Idadi Ya Watoto Wa Nabiy Aadam (عليه السلام)

 

 

Idadi Ya Watoto Wa Nabiy Aadam  (عليه السلام)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Nabii Aadam  alayhisaalaam pamoja na mama yetu Hawwaa   walizaa watoto wangapi?

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza tufahamu kuwa Qur-aan na Sunnah hazikutoa maelezo yoyote kuhusiana na idadi ya watoto wa Aadam na Hawwaa (‘Alayhimas Salaam), au kuwa walikomea kwa Haabiyl na Qaabiyl.

 

‘Ulamaa wanaeleza kuwa Aadam alipata watoto wengi, na Qur-aan inadhihirisha hilo kwa dhahiri yake: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا ﴿١﴾

“Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana (haki zenu kwa kuunga) undugu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwachunga daima.” [An-Nisaa: 1]

 

Amesema Ibn Jariyr Atw-Twabariy (Rahimahu-Allaah):

“Imetajwa kuwa Hawwaa alimzalia Aadam (‘Alayhis Salaam) matumbo mia na ishirini. Wa mwanzo alikuwa Qaabiyl na pacha wake wa kike Qaliyma, na wa mwisho wao alikuwa ‘Abdul-Mughiyth na pacha wake wa kike Amatul-Mughiyth.

 

Ama Ibn Is-haaq imetajwa kutoka kwake kuwa wote aliowazaa Hawwaa na Aadam ni watoto wa kiume ishirini na wa kike ishirini kutokana na matumbo ishirini. Na akasema: Imetufikia baadhi ya majina yao na mengine hayakutufikia. [Taariykh Al-Ummam wal Muluwk, mj. 1, uk. 98]

 

Amesema vilevile Al-Haafidhw Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah):

“Wametaja wana historia kwamba Aadam (‘Alayhis Salaam) hakufariki hadi alipoona katika kizazi chake – watoto na wajukuu wake - wamefikia idadi ya laki nne. Na Allaah Anajua zaidi. [Al-Bidaayah wan Nihaayah, mj. 1, uk. 96]

 

Kadhaalika ‘Ulamaa wanaeleza kuwa Aadam (‘Alayhis Salaam) alikuwa anapata watoto mapacha; kila tumbo ni mtoto wa kiume na wa kike, kisha akawa anawaozesha mtoto wa kiume wa tumbo moja kumuoa mtoto wa kike wa tumbo lingine. Yaani pacha wa kiume humuoa pacha wa kike wa kaka yake.

 

Anasema Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah):

“Imesimuliwa na kunukuliwa na wengi wa ‘Ulamaa waliotangulia, kwamba Allaah Alimwamrisha Aadam (‘Alayhis Salaam) awaozeshe mabint zake kwa watoto wake wa kiume kwa mlango wa dharura. Lakini (‘Ulamaa) hao wakaeleza kuwa, pacha ya mwanamme na mwanamke walikuwa wakizaliwa kutokana na kila mimba; kwa hivyo, akawa anamuozesha bint wa mimba ya mwanzo kwa mvulana wa mimba iliyofuatia.

 

Dada yake Haabiyl alikuwa havutii na dada yake Qaabiyl alikuwa akivutia sana. Qaabiyl akataka lazima amuoe dada yake wa tumbo moja – kwa sababu alikuwa anavutia sana - na hakutaka kumwachia huyo dada yake aolewe na kaka yake, lakini Aadam (‘Alayhis Salaam) hakuridhia na akasisitiza watoe kafara, na ambaye kafara yake itakubaliwa na Allaah, basi ndiye atakayemuoa huyo dada yao (aliyekuwa mzuri anayevutia).

 

Wakatoa kafara, lakini kafara ya Qaabiyl haikukubaliwa. Kisa hicho kimetajwa katika Kitabu cha Allaah. [Tafsiyr Ibn Kathiyr, mj. 3, uk. 82]

 

Kafara ya Haabiyl ilipokubaliwa na ya nduguye Qaabiyl kutokubaliwa, Qaabiyl alighadhibika na kuamua kumuua nduguye.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuhusiana na kisa hicho:

 

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ ابْنَيْ آدَمَ بِالْحَقِّ إِذْ قَرَّبَا قُرْبَانًا فَتُقُبِّلَ مِنْ أَحَدِهِمَا وَلَمْ يُتَقَبَّلْ مِنَ الْآخَرِ قَالَ لَأَقْتُلَنَّكَ ۖ قَالَ إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّـهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ ﴿٢٧﴾

“Na wasomee (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) habari za wana wawili wa Aadam; kwa haki walipotoa qurbaan (dhabihu) ikakubaliwa ya mmoja wao, na haikukubaliwa ya mwengine; (asiyekubaliwa) akasema: “Bila shaka nitakuua.” (Aliyekubaliwa) Akasema: “Hakika Allaah Anatakabalia wenye taqwa.” [Al-Maaidah: 27]

 

(Aayah kuhusu kisa hicho zinaendelea hadi Aayah namba 31 Suwratul Maaidah).

 

Kwa mukhtasar, ni kuwa, Aadam na Hawwaa walikuwa wakizaa watoto mapacha na kila pacha lina mtoto wa kike na kiume, ili mtoto wa kiume wa pacha hili aweze kumuoa mtoto wa kike wa pacha lingine. Na hiyo ilikuwa ni shariy’ah ya wakati huo kuoana ndugu kwa ajili ya dharura ili kuweze kuendelea kizazi. Lakini baada ya kizazi chao kuwa kikubwa na kupanuka na kuwa ummah mkubwa, hakukuwa tena na haja hiyo ya kuoana ndugu, na shariy’ah hiyo ilikomea huko.

 

Shariy’ah yetu ni kwamba hairuhusiwi mtu kumuoa dada yake au Mahrim wake.

Hayo tumeeleza kwa ziada tu kama walivyotunukulia ‘Ulamaa mbalimbali, ikiwa kutazuka maswali kama hayo.

 

Na Allaah ni Mjuzi zaidi

 

 

Share