Kusafirisha Maiti Kutoka Mji Hadi Mji Mwengine Inajuzu?

 

Kusafirisha Maiti Kutoka Mji Hadi Mji Mwengine Inajuzu?

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

As-salaam Aleykum.

 

Nawashukuru sana nyote mnaotupa elimu kupitia mtandao, na  sifa zote njema ni za ALLAAH (SW).

 

In shaa Allaah nategemea kupata elima kuhusu kusafarisha Maiti kwa wale wanaokutwa na umauti mjini kisha kwenda kuzikiwa vijijini (nyumbani) kwao.

Na ni ipi hukumu ya wanaokwenda kwenye misafara hiyo. 

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

 

Hakika ni kuwa mas-ala haya hayana utata kwani haijapatikana katika maisha ya watangu wema waliopita kwamba walifanya shughuli hiyo ya kusafirisha maiti. Swahaba (Radhwiya Allaahu 'anhum) walikufa miji ya mbali – wapo wale waliokufa sehemu ya Shaam, Misri, Ethiopia, Iraq, Yemen, Morocco, Uturuki na sehemu nyingine za mbali. Ilikuwa ni aula kwao kusafirishwa katika sehemu walizotoka ambazo pia zilikuwa tukufu kama Makkah na Madiynah lakini hakuna hata mmoja aliyesafirishwa kuzikwa sehemu hizo.

 

Yapo makaburi ya Swahaba (Radhwiya Allaahu 'anhum) takriban 18,000 katika sehemu ya Shaam pekee.

 

Hili la kusafirisha maiti ni uzushi mpya ambao umejitokeza katika sehemu zetu tukiwaiga wasiokuwa Waislamu katika hilo au kufuata ada na desturi zetu ambazo sio nzuri. Mazishi ya Uislamu ni kuwa yanatakiwa yafanywe haraka iwezekanavyo ili akiwa maiti ni mwema afike kwa Allaah Aliyetukuka mapema na akiwa ni muovu basi muondoshe uovu huo nyumbani kwa haraka.

 

Anasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Harakisheni jeneza, akiwa ni mtu mwema, basi ni kheri mnayoitanguliza kwake, na akiwa ni kinyume chake (muovu) basi hiyo ni shari (mliyoibeba ambayo mnatakiwe haraka) muishushe kutoka katika shingo zenu". [Al-Bukhaariy na Muslim na wengneo].

 

Maamrisho hayo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) si tu kuharakisha kulipeleka jeneza kaburini, bali ni kuharakisha kuzifanya taratibu zote za kumuandaa maiti kwa ajili ya kumswalia na kumzika.

 

Kadhalika Hadiyth hiyo inajulisha umuhimu wa kumzika pale pale alipofariki maiti na si kumchelewesha kwa kumsafirisha eneo jingine au mji au nchi nyingine, kwani kufanya hivyo kutachelewesha kuzikwa maiti na hivyo kutagongana na maamrisho hayo ya kipenzi chetu.

 

Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) anasimulia:

 

"Katika vita vya Uhud Waislamu waliokufa walikuwa wakibebwa kupelekwa (katika makaburi ya) al-Baqiy’i. Lakini baadaye ikatangazwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kaamrisha nyinyi kuzika waliokufa pale walipofia/walipouliwa. Hapo ni wakati ambao mama yangu alikuwa tayari keshaweka maiti ya baba yangu na mjomba wangu juu ya ngamia. Na hapo wakachukuliwa na kurudishwa kwenda kuzikwa kule walipouliza." [Ahmad, Abu Daawuud na wengineo. Imethibitishwa usahihi wake na Shaykh al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz uk.25]

 

Pia tunapata kuwa ‘Abdur-Rahmaan bin Abi Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) alifariki katika sehemu iitwayo Waadul Habasha kiasi cha maili 12 kutoka Makkah na akasafirishwa kuzikwa Makkah. Na mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye ni ndugu na ‘Abdur-Rahmaan alipokwenda Makkah alizuru kaburi lake na akasema:

 

"Nimehuzunishwa kwa kuwa hakuzikwa kule alipofia" [Kainukulu al-Bayhaqiy, na Shaykh al-Albaaniy kaeleza usahihi wake kwenye Ahkaamul Janaaiz uk. 25]

Na kwa hili akasema Imaam an-Nawawiy:

 

"Ikiwa mtu kaacha katika wasia wake kuwa atakapokufa asafirishwe kuzikwa mahala pengine, wasia kama huo unapaswa kutofanyiwa kazi kwani unapingana na mafunzo ya kukatazwa kusafirishwa maiti. Na huu ndio msimamo sahihi na uliokubalika, ambao unawafikiwa na Wanachuoni wengi." [Imaam an-Nawawiy Al-Adhkaar]

 

Muislamu anafaa azikwe anapokufa kwani hakuna fadhila ya kupelekwa nyumbani au kijiji mlichotoka. Utapata kuwa warithi ambao wanafaa wabakishiwe mali huwa hawapati kwani mali nyingi inafujwa kwa ajili ya kusafirishwa au inatumika kwa wingi ambapo mazishi ya Kiislamu yanatakiwa yawe ni mepesi na yenye kutumia pesa ndogo. Hakika ni kuwa ikiwa kusafirisha kunakatazwa na wenye kulifuata pia kwenda nalo kijijini watakuwa na sehemu yako ya madhambi. Inatakiwa watu wasifanye hivyo ili hii ada mbaya iondoke.

 

Maiti inaweza kusafirishwa ikiwa pale alipokufa Muislamu hakuna Waislamu ambao wanaweza kumuosha, kumvisha sanda, kumswalia na baadaye kumzika. Ikiwa ipo shida hiyo basi maiti hiyo itasafirishwa sio kijijini kwao bali kijiji kilicho karibu na hapo alipokufa ili aweze kutimiziwa mambo hayo manne.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share