Skip navigation.
Home kabah

Je, Inafaa Kuibia Serikali Mita Za Taa?

SWALI

assalaam alaikum nashkuru sanaa kwa kunijibu maswali yangu mengi alla akulipenl ila nna tatizo jengine mimi kama mnavojua huku kwetu zanzibar matumizi ya umeme ni madogo kwenye nyumba zetu lakini hubambikiziwa bili kubwaa pengine kwa mwezi utalipa hata sh 30000 sasakuna fundi ataibana mita nitalipa sh 7000tu kwa mwezi jee mashekh wetu kisheria inafaa?

 



JIBU:

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad:

 

Tunashukuru kuona kwamba ndugu zetu wako katika khofu ya kujiepusha na maovu na kuchuma dhambi na hivyo ndivyo anavyotakiwa Muislamu awe kila anapokosa ajirudi.

 

Lakini kuna dhambi ambazo hugeuka kuwa ni dhulma nazo ni baina ya mja na Mola wake kama kumshirikisha Allaah سبحانه وتعالى. Na zilizo baina ya binaadamu na binaadamu mwenzake. Na  Zilizo baina ya mja na Mola wake, huenda Allaah سبحانه وتعالى Akamsamehe pindi akiomba maghfira na tawbah kabla ya kufariki huyo mtu au kabla ya jua kuchomoza upande wa Magharibi. Ama dhambi zilizo baina yake na baina ya mwenzake hizi huwa ni haki za huyo mwenzake, na haifai kabisa kuchukua haki ya mtu kwa aina yoyote  kama kumuonea au kumvunjia heshima yake au kumchukulia mali yake na kadhalika, kama tunavyopata mafundisho katika Hadiyth hizi ifuatayo:

  ‏ ‏عن ‏ ‏أبي هريرة رضي الله عنه ‏ ‏أن رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏قال ‏‏ (( أتدرون ما المفلس))  قالوا المفلس فينا يا رسول الله من لا درهم له ولا متاع قال رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏‏)) المفلس من أمتي من يأتي يوم القيامة بصلاته وصيامه وزكاته ويأتي قد شتم هذا ‏ ‏وقذف ‏ ‏هذا وأكل مال هذا وسفك دم هذا وضرب هذا فيقعد ‏ ‏فيقتص ‏ ‏هذا من حسناته وهذا من حسناته فإن فنيت حسناته قبل أن ‏ ‏يقتص ‏ ‏ما عليه من الخطايا أخذ من خطاياهم فطرح عليه ثم طرح في النار)) ألترمذي

 Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Mnamjua nani aliyefilisika))  Wakasema (Maswahaba): Aliyefilisika ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirham au mali. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Aliyefilisika katika umma wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyaamah na Swalah zake, Swawm zake na Zakah zake, lakini atakuja akiwa amemtukana huyu, amemtuhumu huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu na amempiga huyu, yatachukuliwa mema yake na kulipwa wale aliowadhulumu. Yatakapomalizika mema yake kabla ya kufidia madhambi aliyowakosea wenzake, zitachukuliwa dhambi za wale aliowakosea kisha atajaliziwa yeye na mwishowe atakuwa ni wa kutupwa motoni)) [At-Tirmidhiy]

Kitendo hicho cha kubana mita za umeme wa serikali ili itembee polepole na uweze kulipa gharama ndogo, ni kitendo cha wizi na Allaah سبحانه وتعالى Amelikataza jambo hili kwa makatazo makali kabisa hata Ametoa hukmu yake kuwa ni kukatwa mkono:

Anasema Allaah سبحانه وتعالى  

 وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُواْ أَيْدِيَهُمَا جَزَاء بِمَا كَسَبَا نَكَالاً مِّنَ اللّهِ وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ  

((Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, hayo ni malipo ya waliyoyachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima)) [Al Maaidah: 38]

Nayo pia huwa ni dhulma pindi hatorudisha mtu haki hiyo aliyochukua. Na inabidi arudishe haki hiyo kabla ya mauti kumfika binaadamu au sivyo itabidi ahesabiwe Akhera kama tulivyoona katika Hadiyth hiyo ya juu.

Ikiwa hakuna uwezekano wa kumrudishia mtu haki yake, kama kuwa na khofu kuwa labda itamletea madhara zaidi, basi anatakiwa Muislamu aombe  Maghfira na Tawbah, kisha baada ya kuacha kitendo hicho kabisa, azidishe mema yake na amfanyie wema yule mwenzake aliyemdhulumu na kumuombea maghfira na du'aa. Vile vile mnasihi na huyo fundi maana naye anashiriki kwenye wizi huo, na ni wangapi anaowasaidia kwenye wizi huo?? Mfikishie nasaha na mwambie amche Mwenyeezi Mungu.

Na Allah Anajua zaidi.