Skip navigation.
Home kabah

Kutengeneza Au Kupunguza Ndevu Kunaharibu Swawm?

 

 

SWALI:

 

Asalam Aleykum Warahmat Taalah wa barakatuhu,

Kwanza ni kuwatakia kheri na baraka za mwezi huu mtukufu wa ramadhani, na ALLAH atukubalie saumu zenu, Inshaa ALLAH, Swali ni kuwa, ikiwa mtu atazisawazisha ndevu kwa mkasi, siyo kunyoa au kupunguza sana na yeye amefunga mwezi hu wa ramadhani, jee saumu yake imeharibika??

 



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa kaka yetu ambaye ameuliza swali hili ambalo linampatia mtu sifa ya uume wake.

Mtume wa Allah (s.a.w.) amehimiza sana kuhusu kuacha ndevu na kupunguza masharubu katika Hadithi ambazo zimenukuliwa na Maimamu kama Al-Bukhari, Muslim, Abu Dawud, At-Tirmidhy, Maalik na wengineo. Kueka ndevu inampatia mtu heshima katika jamii na ni ishara ya uanaume.

Ndevu kama nywele ni lazima zikirimiwe na kuwekwa katika hali nzuri kwa kuchanwa na kupakwa mafuta. Haifai kuwa na ndevu kisha zikawa haziangaliwi inavyotakiwa. Katika mas-ala ya kupunguza ndevu ipo Hadithi ya Ibn ‘Umar (r.a.) ambayo inasema kuwa alipokuwa akimaliza ‘Umrah au Hijjah basi huzishika ndevu zake kwa mkono wake na chochote kilichozidi hukipunguza kwa kukata sehemu hiyo ya ndevu iliyozidi saizi ya mkono (Al-Bukhari na Maalik).

Kwa kupima saizi hiyo kwa mkono wangu nimeona kuwa inafika sentimita 7.5 au inchi 3. Kwa hivyo mwanamume akiwa atapunguza hafai kupunguza chini ya kipimo hicho. Na lau ikiwa ndevu za mmoja wetu hazipo sawa kuna zile ambazo ni ndefu na fupi basi inafaa kuzikirimu na kuzitizama kwa kuziweka sawa.

Kusawazisha ndevu au kupunguza hakumfungulisha mtu Swawm yake.

Na Allah Anajua zaidi.