka wafungue akili zao. Allaah Kawaumba wao, Akawapa uhai, nguvu, afya, akili na kila kitu, nao bado ni viumbe ajizi, hawawezi lolote. Na hiyo miungu yao ambayo wao wanaitengeneza kwa mikono yao, ndio ajizi zaidi kuliko wao wenyewe. Vipi basi itaweza kuumba chochote kifanane na Alivyoviumba Allaah?

 

[12] Mfano Wa Haki Na Batili:

 

Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akapiga mfano wa ukweli na urongo kuwa ni kama maji Aliyoyateremsha kutoka juu, yakapita kwenye mabonde ya ardhi kwa kadiri ya udogo wake na ukubwa wake. Mikondo ya maji ikabeba povu likiwa juu yake lisilo na faida. Na Akapiga mfano mwingine wa madini ambayo watu huyachoma moto ili kuyayeyusha kutaka kutengeneza pambo, kama vile dhahabu na fedha, au kutaka manufaa ya kujinufaisha, kama vile shaba, ukatoka uchafu wake usio na faida kama ule uliokuwa pamoja na maji. Kwa mfano huu, Allaah (سبحانه وتعالى) Apigia mfano ukweli na urongo. Urongo ni kama povu la maji, linapotea au linatupwa kwa kuwa halina faida, na ukweli ni kama maji safi na madini yaliyotakasika, yanasalia kwenye ardhi kwa kunufaika nayo. Kama Alivyowafafanulia nyinyi mifano hii, hivyo ndivyo Anavyoipiga kwa watu upate kufunuka wazi ukweli ujitenge na urongo, na uongofu ujitenge na upotevu. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[13] Ahadi ya Alastu  - Rejea Al-Ar’aaf (7:172), na Suwrah hii Ar-Ra’d (13:25).

 

[14] Kuunga Aliyoyaamrisha Allaah:

 

 Ni kuunga mambo ya kiujumla, nayo ni mengi katika kila Alichoamrisha Allaah (سبحانه وتعالى) kuungwa kama vile kumuamini Yeye na Rasuli Wake, kumpenda Yeye na Rasuli Wake, kumuabudu Yeye Pekee bila ya kumshirikisha, na kumtii Yeye na Rasuli Wake. Na Pia, kuwasiliana na kuungana na baba zao na mama zao kwa ihsaan na wema kwa kauli na matendo, bila kuwaasi. Vile vile, wanawasiliana na kuwaunga jamaa na Arhaam (ndugu na jamaa wenye uhusiano wa damu) kwa kuwatendea ihsaan na wema kwa kauli na matendo, na wanaunganisha yaliyo baina yao na baina ya waume na wake zao, rafiki zao na watumwa wao kwa kutimizia haki zao kikamilifu, haki za kidini na za dunia. [Tafsiyr As-Sa’diy)]

 

Rejea Suwrah hii Ar-Ra’d (13:25). Ama kuhusu kukata undugu, basi kuna Laana ya Allaah, Rejea Muhammad (47:22-23).

 

[15] Fadhila Ya Kuhidika Pamoja Na Wazee, Wana Na Jamaa Wa Karibu:  

 

Hii ni sawa na Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrah Atw-Twuwr (52:21) kwamba watu wenye uhusiano kama huu wa imaan watakutanishwa kuwa pamoja katika Jannah.

 

[16] Nyoyo Kutua Kwa Dhikru-Allaah (Kumdhukuru Allaah):

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja alama za Waumini Anaposema:

الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ

“Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa Dhikru-Allaah.”

 

Yaani: Wahka, wasiwasi, mashaka yao hutoweka, na badala yake kubadilishiswa furaha na raha.

أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾

“Tanabahi!  Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia.”  

 

Yaani: Hii ni asili yao (Waumini) na ni ya kutarajiwa kwamba wao hawapati faraja kwa chochote isipokuwa kwa Dhikru-Allaah kwa sababu hakuna kinacholeta furaha kubwa ya nyoyo na hakuna kitu kinachohitajika zaidi na chenye ladha  zaidi moyoni isipokuwa  Kumpenda Muumba wake, na kujikurubisha Kwake na  maarifa Yake (kumtambua Kwa Majina Yake Mazuri na Sifa Zake). Basi kulingana na jinsi ya maarifa ya Allaah na kumpenda Kwake, ndivyo itakavyokuwa kiwango cha kumdhukuru.   Kinachomaanishwa ni kuwa Dhikru-Allaah, ni mja kumdhukuru Allaah kwa Tasbiyh (Kumtakasa), Tahliyl (Kumpwekesha), na Takbiyr (Kumtukuza) na vinginevyo.

 

Na ikasemwa: Maana ya Dhikru-Allaah ni Kitabu Chake Alichokiteremsha kuwa ukumbusho kwa Waumini. Na kinachomaanisha nyoyo kutulia kwa Dhikru-Allaah, ni pindi moyo unapojua na kufahamu  maana za Qur-aan na hukumu zake basi  moyo hutulia kwa sababu    (Qur-aan) inabainisha ukweli uliowazi unaoungwa mkono na burhani (dalili za waziwazi) hivyo basi nyoyo hutulia kwani   nyoyo hazitulii ila kwa yakini na ilimu. Na hayo yamo katika Kitabu cha Allaah kilichohakikishwa kwa utimilifu na ukamilifu. Ama vitabu vingine ambavyo haviambatani na nyoyo, basi nyoyo hazitapata utulivu bali zitabakia kuwa na wahka, mashaka wasiwasi kwa sababu ya kukinzana ushahidi wake na hukmu zake. Na ndio Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا ﴿٨٢﴾

“Je, hawaizingatii Qur-aan? Na lau ingelikuwa imetoka kwa asiyekuwa Allaah, bila shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi.” [An-Nisaa (4:82)]

[Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[17] Tofauti Ya Ikabu Na Adhabu: Rejea Al-Hashr (59:4).

 

[18] Ummul-Kitaab (Mama Wa Kitabu):

 

Katika Aayah hii, Ummul-Kitaab imekusudiwa Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa) Rejea Al-Buruwj (85:22). Ndani yake humo, Allaah Ameandika yote yaliyotokea na yatakayotokea mpaka Siku ya Qiyaamah. Na maana nyengineyo ya Ummul-Kitaab ni mojawapo ya majina ya Suwrah Al-Faatihah.

 

 

 

Share