Wanaume Kuoa Wake Wanne Na Wanawake Kuolewa Na Mume Mmoja

 

Wanaume Kuoa Wake Wanne Na Wanawake  Kuolewa Na Mume Mmoja

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Assalam Alaikum,

 

Mimi nawa andikia nikiwa mgeni katika dini hiyi ya Allaah ninayo mswali ambayo ningelipenda kujua majibu yake kwani yatachangia kuniweka sawa na kuifuata vyema dini ya Allaah.

 

Nataka Kujua Kwa Nini Dini Ya Islam Inaruhusu Mwana ume Kuowa Mke ZaidiYa Mmoja (Na Kusudia Kuowa Wake Wengi) Na Kwa nini Dini Haimruhusu Mwana Mke Wa Kiislam Kuolewa Na Mwana Ume Zaidi Ya Mmoja?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

.

 

Ni jambo linaloeleweka kuwa Uislamu ni mfumo kamili wa maisha ya mwanaadamu kwa ujumla na Waislamu hasa. Japokuwa mfumo huu ambao unamtoa mtu matatani unakimbiwa na wengi. Hakuna lolote isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametuelezea. 

 

Hakika muulizaji, wewe ulikuwa Muislamu lakini mazingira yamekufanya wewe ulelekee katika dini nyengine isiyo ya kimaumbile. Hilo ni kwa mujibu wa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Kila kinachozaliwa kinazaliwa katika Fitwrah (maumbile ya asli ya Uislamu ‘Tawhiyd’) ni wazazi wake ndio wanamfanya awe Myahudi au Mkristo au Majusi". [Al-Bukhaariy].

 

Ukweli ni kuwa si kila kitu kimeelezwa hekima yake lakini Wanachuoni wanajitahidi kuangalia hekima ya mambo kadhaa ambayo yamo katika Qur-aan Tukufu au Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo, Imani ya Muislamu ni kuwa hata asipopata hekima ya amri au katazo fulani basi yeye huwa ni mwenye kusema:

 سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ

Tumesikia na tumetii... [Al-Baqarah: 285].

 

Waislamu huwa kabisa hawafuati ile sifa ya Mayahudi ya kusema:

سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا

Tumesikia na tumeasi. [Al-Baqarah: 93].

 

Kwa minajili hiyo, Muislamu huwa hapati shida kutii kwani anafahamu kuwa Yule Aliyemuumba Ndiye Anayejua lililo zuri kwake na lenye kumfaa na lililo baya kwake na lenye kumdhuru. Hii ni kanuni muhimu sana kwa kila mmoja kati yetu, Waislamu kuifahamu. Ni ajabu kuwa Mjapani anatengeneza gari akawa ni mwenye kufuatwa kikamilifu na aliyenunua gari. Mwenye gari huyo huwa hata mara moja haendi kinyume na maagizo yaliyotolewa na mtengenezaji huyo, kwani anajua kwa yakini kuwa akienda kinyume kwa mfano badala ya kutia petroli katika injini, yeye akatia maji! Hivyo gari halitaweza kufanya kazi. Vipi maagizo ya Allaah Aliyetukuka tuwe ni wenye kuyapuuza? Jambo haliingii akilini  lakini huwa tunakwenda kinyume katika maamrisho Yake mengi. Tutanabahi na turudi Kwake kabla hatujaondoka katika ulimwengu huu.

 

Hakika ni kuwa Uislamu umehalalisha uke wenza na ukaharamisha mwanamke kuolewa na wanaume wengi. Shari’ah hii iko wazi katika machimbuko ya shari’ah ya Dini juu ya yote ikiwa ni agizo katika Qur-aan. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

 

فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً

Basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne. Lakini mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi mmoja tu...[An-Nisaa: 3].

 

Hii ni Aayah ambayo itabaki kutumika mpaka siku ya Qiyaamah.

 

Katika Sunnah, Mama wa Waumimi, ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa) amesema kuwa wakati wa Ujahiliyyah kulikuwa na ndoa aina nne:

 

 

1. Kama ilivyo wakati huu wetu wa sasa (yaani wakati wao na mpaka sasa kwa mwanamume kwenda kumposa binti kwa wazazi wake).

 

2. Mume kwa kutaka apate mtoto mwenye sifa fulani alikuwa akizungumza na mwanamume mwenye sifa hizo ili awe analala na mkewe. Katikahali hiyo alikuwa mume mwenyewe akitoka kwenye hiyo nyumba mpaka mkewe apate mimba. Akishika mimba alikuwa anarudi nyumbani, akitaka alikuwa akimuingilia au akimngojea mpaka azae.

 

3. Mwanamke alikuwa anaolewa na wanaume wengi na pindi anapozaa alikuwa akiwaita wanaume wote. Mjuzi wa kulinganisha sura alikuwa akiitwa na atakaye chaguliwa alikuwa akichukua jukumu la kumlea mtoto huyo.

 

Madanguro ambamo wanawake walikuwa wakiuza miili yao na juu ya nyumba hizo kulikuwa na bendera yenye kuashiria hilo. Mtu yeyote alikuwa na uhuru wa kuingia na kukidhi haja zake.

 

Alipotumilizwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aina zote za mahusiano baina ya mume na mke zilikatazwa ila ile yiliyotaja katika kipengele cha kwanza [Al-Bukhaariy].

 

Swali la sisi kujiuliza ni, Je, uke wenza na utovu wa maadili? Kulijibu swali hili ni lazima tuangalie dini nyengine kama Uyahudi na Ukristo unasema nini kuhusu hilo kwani tushaona kuwa Uislamu umeruhusu mbali na kuwa imeweka masharti yake. Kulingana na Uyahudi na ukitazama hasa katika Agano la Kale utakuta kuwa Manabii watukufu wengi walikuwa na zaidi ya mke mmoja kwa mfano Abrahamu alikuwa na watatu, Daudi mia moja, Suleiman mia saba na wengineo. Hawa ni vielelezo kwa wenye kufuata dini hiyo.

 

Sasa ikiwa hawa wana wake zaidi ya mmoja upo ubaya gani kwa wafuasi kuwa na wake wengi. Ruhusa hii ya kuoa zaidi ya mke mmoja ilipigwa marufuku na kikao cha Marabai cha Worms katika karne ya 11. Katazo hili mwanzo lilitolewa kwa Mayahudi waliokuwa wakiishi Ujerumani na Kaskazini mwa Ufaransa lakini baadae ikawa ni kwa wafuasi wote.

 

Ukiangalia Ukristo utakuta kuwa, kwa kuwa Agano la Kale ni sehemu ya Biblia ruhusa hiyo itakuwepo bila ya matatizo yoyote. Ni yakini kuwa Yesu wa Biblia alisema hakuna kubatilisha wala kufuta kanuni za Taurati bali kutimiza. Na juu ya yote hayo hakuna hata msitari mmoja katika Agano Jipya unaokataza uke wenza.

 

Westermarck anasema kuwa hakuna kikao hata kimoja katika karne za awali za Kanisa zilizokataza uke wenza. Wafalme walikuwa wakioa zaidi ya mke mmoja kwa mfano mfalme wa Ireland kati ya karne ya sita alikuwa na malkia 2 pamoja na masuria wawili pia. Madhehebu kadhaa yaliruhusu ndoa hizo bila ya matatizo yoyote. Mwaka wa 1531 mhubiri wa Anabaptists akiwa Munster alitangaza hadharani kuwa yule anayetaka kuwa Mkristo wa kweli ni lazima aoe mke zaidi ya mmoja. Na ulimwengu wote unajua kuwa Mormons wanachukulia uke wenza kama agizo la Allaah.

 

Hizi ni dalili zifuatazo kuhusiana na hayo: 

 

Biblia inatueleza kuwa Ibrahimu (Abramu) alikuwa na wake watatu kama tunavyoelezwa: "…na Sarai mkewe Abramu…" (Mwanzo 11: 31). Tena: "Kisha, Sarai akampa Abramu Hagari, mtumwa wake wa kike, Mmisri, awe mke wake" (Mwanzo 16: 3).

 

Na pia: "Abrahamu alioa mke mwingine, jina lake Ketura" (Mwanzo 25: 1). Naye Ya'quub (Yakobo) alikuwa na wake wane kama tunavyoarifiwa na Biblia: "Kisha Yakobo akamwambia Labani, 'Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu'. … Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye" (Mwanzo 29: 21 – 23).

 

Pia: "Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli, binti yake mdogo awe mke wake" (Mwanzo 29: 28). Tena: "Kwa hiyo Raheli akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye" (Mwanzo 30: 4).

 

Pia: "Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mtumishi wake wa kike, na kumpa Yakobo ili awe mkewe" (Mwanzo 30: 9).

 

Biblia inatufahamisha tena kuwa kumbe anayefaa kuwa na mke mmoja ni askofu kumaanisha asiyekuwa askofu anaweza kuwa na zaidi ya mmoja. Hebu tusome: "Basi, askofu anapaswa kuwa mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu" (1 Timotheo 3: 2). Sijui kwa nini maaskofu wa Kikatoliki hawaruhusiwi kuoa kabisa?

 

Mwingine anayefaa kuwa na mke mmoja ni mzee wa Kanisa kama tunavyoarifiwa: "Mzee wa Kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini" (Tito 1: 6).

 

Ni jambo linalojulikana kuwa hata wale wenye kufuata dini za kitamaduni hasa za Kiafrika wanachukua uke wenza kama jambo la kawaida kabisa. Hivyo, katika sehemu ya Kenya wamisheni walibidi wakubali hao kushika baadhi ya mila zao ili wawavutie kuingia katika Ukristo.

 

Ifahamike kuwa Aayah tuliyoinukuu juu (4: 3) ina maelezo ambayo yanafaa yaeleweke ili tuweze kuwa na ufahamu mzuri wa suala hili la uke wenza katika Uislamu. Dondoo zifuatazo zitatusaidia:

 

- Uke wenza si lazima lakini ni jambo linaloruhusiwa.

 

- Ruhusa hiyo si kutekeleza uchu wa mwanamume wa kujitosheleza kimapenzi bali ni kuweza kuwa na huruma kwa wajane, mayatima na wanawake wengineo.

 

Hata katika hali hiyo ya ruhusa uke wenza umewekewa kikwazo kuwa mwanamume hawezi kuoa zaidi ya wanne.

 

Mwanamume ni lazima awafanyie uadilifu wake zake   wote. Huu ni wajibu, na unahusu makazi, chakula, mavazi, na kuwatendea wema. Haya ni majukumu ya mume.

 

Aayah inasema “oa” sio kuteka nyara, kubaka au kutongoza. Kwa hiyo, mwanamke hawezi kushurutishwa au kupatiwa mwanamume ambaye yeye hamtaki.

 

Swali ambalo linaweza kujitokea ni kuwa, je uke wenza unaweza kuwa ndio suluhisho la matatizo yetu ya kijamii? Kabla ya kujibu swali hili tungependa kusema kuwa Uislamu umekuja na shari’ah yenye kuwafaa watu wote kwa zama zote na katika nchi zote. Kwa ajili hiyo haukuweka shari’ah kwa watu wa mijini na kuwasahau watu wa mashambani, au kwa nchi za baridi na kuwapuuza watu katika nchi za joto, au kwa nyakati fulani ikasahau zama zijazo na vizazi vijavyo. Uislamu unakisia dharura na haja za kila mmoja binafsi na jamii kwa ujumla wake.

 

Kadhaalika ni vizuri tutazame vipengele vifuatavyo:

 

1. Mume anayegundua kuwa mkewe hazai kwa sababu ya utasa, maradhi au kwa sababu nyengine yoyote ile. Je, si bora kwa mwanamke, na ni afadhali kwake yeye mwanamume; kuoa yule atakayemhakikishia raghba hiyo ya kupata mtoto na kubaki na mkewe wa kwanza. Bila kufanya hivyo atabaki bila watoto na kukosa ubaba au amuache mkewe na kuoa mke mwengine. Suluhisho hizo mbili zote hazifai na inabaki kwetu kuukubali uke wenza.

 

2. Mwanaume mwenye mke ambaye wakati wote ni mgonjwa au ana wakati mrefu wa hedhi. Mume anaweza kuwa na uchaguzi wa kukandamiza matamanio yake kwa uhai wake wote au amuache mkewe aliye mgonjwa wakati ambao mke anahitaji huruma zaidi au anaweza mume kubaki naye lakini akawa na vimada nje ya ndoa. Ukitazama haya mambo matatu utakuta kuwa la kwanza ni dhidi ya maumbile ya mwanadamu. Uislamu unatambua mahitaji ya kutimiza matamanio ya kimwili. Suluhisho la pili si la huruma hasa kukiwa na mapenzi baina ya wawili wapendanao. Suluhisho la mwisho ni dhidi kabisa na mafundisho ya Uislamu ambayo yanakataza zinaa wazi wazi. Kwa kuwa Uislamu uko dhidi ya utovu wa maadili, unafiki wa kitabia na talaka ila kwa dharura zisizoepukika, mbadala muafaka ni uke wenza.

 

3. Kimaumbile wanaume wana shauku kubwa zaidi kuliko wanawake na hivyo kuweza kuwamudu wake wengi.

 

4. Kimaumbile upo wakati mrefu ambapo mwanamke hawezi hutekeleza majukumu yake ya kindoa kwa mabadiliko ya kisaikolojia na kifiziolojia na kimwili kama wakati akibeba mimba, hedhi na nifasi. Katika hali ya kwanza wapo wanawake huwa hawataki kuonana hata na mwanaume na katika mbili za mwisho Uislamu umekataza mume kumuingilia mkewe.

 

5. Inajulikana kuwa wanawake ni wengi zaidi katika ulimwengu. Na vita ambavyo vinaendelea ulimwengu mzima vinawaacha wajane wengi zaidi na watoto wanaokosa mapenzi ya baba. Je, hawa wanawake wa ziada watimize uchu wao vipi? Ni maslahi ya kijamii kuwa wanawake wawe ni wenye kuolewa na hivyo kupata himaya ya kifamilia. Kawaida hawa wanawake huwa wana hamu ya kuolewa, nao hawana ila njia tatu mbele yao: Kuishi umri wao bila ya kuolewa; au walegeze hatamu wakiishi huku wakitumiwa na wanaume kwa kutimiza matamanio yao; au waolewe na waume wengine wenye uwezo wa kuwatazama. Suluhisho ni kuchukua msimamo wa tatu wa kuoa wake wengi.

 

6. Ipo shida kubwa sana Marekani na nchi za Bara Ulaya ambapo kumepigwa marufuku mume kuoa mke mwengine. Kwa sababu ya kanuni hiyo iliyo kinyume na maumbile ya mwanadamu utawakuta wanaume wengi wana vimada nje ya ndoa. Wanazaa nao watoto lakini hawana jukumu lolote la kuwatazama, kwao ni kutimiza haja yao ya kimapenzi tu.

 

7. Rusuli (‘Alayhimus Salaam) ambao ni kielelezo kwetu walikuwa na wake wengi hata katika Biblia kwa nini hatufuati mienendo yao kwani wao wamekuja na maisha yaliyo bora kabisa.

 

8. Wanawake wengi katika jamii tofauti ulimwenguni wanafadhilisha waume wenye wake wengi (tazama Campbell, D., In the Heart of Bantuland, uk. 160).

 

Mbali na hayo yote tuliyoyasema linajitokeza swali:

 

Kwa nini mwanamke asiolewe na waume wengi?

 

Katika hili tunasema yafutayo:

 

1. Ni hakika kuwa maumbile ya mwanamke kisaikolojia na fiziolojia ni tofauti na mwanaume. Kisaikolojia ni kuwa mwanamke anatosheka na mume mmoja. Kifiziolojia mwanamke hawezi kujimudu kuwa na wanaume zaidi ya mmoja kwa sababu ya mabadiliko ndani ya mwili wake.

 

2. Katika tamaduni zote, za zamani na sasa, uongozi wa nyumba (familia) ni wa mwanaume. Unaweza kufikiria katika familia ambayo ina kiongozi zaidi ya mmoja, nyumba hiyo itaendeshwa vipi? Ndio wahenga wakawa na msemo: "Fahali wawili hawakai kwenye zizi moja".

 

3. Mwanamke huyu ataweza vipi kuwaridhisha wanaume hao wote katika chakula na mapenzi. Tuseme kuwa utawagawia siku, mmoja wao anakuja na mke huyo yuko katika hedhi naye ana shauku ya juu sana, atafanyaje? Je, mke atachukua amri kutoka kwa nani?

 

4. Mke anayeolewa na mume zaidi ya mmoja, anaposhika mimba itakuwaje? Mtoto huyo atakuwa wa nani? 

 

Hivyo, mke kuolewa na mume zaidi ya mmoja ni jambo ambalo halikubaliki wala haliwezi kutekelezeka na hii yote ndio hikma ya Rabb Mtukufu Aliyetuumba na kutufahamu yanayotunufaisha na yanayotudhuru.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share