115-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Baqarah Aayah 115: وَلِلَّـهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ ۚ فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ

 

 

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

 

Al-Baqarah Aayah 115: Na Mashariki na Magharibi ni ya Allaah; basi popote mnapogeuka...

 

 

وَلِلَّـهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ ۚ فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿١١٥﴾

115. Na Mashariki na Magharibi ni ya Allaah; basi popote mnapogeuka kuna Wajihi wa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote.

 

Sababun-Nuzuwl:

 

Aayah hii imeteremka pale Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa akiswali akiwa juu ya mnyama wake, alipokuwa akirudi kutoka Makkah kuelekea Madiynah, basi hapo ikateremshwa: “basi popote mnapogeuka kuna Wajihi wa Allaah.” [Amehadithia Ibn ‘Umar (رضي الله عنه) amepokea At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ahmad na Ibn Jariyr. Na amesema At-Tirmidhiy ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Faida: 

 

Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  amesema: “Sehemu ya kwanza ya Aayah imefutwa hukmu yake kuhusu Qiblah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipohamia Madiynah ambako walikuweko wakaazi Mayahudi, aliamrishwa kuelekeza uso wake Baytul-Maqdis (Palestina). Mayahudi wakafurahi na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaelekeza uso wake huko kiasi miezi kumi. Lakini Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akipenda kuelekeza uso wake Qiblah cha Nabiy Ibraahiym (Al-Ka’bah Makkah) na alikuwa akitazama tazama mbingu kuomba, basi Allaah Akateremsha: “Kwa yakini Tumeona (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) unavyogeuza geuza uso wako mbinguni. Basi Tutakuelekeza Qiblah unachokiridhia…” (2: 144) [Tafsiyr Ibn Kathiyr na kwa riwaayah nyinginezo katika Al-Bukhaariy na wengineo]

 

Share