187-Asbaabun-Nuzuwul: Mmehalalishiwa Usiku Wa Swiyaam Kujamiiana Na Wake Zenu...

 أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

Al-Baqarah Aayah 187: Mmehalalishiwa Usiku Wa Kufunga Swiyaam Kujamiiana na wake zenu...

 

 

 أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ ۚ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ ۗ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ ۖ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ ۚ وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ ۗ تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَقْرَبُوهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿١٨٧﴾

187. Mmehalalishiwa usiku wa kufunga Swiyaam kujamiiana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu na nyinyi ni vazi kwao. Allaah Anajua kwamba nyinyi mlikuwa mkijifanyia khiyana nafsi zenu, hivyo Akapokea tawbah yenu na Akakusameheni. Basi sasa waingilieni na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku). Kisha timizeni Asw-Swiyaam mpaka usiku. Na wala msiwaingilie hali ya kuwa nyinyi wenye kukaa i’tikaaf Misikitini. Hiyo ni mipaka ya Allaah basi msiikaribie. Hivyo ndivyo Allaah Anavyobainisha Aayaat (na hukmu) Zake kwa watu wapate kuwa na taqwa.

 

Sababun-Nuzuwl: 

Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه)   kwamba: Maswahaba wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) walipokuwa wakifunga Swawm kisha ikatokea kuwa walale bila ya kufuturu (Magharibi), walikuwa huendelea kufunga Swawm (usiku wote na mchana) mpaka kufike jioni tena (Magharibi). Siku moja Swahaba Qays Ibn Swirmah alikuwa amefunga Swawm. Ulipofika wakati wa kufuturu alimwendea mkewe akamuuliza: Je, una chakula? Akajibu: Hapana! Lakini nitajaribu kukupatia. Na alikuwa akifanya kazi ngumu. Akaghilibiwa na usingizi na alipokuja mkewe (na chakula) alimkuta ameshalala. Akasema: Ole wako, umelala! Ilipofika mchana wa siku ya pili, alzimia. Yakatajwa hao kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) , hapo Aayaah hii ikateremshwa: Mmehalalishiwa usiku wa kufunga Swiyaam kujamiiana na wake zenu…” wakafurahi mno! Na ikateremka: “Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku). Kisha timizeni Asw-Swiyaam mpaka usiku” [Al-Bukhaariy kutoka kwa Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه)].  Na pia hukmu ya kufunga Swawm ilipotolewa Waislamu walijizuia kujamiana na wake zao mwezi mzima, lakini baadhi ya watu walikuwa wakifanya khiyana (kuvunja shariy’ah) basi Allaah Akateremsha: Allaah Anajua kwamba nyinyi mlikuwa mkijifanyia khiyana nafsi zenu, hivyo Akapokea tawbah yenu na Akakusameheni. Basi sasa waingilieni na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu...”

 

Na Sababun-Nuzuwl kuhusu kauli ya Allaah: Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe…. ni kwa sababu walikuwa baadhi ya Maswahaba wanaendelea tu kula huku wakiwa wamefunga nyuzi (kamba) mbili mguuni; mmoja mweusi na mmoja mweupe mpaka ibainike kuzitofautisha kwake nyuzi hizo. Allaah Akateremsha: (Ufafanuzi wa): mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku)”. [Al-Bukhaariy na Muslim; Hadiyth ya Sahl bin Sa’d  (رضي الله عنه)].

 

Faida: Maswahaba walitatanishwa na kushindwa kuelewa maana ya neno uzi mweupe kutokana na uzi mweusi”.  ‘Adiyy bin Haatim (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Ilipoteremshwa Aayah: mpaka ubainike kwenu uzi mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku).”, Nilichukua uzi mmoja mweupe na mmoja mweusi nikaweka chini ya mto wangu lakini haikunibainikia. Nikamwendea Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) asubuhi nikamwelezea. Akasema: “Hakika hiyo (imekusudiwa) ni kiza cha usiku na weupe wa Alfajiri” [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

 

Share