Kupokea Mchango Kutoka Kwa Makafiri Kwa Ajili Ya Msikiti Inajuzu?


SWALI:

Assalaam Alaykum,

Nashukuru sana kwa majibu mazuri kwa swali langu lililopita, Mwenyezi Mungu atawalipa kwa jihada mnazozionyesha inshaalah. Naomba pia mnifahamishe kama inajuzu kupokea michango kutoka kwa makafiri kwa ajiri ya ujenzi wa misikiti na hata madrasa. Wabillah Tawfiq.

 



 

JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.



Shukran kwa swali lako hilo ambalo ni nyeti hasa wakati huu wetu wa sasa baada ya Septemba 11, 2001. Imekuwa sasa kwa sababu ya kufungwa hasa katika Afrika Mashariki Vyama visivyokuwa vya Kiserikali vya Kiislamu (NGO) kwa kisingizio cha ugaidi, vyama vya Kikristo hasa kutoka Marekani ndivyo vinasaidia ujenzi wa Misikiti, Madrasa na hata kulipa Maimamu na walimu wa Madrasa kwa malengo yao hasa.

Je, yumkinika kwa kila mwenye akili kuwa watu hawa ambao wanawaua na kuwanyanyasa ndugu zetu katika Imani ikiwa ni Afghanistan, au Iraq, au Palestina (kwa kusaidia serikali ya Kizeyuni), au Kashmir (kwa kusaidia serikali ya Kibaniyani), au ni Chechnia kisha wakatupendelea sisi mema na mazuri? Jibu ni la!

Hivyo, malengo yao ni yepi kwa sababu sasa wanasaidia hata kuandaa Mawlid ya Mtume (Swalla-Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili kuwapatia nguvu watu wanaopinga Sunnah za kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla-Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) dhidi ya wenye kuunga na kuitetea Sunnah.

Mas-ala hayo yana jibu la moja kwa moja kutoka kwenye Qur-aan ambapo Alllah Aliyetukuka Anasema: “Haiwi kuwa makafiri ndio waamirishe Misikiti ya Allaah, hali wanajishuhudishia wenyewe ukafiri. Hao ndio vitendo vyao vimeharibika, na katika moto watadumu. Hakika wanao amirisha Misikiti ya Allaah ni wale wanao muamini Allaah, na Siku ya Mwisho, na wakashika Swalah, na wakatoa Zakah, na wala hawamchi isipokuwa Allaah. Basi huenda hao wakawa katika waongofu” ( – 18).

Hizi aya zipo wazi kabisa ya kuwa haifai Misikiti kuamirishwa na watu ambao ni makafiri. Na ujenzi wa Msikiti si lazima uwe mkubwa na wa mawe. Munaweza kuanza kulingana na uwezo wenu mpaka mtakapopata nafasi ya kuujenga kwa vizuri na kuupanua. Mtume Muhammad (Swalla-Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alijenga Msikiti wake kwa udongo, vigogo vya mitende na majani yake kama paa. Hivyo, tusiwe ni wenye kughurika kwa visenti vichache ambavyo vitatupeleka vibaya hapa duniani na Kesho Akhera.

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share