30-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Kutawassal Kwa Uradi Wa: Wasiylatush-Shaafiy

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah

 

30-Kutawassal Kwa Uradi Wa: Wasiylatush-Shaafiy

 

 

 

 Wasiylatush-Shaafiy  وسيلة الشافي

Au:

Wasiylatun-Nabhaaniy  - وسيلة النبهاني

 

 

Uradi huu pia ni maarufu sana katika jamii. Umekusanya Majina na Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) nyingi, lakini ndani yake kuna makosa makubwa mno ya 'Aqiydah pale inaposema:

وحبذا محمد هادينا لولاه ما كنا ولا بقينا

Wahabadhaa Muhammadun haadiynaa lawlaahu maa kunnaa walaa baqaynaa.

“Na uzuri ulioje! Kwa Muhammad tumehidika, bila yeye tusingekuweko wala tusingebakia.”

 

 

Hivyo ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na uumbaji Wake kwani Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Al-Khaaliq (Muumbaji), Naye Ndiye Al-Qayyuwm (Mwenye kusimamia mambo ya waja Wake) na Naye Ndiye Mwenye kutoa tawfiyq ya Alhidaayah kwa waja Wake, Naye Ndiye Al-Wakiyl (Mdhamini Mwenye kutegemewa na waja Wake). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekariri katika Aayah kadhaa kwamba Yeye Ndiye Muumbaji wa kila kitu, mfano kauli Zake Allaah ('Azza wa Jalla):

 

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ﴿٦٢﴾

Allaah ni Muumbaji wa kila kitu, Naye juu ya kila kitu ni Mdhamini. [Az-Zumar: 62]

 

Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ رَبُّكُمْ وَرَبُّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ﴿٨﴾

 Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Anahuisha na Anafisha; Rabb wenu na Rabb wa baba zenu wa awali. [Ad-Dukhaan: 8]

 

Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٥٤﴾

Tanabahi! Uumbaji ni Wake Pekee na kupitisha amri. Tabaaraka Allaah! (Amebarikika Allaah) Rabb wa walimwengu. [Al-A’raaf: 54]

 

‘Ulamaa wa Al-Lajnah Ad-Daaimah walipoulizwa kuhusu uradi huu wametoa Fatwa yao kwamba:

 

“Ama kuhusu Wasiylatush-Shaafiy wa An-Nabhaaniy yamedhihirika mambo mawili:

وحبذا محمد هادينا

Wahabadhaa Muhammadun haadiynaa

 

Kwamba Allaah Ametuhidi kupitia Nabiy wetu na Rasuli wetu  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), jambo ambalo lina aina ya sifa iliyopinduka mipaka.

 

La pili ni kauli:

 

اللهم اغفر لي ولعبدك المذنب الضعيف يوسف بن إسماعيل النبهاني مؤلف هذا الكتاب، وأدخلني وإياه الجنة من غير سابقة عذاب، وأوصل إلى روحه ثواب هذه الفاتحة. وبعد قراءتها يقول... إلخ

 Allaahumma-Ghfir-liy wa li’Abdika al-mudhnibi adhw-dhwa’iyfi Yuwsufa bni Ismaa’iyla An-Nabhaaniy muallifi haadhal-kitaabi, wa Adkhil-niy wa iyyaahu Al-Jannata min ghayri saabiqatin ‘adhaab, wa Awswil ilaa Ruwhihi thawaaba haadhihi Al-Faatihati!

 

“Ee Allaah, nighufurie pamoja na mja Wako mwenye dhambi, aliye dhaifu, Yuwsuf bin Ismaa’iyl An-Nabhaaniy, mwandishi wa kitabu hiki na niingize pamoja naye Jannah bila ya kutangulia adhabu na Mfikishie roho yake thawabu za hii Al-Faatihah! (inasomwa Suwratul Faatihah kisha inasemwa kadhaa wa kadhaa …)

 

Hakuna shariy’ah ya kuwasomea Qur-aan waliokufa na kuwaombea thawabu zake ziwafikie, kwa sababu hakuna dalili ya hilo. Na An-Nabhaaniy amefariki mwaka 1350H ana majanga katika ‘Aqiydah na ana uvukaji mipaka wa bid'ah na shirki katika vitu alivyoviandika vingine ambavyo ‘Ulamaa wametahadharisha. Na miongoni mwa ‘Ulamaa aliyemradi ni Shaykh Mahmuwd Shukriy Al-Aaluwsiy (Rahimahu-Allaah) katika kitabu chake: ‘Ghaayat Al-Amaaniy fiy ar-radd ‘alaa An-Nabhaaniy’. 

 

Basi inampasa Muislamu ailinde Dini yake, na ajiepushe na vitu vilivyotungwa kama hivi kwa sababu ya kuweko ndani yake shari kuu ya shirki na kuhusisha waliofariki, na yote haya yanaangamiza misingi ya Dini na asasi ya Tawhiyd.  [Al-Lajnah Ad-Daaimah lil-Buhuwth wal-Iftaa, Fatwa namba (16863)]

 

 

Na jambo hilo la kusoma Suwratul-Faatihah kama kifungulizi cha du’aa ni miongoni mwa bid’ah zilizozushwa na Masufi na Mashia. Huvutwa hiyo Al-Faatihah “Al-Faaaaatihah!” kisha husemwa mfano: “Biniyyaatil-matwluwb ……” (kwa niyyah ya kuombwa jambo…) ikiwa kama ndio tawassul!

 

 

Tahadhari ee ndugu Muislamu!  Hakuna dalili ya kuthibitisha tawassul hii kamwe! 

 

 

 

Share