027-Aayah Na Mafunzo: Miongoni Mwa Hatari Za Kukata Undugu

 

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Miongoni Mwa Hatari Za Kukata Undugu

 

 

 Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٢٧﴾

27-Wale wanaovunja ahadi ya Allaah baada ya kuifunga Kwake na wanakata Aliyoyaamrisha Allaah kuungwa, na wanafanya ufisadi katika ardhi, hao ndio wenye khasara.

 

Mafunzo:

 

Makemeo makali ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yametajwa katika Qur-aan na Sunnah kwa mwenye kukata undugu. Baadhi yake ni kama kulaaniwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala):

 

فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِن تَوَلَّيْتُمْ أَن تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ﴿٢٢﴾

Basi huenda nyinyi mkigeuka ndio mfanye ufisadi katika ardhi na kukata jamaa zenu wa uhusiano wa damu?

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَىٰ أَبْصَارَهُمْ﴿٢٣﴾

Hao ndio ambao Allaah Amewalaani; Akawafanya viziwi na Akawapofua macho yao. [Muhammad: 22-23]

 

 Na baadhi ya Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 Jubayr bin Mutw‘im  (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba alimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Hatoingia Jannah mwenye kukata uhusiano wa damu.” [Al-Bukhaariy (5981)]

 

Na pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Hakika Allaah Ameumba viumbe mpaka Alipomaliza ulisimama undugu, ikasema; huyu amesimama anajikinga Kwako na anayemkata, Akasema ndio hivi huridhii Nikimuunga anayekuunga na Ninamkata anayekukata? Akasema sawa. Akasema hilo lako (umekubaliwa ombi lako).” [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Share