Anaweza Kutoa Mimba Msichana Aliyebakwa?

 

 

SWALI:

Asalam aleikum,

Kwa mfano msichana amebakwa na kupachikwa mimba je anaweza kuitoa mimba ile na kama sivyo dini yasemaje? ahsanteni

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunamshukuru Allaah ambaye kwa neema Zake yanatimia kila yalio mema na mazuri. Na tunamuomba Atupe yaliyo mema hapa duniani na kesho Akhera.

Hili ni jambo ambapo limekuwa la kawaida katika nchi za Magharibi na sasa limekuwa la kawaida hata katika nchi za Kiafrika. Kwanza inatakiwa ifahamike kuwa msichana aliyefanywa tendo hilo hana dhambi na heshima yake iko palepale na haifai kwa watu kuanza kumkebehi kwa kitendo hicho kwani hakuwa ni mwenye kutaka kwa hiari yake bali ametendeshwa nguvu. Na Allah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanatueleza kuwa mwenye kufanyiwa kitendo chochote kwa nguvu huwa hana makosa yoyote. Allah Anasema kuhusu kutenzwa nguvu katika kukufuru:

“Anayemkataa Mwenyezi Mungu baada ya kuamini kwake - isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya Imani, lakini aliyekifungulia kifua chake kukataa - basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ipo juu yao, na wao watapata adhabu kubwa (16: 106).

 

Katika hali kama hiyo ya msichana ambaye amefanyiwa kitendo hicho, baadhi ya Maulamaa wanaonelea kuwa anaruhusiwa aitoe hiyo mimba kwani ikibakia mpaka mtoto kuzaliwa inaweza kumletea shida ya kila wakati kukumbuka kitendo hicho alichofanyiwa na hivyo kidonda kitaendelea kuwepo na kumwathiri kisaikolojia, kifikra na athari nyenginezo. Na ni bora aende asafishwe kwa daktari aliyebobea (mtaalamu) katika masuala hayo siku ile ile baada ya kujimudu kuweza kufanya hivyo. Hii ni kwa mujibu wa msingi wa Fiqihi unaosema kuchagua Akhaffudh Dhwarayn (Dhara lililo dogo zaidi katika mambo mawili yenye madhara). Na ikiwa amedhania ya kuwa hakutunga mimba kisha akafahamu kuwa ana mimba itabidi aitoe kabla ya kufika kwa miezi minne wakati ambapo mtoto hutiwa roho.

Pia ni muhimu sana kwa msichana huyo kwenda kupima ukimwi kwani huenda akawa ameambukizwa na yule aliyembaka.

Lakini rai ya Maulamaa tunayoiona ina nguvu zaidi, ni kuwa mwanamke hatakiwi kuitoa mimba kwa tendo kama hilo, kwani si makosa yake na si makosa ya kiumbe hicho. Hivyo, endapo mwanamke huyo atafanya subira na kulea mimba hiyo na akaamua kubaki nayo, basi hiyo ni bora zaidi kwani kumbe hicho hakina makosa yoyote na hakihusiki kwa lolote katika yaliyojiri.

Tufahamu kuwa kila kiumbe anayezaliwa anakuwa ni Muislam, na huenda huyo mtoto wa tendo la zinaa akawa Muislam bora sana kuliko wengi. Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aallihi wa sallam) anasema: "Kila mtoto anazaliwa katika hali ya fitwrah (maumbile ya asli; Uislam)..." (al-Bukhaariy). 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share