Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Makosa Ya Kunyanyua Viungo Vyenye Kusujudu Wakati Wa Kusujudu

 

Miongoni Mwa Makosa Ya Wenye Kuswali

 

Kunyanyua Moja Ya Viungo Vyenye Kusujudu Wakati Wa Kusujudu

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa:

 

“Mtu amenyanyua kiungo kimoja katika viungo vya kusujudia (mfano utaona mtu kasujudu kisha miguu iko hewani inaelea au mguu mmoja uko juu ya mwenzake), je, inabatilisha Swalaah?”

 

 

Akajibu (Rahimahu Allaah):

 

“Kwa udhahiri ni kwamba, anaponyanyua mtu kiungo chake katika Sujuwd yote (wakati anaposujudu), basi Sujuwd yake inakuwa ni batili. Na inapobatilika Sujuwd yake, inabatilika Swalaah yake.

 

Ama ikiwa kunyanyua kwake (kiungo) kwa muda mfupi tu mfano anaukuna mguu wake kuukuna mwengine (unaowasha) kisha akaurudisha chini, basi nataraji hakuna juu yake ubaya.”

 

 

[Liqa-aat Al-Baab Al-Maftuwh - Liqaa Al-Baab Al-Maftuwh 25]

 

 

Na kadhaalika akasema (Rahimahu Allaah):

“Na Sujuwd (kusujudu) juu ya viungo hivi saba, ni waajib katika kila hali ya kusujudu. Kwa maana kuwa haijuzu (mtu) kunyanyua kiungo katika viungo vyake wakati wa kusujudu kwake. Si mkono, wala mguu, wala pua, wala kipaji cha uso, wala chochote kile katika hivyo viungo saba. Na atakapofanya hivyo katika Sujuwd zote, basi pasi na shaka ni kuwa Sujuwd yake haisihi; kwa sababu kutakuwa kumepungua kiungo miongoni mwa viungo vinavyopasa kusujudu juu yake.

 

Na ama ikiwa ni katikati ya Sujuwd, kwa maana mtu anawashwa mguu wake, mfano (akaunyanyua mguu mmoja) akaukuna mguu wake mwengine; hapo panahitaji mtazamo. Kunaweza kusemwa: Kwamba Swalaah yake haisihi kwa sababu kaacha nguzo hiyo katika baadhi ya Sujuwd.

 

Na kunawezwa kusemwa: Inamtosheleza, kwani mazingatia ni kwa ujumla na kwa wingi, inapokuwa kwa ujumla na kwa wingi, kwamba yeye ni mwenye kusujudu juu ya viungo saba; basi humtosheleza. Na juu ya hili panahitaji kuwepo akiba; kwamba asinyanyue chochote kile na afanye subira hata ikiwa atapatwa na muwasho mfano katika mkono wake, au katika paja lake, au katika mguu wake, asubiri hadi atakaposimama kutoka katika Sujuwd.”

 

 

[Ash-Sharh Al-Mumti’, mj. 3. Uk. 37]

 

 

Share