032 - As-Sajdah

 

 

 

  السَّجْدَة

 

As-Sajdah: 032

 

(Imeteremka Makkah)

 

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

الم ﴿١﴾

1. Alif Laam Miym.

 

 

تَنزِيلُ الْكِتَابِ لَا رَيْبَ فِيهِ مِن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾

2. Ni uteremsho wa Kitabu, hauna shaka ndani yake, umetoka kwa Rabb wa walimwengu.  

 

 

 

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۚ بَلْ هُوَ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أَتَاهُم مِّن نَّذِيرٍ مِّن قَبْلِكَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ ﴿٣﴾

3. Au wanasema ameitunga (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم hii Qur-aan)? Bali hiyo ni haki kutoka kwa Rabb wako ili uonye watu ambao hawakufikiwa na mwonyaji yeyote kabla yako, huenda wakahidika.

 

 

 

اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ مَا لَكُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا شَفِيعٍ ۚ أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ ﴿٤﴾

4. Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arsh. Nyinyi hamna badala Yake mlinzi yeyote wala mwombezi. Je, basi hamkumbuki?

 

 

 

يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مِنَ السَّمَاءِ إِلَى الْأَرْضِ ثُمَّ يَعْرُجُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ أَلْفَ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٥﴾

5. Anadabiri mambo kutoka mbinguni mpaka ardhini, kisha inapanda Kwake katika siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu katika ile mnayoihesabu nyinyi.

 

 

 

ذَٰلِكَ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٦﴾

6. Huyo Ndiye Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, Mwenye Enzi na Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ ۖ وَبَدَأَ خَلْقَ الْإِنسَانِ مِن طِينٍ ﴿٧﴾

7. Ambaye Amefanya uzuri kila kitu Alichokiumba, na Akaanzisha uumbaji wa insani kutokana na udongo.

 

 

 

ثُمَّ جَعَلَ نَسْلَهُ مِن سُلَالَةٍ مِّن مَّاءٍ مَّهِينٍ ﴿٨﴾

8. Kisha Akajaalia kizazi chake kutokana na mchujo safi wa maji dhalilifu.

 

 

 

ثُمَّ سَوَّاهُ وَنَفَخَ فِيهِ مِن رُّوحِهِ ۖ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۚ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٩﴾

9. Kisha Akamsawazisha, na Akapuliza humo roho yake (Aliyoiumba Allaah). Na Akakujaalieni kusikia na kuona na nyoyo, ni machache mno yale mnayoshukuru.

 

 

 

وَقَالُوا أَإِذَا ضَلَلْنَا فِي الْأَرْضِ أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ ۚ بَلْ هُم بِلِقَاءِ رَبِّهِمْ كَافِرُونَ ﴿١٠﴾

10. Na wakasema: Je, tutakapokwisha kufa na tukapotea chini ya ardhi je, hivi kweli sisi tutaumbwa katika umbo jipya?! Bali wao ni wenye kukanusha kukutana na Rabb wao. 

 

 

قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ ﴿١١﴾

11. Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu, kisha kwa Rabb wenu mtarejeshwa.

 

 

 

وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الْمُجْرِمُونَ نَاكِسُو رُءُوسِهِمْ عِندَ رَبِّهِمْ رَبَّنَا أَبْصَرْنَا وَسَمِعْنَا فَارْجِعْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا إِنَّا مُوقِنُونَ ﴿١٢﴾

12. Na ungeliona pale wahalifu wanainamisha vichwa vyao mbele ya Rabb wao (wakisema): Rabb wetu! Tumekwishaona, na tumeshasikia, basi turejeshe tutende mema, hakika sisi sasa ni wenye yakini.

 

 

 

وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴿١٣﴾

13. Na Tungelitaka, Tungeliipa kila nafsi mwongozo wake, lakini imethibiti kauli kutoka Kwangu kwamba: Bila shaka Nitajaza Jahannam kwa majini na watu pamoja.

 

 

 

فَذُوقُوا بِمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا إِنَّا نَسِينَاكُمْ ۖ وَذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٤﴾

14. Basi onjeni kwa sababu ya kusahau kwenu kukutana na Siku yenu hii. Hakika Nasi Tumekusahauni. Na onjeni adhabu yenye kudumu milele kutokana na yale mliyokuwa mkiyatenda.

 

 

 

إِنَّمَا يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا الَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِهَا خَرُّوا سُجَّدًا وَسَبَّحُوا بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ ۩﴿١٥﴾

15. Hakika wanaamini Aayaat Zetu wale wanapokumbushwa nazo huporomoka kusujudu, na wakasabbih wakimhimidi Rabb wao, nao hawatakabari.

 

 

 

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿١٦﴾

16. Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa.

 

 

 

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٧﴾

17. Basi nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.

 

 

 

أَفَمَن كَانَ مُؤْمِنًا كَمَن كَانَ فَاسِقًا ۚ لَّا يَسْتَوُونَ ﴿١٨﴾

18. Je, aliye Muumini atakuwa sawa na aliye fasiki? Hawalingani sawa!

 

 

 

أَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ جَنَّاتُ الْمَأْوَىٰ نُزُلًا بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٩﴾

19. Ama wale walioamini na wakatenda mema, basi watapata Jannaat za makazi mazuri, takrima kwa yale waliyokuwa wakitenda.

 

 

 

وَأَمَّا الَّذِينَ فَسَقُوا فَمَأْوَاهُمُ النَّارُ ۖ كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا أُعِيدُوا فِيهَا وَقِيلَ لَهُمْ ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ ﴿٢٠﴾

20. Na ama wale waliofanya ufasiki, basi makazi yao ni motoni. Kila watakapotaka kutoka humo, watarudishwa humo, na wataambiwa: Onjeni adhabu ya moto ambayo mlikuwa mnaikadhibisha.

 

 

 

وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنَ الْعَذَابِ الْأَدْنَىٰ دُونَ الْعَذَابِ الْأَكْبَرِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٢١﴾

21. Na bila shaka Tutawaonjesha adhabu ndogo kabla ya adhabu kubwa huenda wakarejea (kutubia).

 

 

 

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن ذُكِّرَ بِآيَاتِ رَبِّهِ ثُمَّ أَعْرَضَ عَنْهَا ۚ إِنَّا مِنَ الْمُجْرِمِينَ مُنتَقِمُونَ ﴿٢٢﴾

22. Na nani dhalimu zaidi kuliko yule anayekumbushwa Aayaat za Rabb wake, kisha akazikengeukia? Hakika Sisi Tutawalipiza wahalifu.

 

 

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَلَا تَكُن فِي مِرْيَةٍ مِّن لِّقَائِهِ ۖ وَجَعَلْنَاهُ هُدًى لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿٢٣﴾

23. Na kwa yakini Tulimpa Muwsaa Kitabu, basi usiwe na shaka katika kukutana naye. Na Tukakijaalia ni mwongozo kwa wana wa Israaiyl.

 

 

 

وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ ﴿٢٤﴾

24. Na Tukawajaalia miongoni mwao Maimamu wanaongoza kwa Amri Yetu waliposubiri, na walikuwa wakiziyakinisha Aayaat (na Ishara) Zetu.

 

 

 

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٢٥﴾

25. Hakika Rabb wako Ndiye Atakayepambanua baina yao Siku ya Qiyaamah katika yale yote waliyokuwa wakikhitilafiana.

 

 

 

أَوَلَمْ يَهْدِ لَهُمْ كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْقُرُونِ يَمْشُونَ فِي مَسَاكِنِهِمْ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ ۖ أَفَلَا يَسْمَعُونَ ﴿٢٦﴾

26. Je, haijawabainikia karne ngapi Tumeangamiza kabla yao, nao wanapita katika masikani yao? Hakika katika hayo mna ishara na mazingatio. Je, basi hawasikii?

 

 

 

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَسُوقُ الْمَاءَ إِلَى الْأَرْضِ الْجُرُزِ فَنُخْرِجُ بِهِ زَرْعًا تَأْكُلُ مِنْهُ أَنْعَامُهُمْ وَأَنفُسُهُمْ ۖ أَفَلَا يُبْصِرُونَ ﴿٢٧﴾

27. Je hawaoni kwamba Sisi Tunayaendesha maji katika ardhi kame, kisha Tunatoa kwayo mimea, wanakula humo wanyama wao wa mifugo na wao wenyewe! Je, basi hawaoni?

 

 

 

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْفَتْحُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٢٨﴾

28. Wanasema: Ni lini itakuwa kuhukumiwa huko ikiwa nyinyi ni wakweli?

 

 

 

 

قُلْ يَوْمَ الْفَتْحِ لَا يَنفَعُ الَّذِينَ كَفَرُوا إِيمَانُهُمْ وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ ﴿٢٩﴾

29. Sema: Siku ya hukmu haitowafaa wale waliokufuru iymaan zao, na wala hawatopewa muhula.

 

 

 

فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَانتَظِرْ إِنَّهُم مُّنتَظِرُونَ ﴿٣٠﴾

30. Jiepushe nao na ngojea (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), hakika wao (pia) wanangojea.

 

 

Share