00-Wewe Pekee Tunakuabudu: Utangulizi

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

00-Utangulizi:

           

 

 

 

Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Rahma na amani zimshukie kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jamaa zake, na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum)  na wote waliotangulia kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Du’aa ni ‘ibaadah kwa dalili kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ﴿٦٠﴾

Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingika Jahanam wadhalilike. [Ghaafir: 60]

 

Na kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فِي قَوْلِهِ ((وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ )) قَالَ: ((الدُّعَاءُ هُوَ الْعِبَادَةُ)) وَقَرَأَ ((وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ )) إِلَى قَوْلِهِ: ((دَاخِرِينَ))

Amesimulia Nu’maan bin Bashiyr (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kauli yake [Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa] ((Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni)) Amesema: ((Du’aa ni ‘ibaadah)) kisha akasoma: ((Na Rabb wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni)) mpaka kauli Yake: ((daakhiriyn)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad – Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Na kwa kuwa lengo la kuumbwa kwa binaadamu ni kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema:

 

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. [Adh-Dhaariyaat: 56]

 

 

Ndio maana tunasoma Suwratul Faatihah katika Swalaah zetu zote, Suwrah ambayo imethibitisha kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa aina zote za Tawhiyd na tunakiri humo:

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾

Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada. [Al-Faatihah: 5]

 

 

Basi hakuna budi kwamba tunamhitaji Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa haja zetu zote kila wakati, bali tunamhitaji Yeye kuliko tunavyohitaji chakula, hewa, maji au vyovyote vinginevyo Anavyoturuzuku. Pia tunamhitaji Atuongoze katika njia iliyonyooka ili tutimize lengo la kuumbwa kwetu kuwa ni kumwabudu Yeye Pekee bila ya kumshirikisha ili tutakapokutana Naye Aakhirah Aridhike nasi. Hali kadhaalika binaadamu hana budi imsibu mitihani mbali mbali; maafa, maradhi, shida, dhiki, maovu na kila aina za shari kutoka kwa binaadamu na majini; kwa hiyo binaadamu hatoacha kumhitaji Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa du’aa ili Amuondoeshee madhara hayo au amkinge nayo kwani hakuna Muweza ila Yeye. Lakini Ameonya kutokuelekeza du’aa kwa asiyekuwa Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ﴿١٠٦﴾

Na wala usiombe badala ya Allaah visivyokufaa wala visivyokudhuru. Na ukifanya, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.

 

 

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ ۚ يُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۚوَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿١٠٧﴾

Na Allaah Akikugusisha dhara, basi hakuna wa kuiondosha isipokuwa Yeye. Na Akikutakia kheri, basi hakuna wa kurudisha fadhila Zake, Anasababisha kumfikia kwayo (fadhila Yake) Amtakaye katika waja Wake. Naye ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Yuwnus: 106-107]

 

Sababu za kukusanya makala za maudhui hii ya du’aa ni kutokana na kudhihirika makosa mengi yanayotendwa na ndugu zetu Waislamu katika kuomba du’aa ima kwa kumshirkisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) au kwa kuomba du’aa zisizothibiti katika mafunzo Swahiyh ya Dini, jambo ambalo ameonya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ عَائِشَةُ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ:  ((منْ أَحْدَثَ في أَمْرِنَا هذا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدٌّ))

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayezusha [kitu] katika mambo yetu haya [katika Dini yetu] kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Juu ya hivyo kumzulia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa uzushi ni dhambi kubwa itakayompeleka Muislamu katika makazi ya Moto:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم): ((مَنْ كَذَبَ عَلَيَّ مُتَعَمِّدًا فَلْيَتَبَوَّأْ مَقْعَدَهُ مِنْ النَّارِ)) 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake Motoni)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Pia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitanguliza khutbah zake kwa kutoa maonyo hayo:

 

 ((إِنَّ أَصْدَقَ الْحَدِيثِ كِتَابُ اللَّهِ وَأَحْسَنَ الْهَدْيِ هَدْيُ مُحَمَّدٍ وَشَرَّ الأُمُورِ مُحْدَثَاتُهَا وَكُلَّ مُحْدَثَةٍ بِدْعَةٌ وَكُلَّ بِدْعَةٍ ضَلاَلَةٌ وَكُلَّ ضَلاَلَةٍ فِي النَّارِ))  

((Hakika mazungumzo bora ni kitabu cha Allaah [Qur-aan] na mwongozo mbora kabisa ni mwongozo wa Muhammad, na jambo la ovu kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya [katika dini] ni bid'ah na kila bid'ah ni upotofu, na kila upotofu ni Motoni)) [An-Nasaaiy]

 

Tunatumai na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ajaalie makala hizi ziwe zenye kuwanufaisha ndugu zetu Waislamu na ziwe ni sababu ya kuepukana na shirki pamoja na du’aa za uzushi na badala wabakie katika amani na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kutokumshirikisha na pia yafuatwe mafunzo Swahiyh ya Sunnah za Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika ‘ibaadah hii tukufu ya kuomba du’aa. Hatuna tawfiyq isipokuwa kutoka kwa Allaah, Kwake tunatawakali na Kwake tunarejea kutubia.

 

 

 

Share