Mume Na Watoto Hawaswali Na Hawataki Kunisikiliza

SWALI:

Assalam alaykum swala langu ni: mimi ni mwanamke nilio olewa na nna watoto swala langu  liko hapa huyu mume wangu na watoto hawataki kuswali na kila siku nawambie na hawataki kunisikia, mimi nnaswali,  Je sala  yangu inakubaliwa wakati wao hawaswali , halafu nimeshachoka kuwambia kila siku kwahiyo nnaomba msaada wenu mnitumie hikma gani? Naomba nijibiwe swala langu maasalam


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani dada yetu kwa swali lako hilo kuhusu usumbufu wa hali ya juu katika ndoa yako. Hili ni tatizo sugu ambalo limezagaa katika jamii yetu. Tatizo hili linatokea kwa sisi kutotilia maanani agizo la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mke kuchagua mume au kinyume chake. Wakati ambapo tutakiuka agizo la kuchagua mwenye Dini, maadili, muruwa, mwenye Ibaadah, basi isipokuwa wale wanaorehemewa na Allaah Aliyetukuka lakini ndoa inatukua na misukosuko mingi.

Wakati mmoja mtu mmoja alikwenda kwa shaykh ili kupata mawaidha jinsi ya kumlea mtoto baada ya mkewe kuzaa. Yule Shaykh alimwambia umechelewa. Mtoto ana haki ya kuchaguliwa baba na mama mzuri na mwema. Ikiwa tutashindwa kutekeleza hivyo basi tunakuwa na matatizo katika uanandoa wetu.

Mara nyingi mtoto huwa anafuata ada na desturi za wazazi wao. Ikiwa mtoto ni wa kiume akawa anamuona baba hashughuliki na Ibaadah basi naye atafuata mtindo huo huo na inamwia vigumu kumuelekeza mtoto huyo.

Mwenyeezi Mungu Akubarikie juhudi zako za kutaka watu wako waongoke kama ulivyo wewe. Jambo hilo ndilo lilihimizwa katika Qur-aan: “Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu, na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe” (66: 6). Kwa hiyo, kwa mujibu wa ayah hii wewe unawajibika katika kugeuza familia yako ili wasiingie katika ghadhabu ya Allaah Aliyetukuka.

Hakika ni kuwa Ibaadah zako zote unazofanya utapata ujira kamili bila kupunguziwa chochote na Allaah Aliyetukuka, ambaye sifa Yake ni Uadilifu. Swalah zako zote utalipwa kamili pamoja na juhudi unazofanya katika kuwavuta watu wako waje waingie katika njia nyoofu inayomridhisha Allaah Aliyetukuka.

Dada yetu katika kazi hii usiseme nimechoka, kwani Muislamu hana nafasi ya kusema hivyo. Hiyo si sifa ya Muislamu wa kihakika. Kuhusu hili Allaah Aliyetukuka Anasema kuelezea namna Nabii Ya'aquub ('Alayhis Salaam) alipokuwa akiwasisitiza wanawe kutokuwa na tabia ya kukata tamaa: “Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yuusuf na nduguye, wala msikate tamaa na rehema ya Allaah. Hawakati tamaa na rehema ya Allaah isipokuwa watu makafiri” (12: 87).

Jambo la kuamrisha Swalah ni jambo lipasalo kuendelezwa na wazazi na kila mchungaji, na hakika ni jambo gumu linalohitaji azma na subira, ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuhimiza nalo Anaposema:

((وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا))

((Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo)) [Twaahaa: 132]

Nasaha ambazo tunaweza kukupa sasa ni kama zifuatazo:

1.  Jaribu kuwa laini kwa mumeo na uwe mpole katika kumrekebisha tatizo lake hilo la kutoswali. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Nendeni (yaani Muusa na Haarun) kwa Firauni, kwani amepindukia mipaka. Kamwambieni maneno laini huenda akashika mawaidha au akaogopa” (20: 43 – 44). Tazama hapa Allaah Aliyetukuka Anawatuma Manabii wake wawili watukufu kwa mtu aliyejidai kuwa ni mungu lakini wakaamriwa waseme naye maneno laini na kwa upole. Na ndio Allaah Aliyetukuka Anatuelezea sifa ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema: “Basi kwa sababu ya rehema itokayo kwa Allaah umekuwa laini kwao. Na kama ungekuwa mkali na mwenye moyo mgumu bila shaka wangalikukimbia” (3: 159).

 

2. Pia jaribu kukaa naye faragha mukiwa yeye na wewe tu ili umpatie nasaha kama mume na mke. Huenda kwa njia hii akawa ni mwenye kukusikiliza katika hilo. Zungumza naye mara moja, mbili na kadhaa. Kwa kukariri kuzungumza naye huenda akabadilika na ikiwa hakubadilika basi fahamu kuwa Allaah Anasema: “Hakika wewe huwezi kumuongoa umpendaye, lakini Allaah humuongoa Amtakaye” (28: 56).

3. Je, kutoswali kwake anaamini kuwa Swalah si wajibu? Ikiwa anaamini hivyo basi huyo ametoka Dini hii ya Uislamu na kukaa na mtu kama huyo haifai kwa Muumini wa kihakika. Lakini kabla ya kuacha naye kabisa unaweza kumpatia fursa ajirekebishe, kwa kumuitia Mashaykh wazungumze naye na asimamishiwe hoja. Hilo likishindikana basi itabidi uitishe kikao ambamo wataitwa wazazi wake na wako pia watakuwepo. Ikiwa katika kikao hicho atashikilia ya kwake basi itakuwa bora uachane naye. Kwa sababu ya kufanya hilo kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka basi Atakutolea lenye kheri nawe kwa kiasi kikubwa zaidi.

4.  Ikiwa kutoswali kwake ni kwa ajili ya uvivu, goi goi na sababu nyenginezo na anatambua kuwa Swalah ni wajibu basi huyo ni asi. Kwa minajili hiyo itabidi uzungumze naye mwanzo. Kukiwa hapana mabadiliko yoyote yale itabidi uitishe mkutano wa wazazi wake na wako ili mujadili suala hilo. Ikiwa ameshikilia ya kwake basi ni bora kabisa kuachana naye.

Kwa kutumia maelekezo hayo tuna yakini kuwa mambo yatabadilika kwa njia nzuri. Nasi hapa tunakuombea kila la kheri na fanaka katika shughuli hiyo na Allaah Akupatie tawfiki.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share