Kumlingania Mtu Aingie Katika Uislamu Kwa Kudanganya Inajuzu?

SWALI:

Assalam aleykum.nashukuru kupata fursa hii ya kuuliza..Je sheikh naruhusika kudanganya kusema kwamba mimi kabla nilikuwa mkristo na nikasilimu baada ya kuona kasoro za ukristo.lengo ili nipate kumuingia rafiki wangu wa kikristo na niweze kumsilimisha kwa kupitia hikma hiyo..Je naruhusika au laa? (ukweli ni kwamba nimezaliwa muislam

 



 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Miongoni mwa sifa katika sifa nyingi za Muumini na maadili yake matukufu ni kusema ukweli popote alipo. Ukitoka katika sifa ya ukweli na ukawa muongo basi unaingia katika nifaki. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَكُونُواْ مَعَ الصَّادِقِينَ))

((Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli)) (9: 119).

Na amesema Aliyetukuka:

وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ))))

((Na wasemao kweli wanaume na wanawake)) (33: 35).

Na Mtume Wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia yafuatayo:

1.  Na imepokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika ukweli unamuongoza mtu katika wema na wema unampeleka mtu Peponi. Na hakika mtu huendelea kusema ukweli mpaka akaitwa mkweli mbele ya Allaah. Na hakika uongo unampeleka mtu katika uchafu na uchafu unampeleka mtu Motoni. Na mtu huendelea kusema uongo mpaka akaandikwa kuwa ni muongo mbele ya Allaah” (Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy).

     Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa je, Muumini anaweza kuwa muongo akasema: “Hapana”.

3.  Pia kisa cha wale Maswahaba watatu waliokosa kwenda katika Vita vya Taabuk wakiwa ni Ka‘ab bin Maalik, Muraarah bin ar-Rabi‘ al-‘Umariy na Hilaal bin Umayyah al-Waaqifiy (Radhiya Allaahu ‘anhum). Wanafiki walikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa nyudhuru zao naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawasamehe lakini hawa wakweli wakaambiwa wangojee mpaka Allaah Ateremshe hukumu yake. Ndio aya 117–119 za Suratit Tawbah zikateremshwa kukubaliwa toba yao. Soma kisa hiki kwa kirefu katika Riyaadhus Swaalihiyn, Hadiyth nambari 21.

 

Katika Da‘wah haifai kumwanbia mtu uwongo ili apate kusilimu ikiwa huwezi kuutembeza Uislamu kwa uzuri ulio nao wenyewe basi hujakuwa Da‘iyah (Mlinganiaji) wa kuweza kufanya shughuli hiyo. Na jambo hili haliingii katika akili ya mtu kwani siku moja huenda akajua kuwa wewe umemdanganya hivyo kuutia dosari Uislamu na huenda hata huyo bwana akaanza kuuchukia.

 

Ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) alikuwa ni mkweli kabisa katika kila jambo lake na mbali ya kuwa Maquraysh walikataa mwanzoni kumfuata lakini walikuwa wanamjua kwa jina la as-Swaadiq al-Amiyn (Mkweli, Muaminifu), nasi lazima tuige tabia zake hizo nzuri. Na katika jambo hili la ukweli hata wasiokuwa Waislamu wengi wameandika vitabu vingi kumsifia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share